Home Michezo Kimataifa MOURINHO ANAVYOITUMIA UROPA KUFICHA UBOVU WA MAN UNITED

MOURINHO ANAVYOITUMIA UROPA KUFICHA UBOVU WA MAN UNITED

382
0
SHARE

MANCHESTER, England

JOSE Mourinho mjanja sana. Baada ya kuchungulia na kuona ni ngumu Manchester United kumaliza ligi ndani ya ‘Top 4’, ametangaza kuwa lengo lao kwa sasa ni kubeba kombe la Uropa.

Kesho watashuka Old Trafford kucheza nusu fainali ya pili dhidi ya Celta Vigo, huku sare yoyote kwenye pambano hilo itawahakikishia tiketi ya moja kwa moja kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa msimu ujao.

Lakini ni kweli lengo la Jose Mourinho lilikuwa ni Kombe la Uropa tu? Si kweli, Manchester United walihitaji kubeba mataji yote walioshiriki msimu huu ila ziko sababu zilizowafelisha.

Ufinyu wa mabao

Kwa kuzitazama timu sita za juu kwenye Premier League, United ndio wamefunga mabao machache zaidi mpaka sasa.

Arsenal wanaoshika nafasi ya 6, wamefunga mabao 66 huku United wanaoshika nafasi ya 5 wakifunga mabao 51. Kuna tatizo kubwa sana kwenye safu yao ya ushambuliaji msimu huu.

Zlatan Ibrahimovic ndiye kinara wa mabao ya United akifunga mabao 17 kwenye Premier League, lakini ndiye mchezaji anayeongoza kwa kulaumiwa na mashabiki.

Kwanini? Licha ya kufunga, Zlatan pia amekuwa na tatizo la kukosa mabao mengi ya wazi msimu huu.

Hizi hapa takwimu zake

Amepiga mashuti 46 yaliolenga lango kati ya majaribio 115 aliyoyafanya kwenye lango la wapinzani wake (Achana na mashuti 83 yaliyowabatiza mabeki).

Hii ni takwimu mbovu zaidi ukilinganisha na mastraika watatu bora msimu huu, Diego Costa, Harry Kane na Romelu Lukaku.

Ubutu wa mastraika wa United ndio sababu ya kwanza iliyoifanya Manchester United kupata sare nyingi dhidi ya timu ndogo msimu huu.

Wastani wao wa kupiga mashuti yaliolenga lango ni 9.06 ndani ya mashuti 563 waliyopiga. Ni Middlesbrough, Southampton na Sunderland pekee walio na wastani mbovu zaidi ya United.

Kukosekana kwa Plan B

Ibrahimovic ilikuwa Plan A, B na C kabla hajapata jeraha la goti, Manchester ilicheza kwa kumtegemea.

Msweden huyu ameanza michezo 27 ya Premier League kati ya 28 alipokuwa fiti, mechi nyingine alikosa akitumikia adhabu ya kufungiwa na FA.

Kwa miaka 35, ilikuwa ni jambo la ajabu kwa Jose Mourinho kumtegemea kwa michezo mitatu ndani ya wiki na hili lilifanyika kwa sababu hakukuwa na straika mwingine anayeaminika kwenye kikosi cha United msimu huu.

Wakati flani Ibrahimovic alionekana kukosa nguvu, kupooza na kupoteza nafasi nyingi za wazi kwa sababu ya kupoteza umakini.

Ni Marcus Rashford, kinda aliyecheza dakika nyingi zaidi msimu huu kwenye Premier League, ndiye aliyekuwa akipewa nafasi mara chache kucheza kama straika wa kati.

Kuogopa mechi kubwa

United hawajafunga bao dhidi ya timu sita za juu wakiwa kwenye viwanja vya ugenini msimu huu, labda kama watafanikiwa kufanya hivyo kwenye mchezo unaofata dhidi ya Tottenham.

Pia wamevuna pointi mbili tu wakiwa ugenini dhidi ya timu kubwa, wakipata suluhu mbili dhidi ya Liverpool na Manchester City.

Kwenye michezo hiyo miwili (Liverpool na Man City), United walipiga mashuti mawili tu yaliolenga lango ndani ya dakika 180 na kibaya zaidi walicheza soka la kujilinda kwa asilimia kubwa.

Dhidi ya Arsenal, vijana wa Mourinho walifanya mashambulizi japo hayakuwa ya hatari na walikuwa kwenye kiwango kibovu zaidi walipolala bao 4-0 mbele ya Chelsea, Oktoba mwaka jana.

Kukosa ari ya ushindi

Si kawaida kwa Man United kucheza bila kiu ya kupata matokeo, mara kwa mara hili limejitokeza kwenye michezo yao hasa wakiwa katika uwanja wao wa Old Trafford.

Mbinu pekee iliyowapa mafanikio msimu huu ni ‘mashambulizi ya kushtukiza’ na hili lilionekana mara nyingi kwenye mechi kubwa.

Dhidi ya timu ndogo walitumia muda mwingi kumiliki mpira huku wakikosa ari ya kulazimisha matokeo kama ilivyo desturi ya mashetani hao wekundu wa Old Trafford.

Antonio Valencia ndiye pekee aliyeonekana kuwa na kiu ya kulazimisha mashambulizi, mara nyingi amecheza kama winga wa pili wa upande wa kulia, jambo ambalo ni ngumu kuona likifanyika upande wa kushoto.

Juan Mata amezidi kuwa mtulivu mbele ya lango la wapinzani, Jesse Lingard kiwango chake kinapanda na kushuka huku fundi wa mpira kutoka Armenia, Henrikh Mkhitaryan, akidumu kwenye ubora wake kwa mwezi mmoja tu msimu huu.

Tofauti pekee ya uchezaji wa United chini ya Van Gaal na Mourinho, ni mmoja kumiliki mpira eneo lake la ulinzi na mwingine kuifanya timu yake icheze na mpira muda mwingi katikati ya uwanja.

Mpaka leo mashabiki wa Steford End hawajaiona Man United ile ya Sir Alex Ferguson ikicheza kwa amsha amsha ya kutaka matokeo.

Mipira ya adhabu

Ni klabu tatu tu ndizo zilizopata kona nyingi zaidi ya United wenye kona 208 msimu huu (Tottenham, Manchester City na Liverpool).

Lakini ni klabu moja tu (Middlesbrough) iliyofunga mabao mengi kwa mipira iliyokufa kulinganisha na United yenye mabao 10 (matatu kwa penalti na saba ya faulo).

United wamekuwa na wastani mbovu wa kufunga mipira ya kona na pengine ndio kazi kubwa ambayo Mourinho anatakiwa kuifanyia kazi katika dirisha la usajili.

Hivi karibuni Mourinho alinukuliwa akijibu kwanini Marcos Rashford amepewa jukumu la kupiga kona huku akisema: “Amekuwa akipiga kwa kasi kuliko wote. Wengine wanapiga vizuri lakini mpira unakuwa hauna kasi. Ni ngumu kufunga kwa kichwa kama kasi hiyo ya mpira.”

Kuna shida katikati ya uwanja

Paul Pogba hakuwa na kiwango kibaya lakini hakuwa na ubora unaoendana na thamani ya pesa ya usajili wake.

Ni mzuri kwa kupiga pasi, fupi kwa ndefu. Ni imara kwa kukokota na kumiliki mpira eneo la katikati, lakini amekuwa akilaumiwa kwa udhaifu wake wa kushindwa kufunga mabao nje ya eneo la 18.

Kumekuwa na lawama kuwa Pogba ameshindwa kung’ara kwenye mechi kubwa lakini wasifu wake akiwa Juventus unaonyesha kitu kingine tofauti. Kimsingi Paul anahitaji viungo wengine bora wa kumsaidia katikati ya uwanja.

“Watu wananizungumza sana, wananihukumu kwa kushindwa kwangu kufunga mabao,” alisema Pogba.

“Mimi nafanya kazi yangu. Natoa asisti kwa wenzangu na hawafungi, lakini watu hawazungumzi hili kabisa.

“Watu wananihukumu, Pogba anatakiwa kufunga, Pogba anatakiwa kufanya hivi lakini kama tungekuwa tunahesabu mabao kwa mipira iliyogonga mwamba sidhani kama ningekuwa kwenye lawama hii,” aliongeza.

Ubora wa wachezaji

Ukiondoa jina la Axel Tuanzebe, wachezaji wote walioanza dhidi ya Arsenal walikuwa wana hadhi ya kucheza Premier League, ishu za kikosi cha pili ni danganya toto tu.

Ukweli ni kuwa msimu huu wachezaji wengi wa United hawako kwenye viwango bora vya kucheza na kupata matokeo na hili ndilo limempelekea Mourinho kuchagua baadhi anaowaamini watampa ubingwa wa Uropa na kuwaamini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here