Home Michezo Kimataifa Mourinho ampa mapumziko Ibrahimovic

Mourinho ampa mapumziko Ibrahimovic

589
0
SHARE
Zlatan Ibrahimovic

MANCHESTER, England

KOCHA mkuu wa klabu ya Manchester United, Jose Mourinho, ameamua kumpa mshambuliaji wake, Zlatan Ibrahimovic, muda mrefu wa mapumziko ya kupisha mechi za kimataifa baada ya fowadi huyo kuonesha kiwango safi ndani ya mechi tatu za awali za Ligi Kuu England.

Ibrahimovic, 34, ameichezea United kwa dakika zote na kufunga jumla ya mabao manne ndani ya michezo minne tangu alipotua bure kwenye dimba la Old Trafford akitokea kwa mabingwa wa Ufaransa, klabu ya PSG.

Kutokana na hilo, Mourinho ameamua kuipumzisha ‘bunduki’ yake hiyo kwa kuipa siku mbili zaidi ya wachezaji wengine wa United ambapo kwa mujibu wa Mourinho, kwa umri wa straika huyo anahitaji mapumziko ya kutosha.

“Ni ngumu kwake (Ibrahimovic) kucheza mechi 70 kwa msimu mmoja. Kwa hiyo vijana wengine ambao hawajaitwa kwenye timu zao za taifa nimewapa siku mbili na yeye nimempa siku nne za kupumzika.

“Kwa umri wake wa miaka 34, anahitaji kupumzika vizuri. Siku za mapumziko nazitoa kwa mujibu wa mipango yangu na inategemea na hali halisi. Ibrahimovic atacheza katika kila mchezo na kila dakika.

“Amecheza mechi nne, hizo ni dakika 360, kwa hiyo atapumzika kwa siku nne.”

Licha ya kuwa na umri mkubwa huku akikabiliwa na jukumu la kuendana na kasi kubwa ya Ligi Kuu England, Ibrahimovic ameonesha uwezo wa hali ya juu ndani ya jezi ya United kwenye mechi za awali za msimu wa 2016/17.

Ibrahimovic alianza kuifungia United kwenye fainali ya Ngao ya Hisani dhidi ya Leicester City kabla ya kupachika bao kwenye mchezo wa kufungua ligi dhidi ya Bournemouth kwenye dimba la ugenini.

Alipachika mabao mengine mawili dhidi ya Southampton kabla ya kukutana na kizingiti cha Hull City wikiendi iliyopita, mchezo uliomalizika kwa United kushinda bao 1-0 lililofungwa na Marcus Rashford.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here