SHARE

NA NIHZRATH NTANI JNR

NDANI ya “Stadium of Light”, uwanja huu wenye uwezo wa kuingiza mashabiki wapatao 49,000, ni moja kati ya viwanja vikubwa vya soka nchini England.
Yapo majina mengi maarufu dimbani hapo yaliyopata kuimbwa kwa nyakati tofauti. Majina kama Charlie Buchan, hata Bobby Gurney yamekuwa katika vitabu vya historia uwanjani hapo. Uwanja huu unamilikiwa na klabu ya Sunderland.
Pamoja ya kuwapo kwa majina hayo, lipo jina moja tu katikati yao. Jina hilo limeandikwa kwenye kitabu cha historia ya klabu hiyo kwa wino wa dhahabu. Ni nani mtu huyu! Wajiuliza?

NI KELVIN PHILIPS
Mnamo mwaka 1999, wakati wa maandalizi ya kuanza msimu mpya wa Ligi Kuu ya England, kulikuwapo na mchambuzi mmoja maarufu aliyeitwa Rodney Marsh.
Mtu huyu aliamini kile akisemacho. Alimtabiria Kelvin Philips aliyekuwa mshambuliaji wa Sunderland wakati huo. Rodney Marsh aliwahi kusema waziwazi kuwa, Kelvin Philips asingeweza kufunga zaidi ya mabao sita mpaka mwisho wa msimu wa 1999/2000. Sote tukamuamini Rodney.
Kumbe ulikuwa mzaha mkubwa kwa Kelvin Philips. Kauli yake Rodney Marsh ikapenya katikati ya masikio ya Kelvin. Rodney Marsh akasikika.
Mpaka kufikia Mei, 2000, Ligi ikiwa imefikia tamati, hakuwa Allan Shearer, Dwight Yorke, Andy Cole wala Thierry Henry waliokuwa wakitisha enzi hizo aliyekuwa kileleni mwa wafungaji bora.
Jina la Kelvin Philips ndilo likawa linazungumzwa na kutawala kurasa za mbele za vyombo vya habari. Magoli yake 30 yalimpa tuzo ya mfungaji bora wa Ligi Kuu ya England msimu huo.

Iliwachukua miaka 15 kuja kuvunjwa kwa rekodi yake ya ufungaji bora wakati Harry Kane alipofanya hivyo akiwa Mwingereza mwingine baada ya Kelvin Philips kufanya hivyo. Kwa miaka 14 tuzo ilikuwa inachukuliwa na wageni pekee.
Mbali na tuzo hiyo, mabao yake hayo yalimpa tuzo ya kiatu cha dhahabu cha mfungaji bora Barani Ulaya. Akiwa Mwingereza wa kwanza na wa mwisho kufanya hivyo.
Kelvin Philips alitamba katikati ya Christian Vieri, Ronaldo De Lima, Rivaldo, Raul Gonzalez, Filipo Inzaghi na wengineo.
Ni wakati huo, Waingereza waliitangazia dunia na kumuita Kelvin Philips kama mtambo wa mabao. Hata wakafikia kukufuru kwa kusema ni muda tu kabla ya Kelvin Philips hajavunja rekodi nyingi za mabao ya mfalme wa soka Duniani, Edson Nascrimento “Pele” wa Brazil. Ulikuwa mzaha. Mzaha wenye kuchekesha.

Akiwa na miaka 27 tu wakati huo, Kelvin Philips aliishi katika ndoto zake. Alikuwa mfalme si tu Stadium of Light, bali Uingereza nzima.
Jina lake likaimbwa mithili ya mfalme. Msimu mmoja baadaye, sote tukala maneno yetu. Kelvin alikuwa mshambuliaji asiye na makali. Mwishowe akaliacha jina lake likitamba kwa msimu mmoja tu. Huzuni iliyoje!

JE, ULIKUWA NI UPEPO TU KWA MO SALAH KAMA ULIVYOMPITIA KELVIN PHILIPS?
Ni mapema kuanza kuhoji kiwango cha Mohamed Salah katika mechi nane tu baada ya kuanza msimu mpya. Lakini kiwango cha Mo Salah kinaanza kutupa wasiwasi kama anaweza kubadilika mbeleni.
MO Salah wa msimu huu ni tofauti na msimu uliopita. Mpaka sasa amecheza mechi 11 za mashindano yote, huku akiwa na mabao matatu tu.
Msimu uliopita Mo Salah aliweka rekodi ya kuwa Mwafrika wa kwanza kufunga mabao 30 kunako Ligi Kuu ya England ndani ya msimu mmoja tu, huku pia akiwa Mwafrika wa pili kutwaa tuzo ya mfungaji bora nyuma ya Didier Drogba.
Unapomtazama Mo Salah akiwa ndani ya jezi ya Liverpool msimu huu, ni kama anatuthibitishia kuwa tulikuwa tunafanya makosa kumuweka kando ya Lionel Messi na Cristiano Ronaldo.
Yuko wapi Mo Salah wa msimu uliopita? Ama pengine ni kama upepo uliowahi kumkumba Kelvin Philips na kutawala msimu mmoja na kisha akapotea?
Bila shaka, sitaki kuwa kama Rodney Marsh katika kumtabiria, ila ni ngumu mno kumuona tena Mo Salah wa msimu uliopita ndani ya msimu huu.
Muda utatupatia majibu sahihi ifikapo Mei mwakani. Anaweza kugeuka kuwa Kelvin Philips mpya. Tusubiri, nipo tayari kuyala matapishi yangu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here