SHARE

NA NIHZRATH NTANI

MSIMU mpya umeanza kutimua vumbi katika viwanja mbalimbali ikiwa ni ligi inayotajwa kuwa bora zaidi ulimwenguni.

Hii ni ligi ya nchini Hispania ambayo kadiri siku zinavyozidi kwenda inazidi kuwa bora na kuupa nguvu ule msemo wa Kiswahili usemao ‘asiye na mwana abebe jiwe’.

Wiki iliyopita viwanja mbalimbali nchini humo viliwaka moto na baadhi ya viwanja vilitoa matokeo ya kushangaza.

Ukurasa huu kama ilivyo kawaida ni mahususi kwa ajili ya La Liga, ni kama umeanza tena kukuletea matukio mbalimbali na habari zinazohusiana na ligi hiyo kila Jumatano kupitia gazeti hili pekee.

Inshalaah! Mola akitujalia uzima tutakuwa hapa mpaka mwisho wa msimu huu.

Makala haya inajaribu kuchambua zile timu nne zinazopewa nafasi kubwa kufanya vizuri zaidi katika La Liga msimu huu.

 

BARCELONA

Wamewapoteza beki wake mahiri wa kulia, Dan Alves, huku pia wakiwapoteza Thomas Varmaelen aliyekwenda AS Roma kwa mkopo. Pia wameachana na Cristian Tello, Marc Batra, Sandro Ramirez, Adriano, Alen Halilovic pamoja na Alex Song, alikwenda Rubin Kazan. Huku kukiwa na taarifa za kukaribia kumuuza kipa wake mahiri, Claudio Bravo kwenda Manchester City.

Hata hivyo, mpaka sasa wameweza kufanya usajili wa wachezaji kama kiungo fundi wa Kireno, Andre Gomes, kutoka Valencia, Lucas Digne, Samuel Umtiti na kumrejesha Denis Suarez kutoka Villarreal. Huku wakikaribia kumtwaa kipa wa timu ya taifa ya Uholanzi, Jasper Cillessen, anayeichezea kunako klabu ya Ajax.

Pamoja na kuondokewa na wachezaji mahiri bado Barcelona wanapewa nafasi kubwa kuweza kutetea taji la La Liga msimu huu kutokana na uimara wa kikosi chake.

Kikosi cha Barcelona hakijafanyiwa mabadiliko makubwa zaidi ya kufufuka kwa kiungo fundi wa Kituruki, Ardan Turan. Kutamfanya kocha wa timu hiyo, Luis Enrique kuwa katika wakati mgumu katika kupanga kikosi chake.

Mechi yao dhidi ya Real Betis katika dimba la Nou Camp kwenye ushindi wa mabao 6 kwa 2 ni kama salamu kwa wapinzani wao wenye shauku ya kuwavua taji hili. Kiwango cha safu yao ya ushambuliaji katika usiku wa Nou Camp dhidi ya Real Betis ni kama mvua za rasharasha tu. Ni kama vita nyingine ya ufungaji bora imeanza rasmi.

Jumapili hii nyasi za uwanja wa San Mames zitawaka moto wakati Athletic Bilbao watakapoikaribisha Barcelona katika mechi inayotabiriwa kuwa yakuvutia kwa timu zote mbili.

 

REAL MADRID

Mabingwa hawa wa Ulaya  wameanza vyema msimu huu baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3 kwa bila kwa mabao mawili kutoka kwa Galeth Bale na moja kutoka kwa chipukizi wa timu hiyo mwenye kipaji cha kushangaza, Marco Asensio, dhidi ya Real Sociedad katika uwanja mgumu kabisa kwa timu ngeni kushinda nchini Hispania wa Anoeta.

Hali ya kiungo fundi wa Colombia, James Rodriguez, kuendelea kuichezea timu hiyo ikiwa shakani. Huku wakikabiliwa na kifungo cha kutofanya usajili kwa madirisha mawili ya usajili.

Real Madrid ni kama wako kimya katika kufanya usajili wa wachezaji wapya  kufidia watakapokuwa kifungoni. Ni kama wanaamini waliopo wanaweza kuleta kile wanachokihitaji na wakianza kuwa na imani na wachezaji wao kutoka kwenye shule yao ya kuibua vipaji vya wachezaji vijana ya Castilla.

Mpaka sasa wamefanikiwa kumrejesha Alvaro Morata kwa pauni milioni 25.50 kutoka Juventus. Ukiwa ndio usajili pekee waliofanya hadi sasa huku wakiwarejesha kundini beki wake, Fabio Coentrao, aliyekuwa Monaco na Marco Asensio kutoka Espanyol.

Huku pia wakiwaruhusu kuondoka Jese Rodriguez aliyeuzwa PSG, Denis Cheryshev aliyeenda Villarreal, Alvaro Medran huku Veterani Alvaro Arbeloa akistaafu. Mpaka sasa wameingiza pauni milioni 29.33 kutokana na mauzo ya wachezaji na wametumia pauni milioni 25.50. Kwa kipato cha Real Madrid ni kama hawajafanya usajili wowote ule.

Mechi yake inayofuata watakuwa nyumbani kwa mara ya kwanza kuwakaribisha Celta Vigo, Jumamosi. Huku kukiwa na taarifa ya kujumuishwa kwa Cristiano Ronaldo ambaye aliukosa mchezo wa kwanza kwa kuchelewa kujiunga kambini na wenzake baada ya mapumziko kutokana na majukumu makubwa ya timu ya taifa.

Bado Real Madrid wanapewa nafasi kubwa kuweza kutwaa La Liga msimu huu tangu walipofanya hivyo miaka minne iliyopita chini ya Jose Maurinho. Real Madrid wana wachezaji mahiri na wenye vipaji hasa sehemu ya kiungo ikiwa ni silaha kubwa kwao huku mabeki wa pembeni wakiwa hatari kwa muda wote kupeleka mashambulizi langoni mwa wapinzani.

 

ATLETICO MADRID

Timu bora isiyo na bahati tunaweza sema hivyo. Uwezo wao wa kujituma kwa dakika zote tisini. Huku uhamasishaji bora kabisa kutoka kwa kocha wao, Diego Simeone ni jambo linalokufanya uanze kuwapa nafasi ya kuweza kutwaa taji hili tangu walipofanya hivyo misimu miwili iliyopita.

Mpaka sasa wamefanikiwa kuwaleta mshambuliaji hatari, Kevin Gameiro, kutoka Sevilla. Wamefanikiwa kumleta winga, Nicolas Gaitan, Diogo Jota, Sime Vrsaljko pamoja na Alex Werner kutoka Ligi Daraja la Kwanza ya Segunda division.

Wamewapoteza Luciano Vietto aliyekwenda kwa mkopo Sevilla kama sehemu ya mauzo ya Kelvin Gameiro, pia wamemuuza Borja Baston. Huku wakiwa bado wanaweza kufanya chochote dirisha hili la usajili kabla ya kufungwa na wao kama ilivyo Real Madrid wakianza kutumikia adhabu ya kutosajili kwa madirisha mawili ya usajili.

Wameanza ligi kwa sare dhidi ya timu iliyopanda daraja ya Alaves nyumbani, Vicente Calderon. Si mwanzo mzuri kwa Atletico Madrid kwa timu inayopewa nafasi kubwa kumaliza utawala wa Barcelona katika La Liga kutokana na uimara wa kikosi chao.

Jumapili hii watakuwa ugenini katika uwanja wa manispaa wa Detarque kukabiliana na timu nyingine iliyopanda daraja ya Leganes. Ni mechi inayotabiriwa kuwa ya upande mmoja kwa Atletico kuzinduka.

 

SEVILLA

Naiona timu nyingine kabisa chini ya kocha mahiri, Jorge Sampaoli. Ametua klabuni hapo baada ya kuondoka kwa kocha, Unai Emery aliyeenda PSG.

Sampaoli ana kazi kubwa kuweza kufuta mafanikio ya Unai Emery aliyeiwezesha timu hiyo kutwaa mataji matatu mfululizo ya Kombe la Europa ligi na kuifanya klabu hiyo kuwa ndio mabingwa wa kihistoria wa michuano ya Europa.

Tayari amepiga mkwara huku akijinasibu kuwa ataanzia pale alipoishia mtangulizi wake kuweza kuiletea mafanikio makubwa Sevilla. Hata hivyo, wamewapoteza wachezaji wake muhimu kama Kelvin Gameiro, kiungo wake Coke, Ever Banega, Beto, Jose Antonio Reyes, Fernando Llorente, Ciro Immobile pamoja na Grzegorz Krychowick aliyeenda PSG.

Wamefanikiwa kuwaleta Franco Vazquez, Ganso kutoka Sao Paulo ya Brazil, Joaquin Correa, Wissam Ben Yedder, Hiroshi Kiyotake, Pablo Sarabia na Luciano Vietto .

Wameanza vyema baada ya kuishindilia Espanyol kwa kipigo cha mabao 6 kwa 4 huku ushindi huo ukichagizwa zaidi na wachezaji wapya waliowasili klabuni hapo msimu huu.

Kwa kiwango kile walichoonesha dhidi ya Real Madrid na Barcelona kwenye Super Cup, bila shaka macho na masikio yetu yanapaswa sana kuingalia klabu hii. Inaweza kushangaza wengi msimu huu. Jumapili hii watawafuata Villarreal katika dimba la El Madrigal ni moja ya mechi bora kabisa kuitazama.

1 COMMENT

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here