SHARE

NA ABDULAH MKEYENGE

EMMANUEL Okwi yuko zake Uganda kwa sasa. Ameenda kwao kujiaadaa na AFCON. Moja ya vitu alivyovibeba kutoka Tanzania kwenda navyo kwao ni mkataba wa Simba. Hajausaini bado.

Anatembea na mkataba huo. Ameubeba katika kibegi chake cha kuhifadhia nyaraka zake muhimu. Simba wamebaki kumshangaa. Kila walivyokumbuka jinsi walivyomalizana kiurahisi na kina Shomar Kapombe, Aishi Manula, John Bocco, wanakuna vichwa na kujiuliza inakuwaje Okwi anatembea na mkataba wao hajausaini mpaka sasa, kwanini?

Hili ni swali wanalojiuliza mabosi wa Simba maskani kwao Daraja la Salenda karibu na katikati ya Jiji. Kila jioni wanakutana pale kujiuliza swali hili, lakini hawapati jibu sahihi. Wamebaki kutazamana kama majogoo yanayopigana.

Okwi hajawahi kuwa mchezaji mwepesi katika masuala ya mkataba mpya. Ni ngumu kumpa mkataba mpya akausaini papo hapo akaachana na viongozi. Kuna vitu vyake lazima avihakikishe vimekwenda sawa. Kama havijakwenda sawa ndiyo anafanya hivi.

Anachokitaka Okwi kwa sasa ni kitu kimoja tu katika maisha yake. Anataka pesa. Kila inapofikia Desemba 25 anapoadhimisha kuzaliwa kwake, hamu ya pesa ndiyo inazidi kumpanda, hivyo hana haraka ya kuusaini mkataba wa Simba katika muda huu ambao anajua zimebaki siku chache fainali za AFCON zianze. Nani anayejua kitakachomtokea huko AFCON? Inabaki kuwa siri ya Mungu.

Kaizer Chief ni timu inayomuhitaji Okwi kwa muda mrefu sasa. Hii ni nafasi yake ya kucheza katika sehemu ya kujionyesha zaidi. Ndani ya AFCON Okwi anaomba afunge angalau mabao mawili. Ni idadi hii itakayobadili kila kitu. Ndani ya Simba ana uhakika wa asilimia 100.

Atakachokwenda kukifanya AFCON ni kujionysha kwa timu nyingine. Ni hiki tu, mambo yakiwa mazuri ataenda, yakiwa magumu atautoa mkataba wake na Simba atausaini msimu ujao tutamuona Taifa.

Katika Simba hii ambayo mshambuliaji Meddie Kagere ndiyo anayelipwa mshahara mzuri kuliko mchezaji mwingine, ulitegemea Okwi awe na sura gani anapoitwa mezani kujadili masuala ya mkataba mpya? Ilikuwa lazima hiki tunachokiona sasa tukione.

Okwi wa leo hadengui kama wakati ule. Akienda kwao anawahi kurudi. Amekuwa mtu mzima. Anajua anachokifanya. Akili yake imejikita katika masuala ya pesa, sio kuchelewa kurudi akienda kwao.

Huyu tunayemshuhudia sasa ni Okwi wa upande wa pili. Okwi huyu hawavutii wengi, anayewavutia wengi ni yule Okwi wa upande wa kwanza tunayemuona uwanjani akifunga mabao ya kideoni.

Okwi wa upande wa pili huwa anajielewa mwenyewe na nafsi yake. Akiwa katika upande huu haitaji mtu mwingine amuelewe. Akijielewa mwenyewe inatosha. Kazi ya mpira ni kazi ya muda mfupi, sio kazi ya muda mrefu kama kazi nyingine.

SHARE
Previous articleUSIKATE TAMAA
Next articleManara aingia chaka Taifa

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here