SHARE

NA CLARA ALPHONCE

BAADA ya kukosa uongozi kwa muda mrefu kufuatia kujiweka pembeni kwa Mwenyekiti wao, Yusuf Manji, Yanga leo inatarajia kupata mrithi wake katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika katika ukumbi wa Bwalo la Maofisa wa Polisi Oysterbay, jijini Dar es Salaam.

Katika uchaguzi huo, wanachama watatu tu, Profesa Mshindo Msola, Jonas Tiboroha na Lucas Mashauri ndio watakaogombea nafasi ya uenyekiti baada ya wenzao wawili ambao ni Eliud Mwanjala na Mbaraka Igangula kujitoa.

Nafasi ya Makamu Mwenyekiti itagombewa na wajumbe wanne, akiwamo Fredrick Mwakalabela, Janeth Mbena, Yona Kevela na Salum Chota.
Wanaogombea nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji ni Athanas Kazige, Benjamin Mwakasonda, Frank Kamugisha, Rodgers Gumbo, Ramadhani Said, Bahati Mwasena, Hamad Islam na Sylvester Haule.

Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ambao ndio wasimamizi, Ally Mchungahela, alisema kuwa maandalizi yote yapo sawa, hivyo anawaomba wana Yanga kujitokeza kwa vingi kuja kuchagua viongozi ambao wataisaidia Yanga kufikia malengo yao.

Januari 13 mwaka huu baada ya viongozi wao wengi kwenye kamati ya utendaji kujiuzulu, huku wakisubiri uchaguzi mkuu ambao ulitakiwa kufanyika mwakani, Januri 13 klabu hiyo ilitakiwa kufanya uchaguzi mdogo kwa ajili ya kuziba nafasi ya Mwenyekiti, Makamu pamoja na wajumbe waliojiuzulu, lakini walishindwa kufanya hivyo kutokana na baadhi ya wanachama kufungua kesi mahakamani wakidai ukiukwaji wa katiba.
Kutokana na hilo, Yanga sasa wameamua kuingia kwenye Uchaguzi mkuu moja kwa moja ili kupisha uchaguzi mkuu wa serikali utakaofanyika mwakani.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here