SHARE

LONDON, England

MAHUSIANO ya Chelsea na Maurizio Sarri yamevunjika, hakuna kingine kilichopo kati yao tena ila kumbukumbu kubwa ni ushindi wa taji la Europa ambalo liliwapa tiketi ya kufuzu kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Kuondoka kwa Sarri kuelekea Juventus, maana yake Chelsea wanahitaji mtu mwingine wa kukiongoza kikosi hicho huku kiungo wa zamani wa timu hiyo yenye maskani yake Stamford Bridge, Frank Lampard akitajwa kuchukua nafasi.

Chelsea na Lampard wana uhusiano mkubwa kati yao. Ni timu ambayo imemfanya kocha huyo wa kikosi cha Derby County mafanikio makubwa na kumtambulisha kama mmoja wa viungo bora nchini England na duniani.

Inaweza kushangaza Lampard yupo tayari kurejea Chelsea, maswali ni mengi kama hilo litatokea kweli, ataweza kufanya kazi ikiwa ana mwaka mmoja tu tangu aanze kazi ya ukocha? Tusubiri.

Hiyo haimaanishi kwamba Lampard hafai kuwa kocha wa Chelsea sababu ya uzoefu, muda unaweza kuhukumu kama akipatiwa kazi hiyo kwa ajili ya msimu ujao na kuendelea.

Chelsea wamempoteza mchezaji wao hatari kikosini, Eden Hazard, kikosi chao ni kikubwa lakini wachezaji wengi hawana uwezo wa kucheza kwa kiwango kizuri kila mwisho wa wiki.

Tatizo ni kubwa kwa upande wao, sababu hawana uwezo wa kusajili nyota wapya ndani ya kikosi hicho kutokana na kufungiwa kwa kushindwa kufuata sheria za usajili.

Hicho ni kitu ambacho Lampard alikifanya Derby, aliazima wachezaji kama Mason Mount na Harry Wilson kutoka Chelsea na Liverpool lakini pia alitoa nafasi kwa wachezaji chipukizi kama Jayden Bogle.

Aina hiyo ya mpira ndio Lampard ataifanya Chelsea na atahitaji timu yake icheze. Inahitaji nguvu kwa kila mchezaji kucheza soka analolihitaji kwa kasi kubwa huku wakicheza kwa kumiliki mpira.

Inawezekana akafanikiwa Chelsea sababu aina ya wachezaji aliokuwa nao Derby hawakuwa na uwezo mkubwa ila walijituma kwa kiasi kikubwa walipokuwa uwanjani.

Tuangalie jinsi Chelsea watavyojipanga chini ya kiungo wao wa zamani aliyekuwa akivalia jezi namba 8 kwa zaidi ya miaka 10.

FALSAFA YAKE NI IPI?

Kwanza kabisa, Lampard anapenda kutumia mfumo wa 4-3-3 kama alivyokuwa akicheza chini ya Jose Mourinho na Carlo Ancelotti, ni ngumu lakini alifanikiwa ndani ya kikosi cha Derby County.

Ingawa, mara chache amekuwa akibadilika kwa kutumia 4-1-4-1, kwa kuwapanga viungo wawili ambao watakuwa na kazi ya kuisukuma timu pinzani kutoka nyuma huku akisisitiza umiliki wa mpira.

Mount alikuwa mmoja wa viungo ambao walicheza michezo mingi, wala haitoshangaza kuona Ross Barkley kwenye machaguo yake au Danny Drinkwater ambaye kwa kiasi kikubwa amekuwa hatumiki ndani ya Chelsea tangu alipojiunga nao akitokea Leicester City.

Upande mwingine wa viungo wa Chelsea wapo akina Ruben Loftus-Cheel, nyota huyo wa England alionyesha kiwango kikubwa msimu uliopita kwa kucheza michezo mingi chini ya Sarri.

Pia, yupo chipukizi Callum Hudson-Odoi ambaye anatajwa kuchukua nafasi ya Hazard kikosini, ubora wake wa kukaa na mpira na kusumbua ngome za ulinzi za wapinzani umekuwa hatari zaidi.

Christian Pulisic ambaye ni moja ya wachezaji wenye vipaji vikuwa kwa sasa Ulaya kuna uwezekano akacheza nafasi ya winga wa kulia, nyota huyo wa Marekani alimaliza msimu wa 2018/19 vizuri akiwa na Borussia Dortmund lakini muda mwingi alikuwa mchezaji wa akiba.

Wengi wanasubiri kumwona jinsi gani atafanikiwa katika soka la England. Lakini jambo kubwa ni uwezo wake wa kupiga chenga na kutengeneza nafasi za mabao kwa washambuliaji.

Lampard kazi kubwa ambayo ataifanya ni kuhakikisha idara ya ushambuliaji inakuwa na uwezo mkubwa wa kufunga mabao ya kutosha kutokana na nafasi ambazo zitatengenezwa.

Kazi kubwa itakuwa katika idara ya ushambuliaji, Olivier Giroud hafiti, Michy Batshuayi ambaye alikuwa kwa mkopo ndani ya timu ya Crystal Palace aliweza kuthibitisha kwa kufunga mabao wakati yupo kwenye mkopo.

Yupo Tammy Abraham mwenye umri wa miaka 21, alikuwa straika tegemeo wa Aston Villa ambayo imefanikiwa kupanda Ligi Kuu kwa ajili ya msimu ujao.

Abraham alifunga mabao 25 katika michezo 37 huko kwenye Ligi Daraja la Kwanza England, akiwa na wastani wa 0.67 kwa dakika 90.

Alizaliwa kufunga mabao, ni hatari zaidi kutafuta nafasi akiwa katika eneo la wapinzani, pia, ni mchezaji ambaye anafanya kazi kubwa anapokuwa uwanjani kwa kusumbua mabeki kwa kukaba au kutengeneza nafasi.

Udhaifu mkubwa wa Abraham upo katika kuunganisha mashambulizi, si mzuri katika kutunza mpira kwa aina ya straika wa aina yake alitakiwa kutengeneza zaidi kwa ajili ya washambuliaji wenzake.

Hana rekodi nzuri katika eneo la mwisho la utengenezaji nafasi za mabao, yaani anazo 0.7 ndani ya dakika 90 alipokuwa Aston Villa msimu uliopita.

Kama Lampard akiweka mfumo ule alioutumia Derby ndani ya Chelsea, Abraham hatoweza kupata shida sana sababu kazi yake kubwa itakuwa kuitanua safu ya ulinzi kisha timu kutumia nafasi hiyo kufunga mabao.

Hiyo huwafanya mawinga kuingia ndani na viungo kuisukuma timu kwa nguvu kwa kupenyeza mipira kwenye nafasi hizo, Abraham atakuwa chaguo sahihi eneo hilo kwa kazi ya Lampard.

Hivyo ndivyo ushambuliaji utakavyokuwa. Nini tutarajie kwenye safu ya ulinzi? Vizuri, jambo kubwa zaidi ambalo litarudisha furaha kwa mashabiki wa Chelsea na wachambuzi wa soka duniani kote ni kurejeshwa kwa N’golo Kante katika eneo lake ambalo hulimudu vizuri kucheza.

Mshindi huyo wa Kombe la Dunia alikuwa mmoja wa viungo bora wakabaji duniani, lakini Sarri alikuwa na maono tofauti na Kante kwa kumtumia katika eneo la kulia la kiungo, hakuonekana kufanya vizuri kama ilivyotarajiwa na wengi.

Kama ilivyokuwa kwa Sarri, hata Lampard atahitaji kuona timu yake inatengeneza au kumiliki mpira kuanzia kwa kipa kuelekea kwenye ulinzi, nadhani bado nafasi ya Jorginho ipo katika kikosi cha kwanza ila inategemea jinsi atakavyotumika.

Jambo kubwa zaidi ni kuwafanya walinzi waanzishe mashambulizi, wakati yupo Derby County safu ya mabeki ilikuwa na uwezo wa kutunza mpira kisha kuanzisha mashambulizi kuelekea mbele.

Mpaka sasa safu ya ulinzi ya ipo hasa mabeki wa pembeni wa Chelsea wamekuwa hawana viwango vizuri au kuridhisha, japo si kwa kiasi kikubwa sana, Emerson atakuwa na nafasi kubwa mbele ya Marcos Alonso.

Cesar Azpilicueta anahitajika kucheza beki wa kulia lakini atakuwa na upinzani mzito kutoka kwa Reece James, huku David Luiz, Antonio Rudiger, Andreas Christensen, Kurt Zouma au Fikayo Tomori, hao wote wanagombania nafasi mbili za beki wa kati.

Ni kazi ambayo Lampard inabidi aifanye Chelsea kwa kutengeneza mfumo ambao utakuwa rafiki kwa ajili ya wachezaji wake, anaweza kutumia 4-2-3-1, ni mfumo ambao utafaa katika kikosi hiki cha Chelsea.

Hilo ni suala la wachezaji kuheshimu mbinu, kuwa tayari kujitoa kwa ajili ya Chelsea chini ya Lampard, makocha wengi hupata kazi kubwa hasa kuingiza falsafa zao kwenye timu kama ilivyokuwa kwa Sarri.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here