Home Michezo kitaifa MTIHANI WA AVEVA KULETA UMOJA

MTIHANI WA AVEVA KULETA UMOJA

857
0
SHARE

NA SAADA SALIM,

KIBAO kipya cha msanii Lameck Ditto ‘Ditto’, ambaye yupo katika Jumba la Kukuza Vipaji (THT) kiitwacho ‘Moyo Sukuma Damu’, ndiyo habari ya mjini kwa sasa.

Na ameweka wazi kabisa, kuwa kazi hasa ya moyo ni kusukuma damu ili isambae katika mfumo wa mwili wa binadamu. Lakini binadamu wameupa moyo kazi nyingi zaidi.

Kuna ambao wameupa moyo kazi ya kupenda wenzao na kwa matamanio yao ya kibinadamu, wanaulazimisha wakati mwingine kufanya kazi kwa haraka kuliko uhalisia wake.

Kama ambavyo wimbo umefanikiwa kubamba, katika mchezo wa soka, habari ya mjini kwa sasa ni pambano la mahasimu Yanga na Simba.

Wakati moyo ukipewa kazi nyingi tofauti na jukumu lake la msingi ambalo ni kusukuma damu, Simba na Yanga zinawapa wachezaji, viongozi na mashabiki wake kibarua kizito kuelekea mchezo huo.

Wababe hao watavaana Jumamosi ya wiki hii katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, vita kubwa ikiwa ni kuwania pointi tatu za Ligi Kuu Tanzania Bara.

Timu hizo zinakutana zikiwa ni takribani siku 46 zimepita tangu zilipovaana katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi kule Zanzibar.

Mtanange huo ulishuhudia Wekundu wa Msimbazi wakiibuka na ushindi wa penalti 4-2, mchezo uliochezwa katika Uwanja wa Amaan.

Katika mchezo wa mwishoni mwa wiki hii, mioyo ya mashabiki wa pande zote mbili itakuwa ikidunda kwa kasi kwa muda wote wa mchezo, hali ambayo kwa mtu asiyekuwa mvumilivu anaweza kupatwa na shinikizo la damu kama ambavyo imekuwa ikitokea kila timu hizo zinapokutana uwanjani.

Lakini pia, mchezo huo utakuwa mtihani mwingine kwa Rais wa klabu hiyo, Evance Aveva, ambaye huu ni mwaka wake wa nne tangu alipochaguliwa kuwa rais wa klabu hiyo. Kwa kipindi chote hicho, Simba imeshinda mara moja tu katika michezo iliyokutana na Yanga.

Ndani ya uongozi wake kulikuwa na matabaka, huku baadhi ya wanachama wakijiweka kando na kususia timu hiyo, kitendo ambacho kilisababisha madhara makubwa katika mwenendo wa kikosi chao.

Aveva aligundua tatizo kubwa lililokuwa likiwasumbua na alijaribu kutafuta dawa ya ugonjwa wa timu hiyo kuhakikisha inafanya vizuri na ikiwezekana kuwafunga wapinzani wao, Yanga.

Baada ya kuona umoja katika klabu hiyo umekufa, bosi huyo alijaribu kurejesha mshikamano huo ili kuleta hamasa kwa wanachama na kuhakikisha timu yao inafanya vizuri kwa msimu huu.

Jitihada zake zilionekana kuzaa matunda, kwani umoja huo uliirejesha Simba upya na hatimaye kuanza kufanya vizuri katika mechi za Ligi Kuu Bara.

Furaha ya mashabiki wa Simba ikarejea kwa kuishuhudia timu yao ikiibuka na ushindi katika kila mechi kabla ya kukwea na kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi.

Kwa bahati mbaya huenda mechi ya Jumamosi ikawa mtihani mwingine kwa Aveva. Hakuna ubishi kuwa Rais huyo ana kibarua cha kuhakikisha umoja aliourejesha klabuni hapo haupotei baada ya filimbi ya mwisho katika mchezo dhidi ya Yanga.

Kinachotia shaka ni ikiwa Simba itapata matokeo mabaya katika mchezo huo. Aveva atakuwa na mtihani mkubwa sana kuhakikisha timu yake inaibuka na ushindi ili kuendeleza mshikamano walionao sasa na kuhakikisha unaendelea kudumu na kuleta mafanikio, hasa katika kile wanachokihitaji.

Ikumbukwe kuwa, imekuwa ni kawaida ya mashabiki na wanachama wa klabu za Simba na Yanga kutibua amani iliyopo kwenye klabu zao pindi tu timu zao zinapopoteza mchezo wa mahasimu wawili hao.

Kwa kulizingatia hilo, si Aveva pekee, bali ni wajibu wa kila mdau wa Simba kuhakikisha umoja na mshikamano ulipo sasa klabuni hapo unaendelea hata kama timu yao itapoteza mchezo dhidi ya Yanga.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here