SHARE

MAREGES NYAMAKA

Ushindi wa mabao 4-2 waliopata Simba dhidi ya Azam jana mchezo wa Ngao ya Jamii umeifanya timu hiyo kuanza kujikusanyia mataji kabatini mapema.

Kwa kutwaa taji hilo kunaifanya Simba kusaliwa na makombe manne ambayo imeapa kuyaweka kibindoni wakianza na lile la Ligi Kuu Bara, Ligi ya Mabingwa Afrika, Kombe la Mapinduzi na Kombe la FA (Azam Sports Federation Cup).

Kwa ushindi huo Simba imeandika rekodi ya kipekee kwa kuwa timu ya kwanza kutwaa Ngao ya Jamii kwa mara ya tatu mfululizo ambapo mara kwanza ilikuwa mwaka 2017, 2018 na 2019.

Utamu wa ushindi wa Simba jana umekolezwa na mabao ya timu hiyo yakifungwa na nyota wote wa kigeni, hatua inayothibitisha usajili walioufanya kwa maproo umeanza kuwalipa.

Katika mchezo huo, Azam ndiyo walikuwa wa kwanza kuzifumania nyavu za Simba dakika ya 13 kupitia kwa Shaban Idd Chilunda aliyefumua shuti kali la mguu wa kushoto na kupita kulia kwa kipa Beno Kakolanya.

Kuingia kwa bao hilo kuliwafanya Simba kucharuka na kuanza kulishambulia lango la Azam kama nyuki ambapo dakika ya 16, Sharaf Eldin Shiboubo, aliisawazishi timu yake baada ya kumtungua kipa Razak Abalora.

Shiboubo alipachika bao hilo kwa kichwa ukiwa ni mpira uliopigwa na Hassan Dilunga na kutemwa na Abalora na kumfanya Msudan huyo kukwamisha wavuni.

Wakati Azam wakiwa bado wanatafakari kufungwa bao hilo, dakika 22 ya mchezo wakajikuta wanapachikwa la pili likifungwa tena na Shiboubo ambaye alikuwa moto kwa safu ya ulinzi ya Wanalambalamba hao.

Kama Simba wangekuwa makini wangekwenda mapumziko na kapu la mabao kwasababu dakika ya 33, Dilunga akiwa amebaki na kipa wa Azam alishindwa kukwamisha mpira wavuni.

Nahodha wa Simba, John Bocco alishindwa kuendelea na mchezo huo kipindi cha kwanza tu baada ya kukaa katikati ya uwanja akiwa pekee yake na kuomba kutolewa ambapo nafasi yake ilichukuliwa na Clatous Chota Chama.

Wachezaji Frank Domayo na Joseph Mahundi wa Azam walilambwa kadi za njano na mwamuzi wa mchezo huo, Elly Sassi, kutokana na faulo zao kwa nyakati tofauti.

Hadi timu hizo zinakwenda mapumziko Wekundu wa Msimbazi walitoka wakiongoza kwa mabao 2-1.

Kipindi cha pili kilikuwa na mafanikio zaidi kwa Simba ambao walifunga mabao mengine mawili na kuwafanya kufikisha mabao 4-2.

Alikuwa mwamba wa Lusaka, Chama aliyefunga kwa umahiri dakika ya 57 akiwa  katikati ya mabeki wawili ambao aliwapiga chenga na kuuweka mpira kimiani.

Licha ya kufungwa bao hilo, Azam waliendelea kujenga mashambulizi ambapo dakika 78 kiungo mwenye nguvu za miguu, Domayo aliwainua mashabiki wa timu hiyo kwa kupachika bao kwa shuti kali kutoka umbali wa mitaa kadhaa na kumuacha Kakolanya akiusindikiza kwa macho wavuni.

Timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa zamu kila mmoja akitafuta bao lakini walikuwa Simba tena waliohitimisha karamu kwa bao lililofungwa na Francis Kahata dakika ya 84 kwa guu lake la kushoto.

Mabadiliko yaliyowafanywa na Azam kwa kumtoa Chilunda na kuingia Masoody Abdallah ‘Cabaye’, Kangwa akimpisha Chirwa, huku Ella Djodi akipishana na Idd Kipagwile, bado mlima ulikuwa mrefu kwao kuupanda.

Pamoja na ushindi mnono wa Simba, Meddie Kagere atakuwa anajilaumu sana usiku wa jana kutokana na kukosa nafasi lukuki ikiwamo dakika ya 71 akiwa yeye na Abalora, huku wakiwapo wachezaji wenzake watatu ambao angewapasia wakamalizia kilaini kabisa.

Kikosi cha Azam FC kilikuwa; Razak Abalora, Nico Wadada/Obrey Chirwa dk63, Bruce Kangwa, Oscar Maasai, Yakubu Mohammed, Frank Domayo, Emmanuel Mvuyekure/Abdulhaj Omar ‘Hama Hama’ dk74, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Shaaban Iddi Chilunda/Iddi Kipagwile dk69, Richard Djodi na Joseph Mahundi/Masoud Abdallah ‘Cabaye’ dk51.

Simba SC: Benno Kakolanya, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Erasto Nyoni, Pascal Wawa, Jonas Mkude, Deo Kanda/Miraj Athumani dk74, Sharif Shiboub/Gerson Fraga Vieira dk83, John Bocco/Clatous Chama dk27, Meddie Kagere na Hassan Dilunga/Francis Kahata dk59.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here