Home Habari MO DEWJI AJA NA MIKAKATI MIPYA SIMBA

MO DEWJI AJA NA MIKAKATI MIPYA SIMBA

385
0
SHARE

Achungulia mafaili ya AS Vita, Al Ahly

CLARA ALPHONCE NA SAADA SALIM

BILIONEA wa Simba, Mohamed Dewji, anaonekana kutoridhika na mwenendo wa kikosi chake kinachoshiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi na kusema kwamba safari yake iko palepale.

Mo Dewji amejikuta akipatwa na maumivu moyoni baada ya kushuhudia kikosi hicho kikichapwa jumla ya mabao 10-0 katika michezo miwili ya ligi hiyo na sasa anafikiria msimu ujao kufanya jambo la ziada.

Simba walifungwa na AS Vita ya DR Congo, mabao 5-0 mchezo uliochezwa Januari 19 mwaka huu ugenini kabla ya kupokea kipigo kama hicho dhidi ya Al Ahly Februari 2, nchini Misri ambapo Mo Dewji, hakufurahishwa na matokeo hayo.

Taarifa kutoka Simba zinadai kuwa bilionea huyo amechungulia mafaili ya Al Ahly na AS Vita kuangalia namna wao wanavyoweza kujiendesha kisasa na shughuli kamili itaanza msimu ujao baada ya kupata mbinu za wenzao waliopiga hatua.

“Unajua kama awali alivyosema anataka Simba iwe klabu kubwa, amegundua kuna kitu wenzetu wametuzidi baada ya kupata matokeo mabaya hivyo anafanya kila linalowezekana ili msimu ujao mambo yaende sawa,” alisema kigogo mmoja ndani ya timu hiyo.

Kigogo huyo aliliambia DIMBA Jumatano kuwa, bilionea huyo pia anafikiria kumwaga fedha za usajili kwa benchi lake la ufundi ili kama kuna mchezaji wamemwona mwenye uwezo mkubwa wamsajili.

“Yani anataka kuangalia mfumo mzima wa timu hizo kuanzia usajili na mambo mengine, anaposema anataka Simba iwe kama TP Mazembe si kwamba anafurahisha baraza, anasema kweli,” alisema.

Kwa upande wake, Mo mwenyewe akizungumzia matokeo yaliyopatikana katika michezo hiyo miwili dhidi ya AS Vita na Al Ahly, alisema ana imani kwamba nafasi ya kusonga mbele ipo wazi.

“Nina imani hata Roma haikujengwa kwa siku moja, hivyo Simba nayo itakuwa na mabadiliko na msimu ujao kuifanya tishio na iwe tayari kupambana na timu bora Afrika katika michuano mikubwa,” alisema.

Simba itajaribu tena bahati yake Fabruari 12, itakapo ikaribisha Al Ahly katika ardhi yake, mchezo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here