SHARE

MANCHESTER, England

KOCHA wa Manchester United, Jose Mourinho, amesema ana imani kuwa vijana wake watapambana na kuifikisha klabu hiyo kwenye nafasi nne za juu za Ligi Kuu England kufikia mwishoni mwa Desemba mwaka huu.

Kabla ya kuikaribisha Old Trafford timu ya Crystal Palace jana, kwenye mchezo wa Ligi Kuu England, klabu hiyo ya Man United ilikuwa inashikilia nafasi ya nane katika msimamo wa Ligi Kuu England.

Mourinho alikiri kuhusu pengo kubwa la pointi lililopo kati ya Man United na Man City, lakini aliweka wazi kwamba mechi za hivi sasa zitawasaidia kupanda juu katika msimamo wa Ligi Kuu England.

“Nafahamu kwamba tumeachwa mbali na Man City,” alisema Mourinho, kuelekea mtanange wao wa jana dhidi ya Crystal Palace.

“Lakini pia nafahamu tuna mechi za kutosha, kama nane hivi ambazo zitatusaidia hadi kufikia mwishoni mwa Desemba kupata angalau pointi 24 za kupanda juu zaidi katika msimamo,” alisema Mourinho.

“Ninachoamini lengo letu litatimia, ninayo imani hiyo,” aliongeza Mreno huyo mwenye umri wa miaka 55.

Ikumbukwe kuwa, United ilibamizwa mabao 3-1 dhidi ya Man City katika mtanange wao wa mwisho kabla ya kuingia kwenye mapumziko ya kimataifa.

Baada ya mchezo wa jana dhidi ya Crystal Palace, United itaikaribisha Old Trafford timu ya Arsenal, kwenye mechi kali ya Ligi Kuu itakayochezwa Desemba 5, kabla ya kuifuata Liverpool, wiki moja baadaye.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here