Home Makala MRISHO NGASSA: NIKO TAYARI KURUDI YANGA HATA BURE

MRISHO NGASSA: NIKO TAYARI KURUDI YANGA HATA BURE

6490
0
SHARE
NA SAADA SALIM    |   

NI ngumu sana kuuzungumza mpira wa Tanzania katika kipindi cha miaka 15 iliyopita bila kulitaja jina la Mrisho Khalfani Ngassa maarufu kama Uncle. Mtoto wa mchezaji wa zamani wa Pamba ya Mwanza na Simba SC ya Dar es Salaam, Khalfan Ngassa.

Ngassa alipata umaarufu mkubwa pale alipojiunga na Yanga mwaka 2006, akitokea katika klabu ya Kagera Sugar. Uwezo wake mkubwa wa kukokota mpira kwa kasi na kupiga mashuti makali langoni, umemfanya Ngassa kuwa mchezaji hatari kwa mabeki wa timu pinzani anazokutana nazo.

Akiweka historia ya kucheza katika klabu kubwa tatu jijini Dar es Salaam, Ngassa kwa sasa anakipiga ndani ya kikosi cha Ndanda ya mkoani Mtwara.

Mrisho alitua Ndanda akionekana anaelekea mwisho wa maisha yake ya soka, baada ya kushindwa kufanya makubwa akiwa na klabu ya Mbeya City.

Lakini katikati ya wiki hii, winga huyu aliyetamba pia akiwa na jezi ya Taifa Stars, alipindua mawazo ya mashabiki wengi baada ya kuonyesha kiwango kikubwa katika mchezo wa Ndanda dhidi ya Yanga, uliopigwa katika dimba la Nangwanda, mkoani Mtwara.

Tayari tetesi zinaonyesha kuwa viongozi wa Yanga wamefanya mazungumzo ya awali na Ngassa na endapo mambo yakienda kama yalivyopangwa, Wanajangwani hao wataliongeza jina lake katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwenye hatua ya makundi.

DIMBA lilimtafuta Ngassa na kufanya naye mahojiano rasmi kwa lengo la kufahamu ukweli wa ishu zake na kuhusishwa kurejea Yanga pamoja na maisha yake ya soka kwa ufupi.

DIMBA: Unazungumziaje Ligi Kuu msimu huu na misimu iliyopita?

Ngassa: Msimu huu ligi ngumu tofauti na uliopita, ambayo nilikuwa hapa nchini.

DIMBA: Unakitazamaje kikosi cha Ndanda kwa nafasi iliyopo sasa?

Ngassa: Kwa upande wangu nina imani na timu yetu ipo vizuri na kuendelea kubaki katika ligi msimu ujao.

DIMBA: Umekuwa ukihusishwa mara kwa mara na Yanga, je, ni kweli?

Ngassa: Ni kweli, ipo hivyo lakini kuna kizuizi kipo kuna siku nitakitaja.

DIMBA: Ni kizuizi gani hicho kilichofanya usisaini Yanga?

Ngassa: Kwamba bado sina uwezo, lakini toka nimefika Ndanda mechi zote nacheza kama nilivyokuwa Yanga, kwa mechi ya juzi naweza kusema sijacheza vizuri kwani mechi za nyuma kila mechi natengeneza nafasi 5 au 4.

DIMBA: Ni kweli dirisha dogo ulihitaji kujiunga na Yanga bure bila dau la usajili lakini bado ukawekewa kikwazo?

Ngassa: Ni kweli lakini kama nilivyokwambia awali wako watu walisema sina uwezo wa kucheza ndani ya kikosi cha timu hiyo.

DIMBA: Je, Yanga wakihitaji kukurudisha upo tayari?

Ngassa: Mpira ni kazi yangu muda wowote kama watahitaji nitakwenda.

DIMBA: Mashabiki wanaamini umri wako umeenda sana hivyo huwezi kucheza katika timu kubwa katika kiwango kile kile ulichozoeleka, unalizungumziaje hilo?

Ngassa: Sasa kama sina nafasi ya kucheza ndani ya kikosi chao, kila kukicha wananiulizia ili niende kuwa kocha wao.

DIMBA: Kwa Yanga ni mchezaji gani anakuvutia kucheza naye?

Ngassa: Nadhani kwa sasa ni Pius Buswita, yupo makini na anatulia anapokuwa uwanjani.

DIMBA: Umecheza ligi Oman na Afrika Kusini kati ya nchi hizo mbili ligi ipi ilikusumbua?

Ngassa: Afrika Kusini ligi ni ngumu sana, hakuna lele mama kule.

DIMBA: Kati ya hizi klabu mbili Simba na Yanga ipi unaipa nafasi ya ubingwa na kwanini.

Ngassa: Yoyote inaweza kuchukua kwa kuwa Simba, Yanga, Azam na Singida hazijapishana sana pointi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here