SHARE

NA ZAINAB IDDY

NI Jumatano ya pili ya Februari tunakutana tena kwenye safu ya Filamu za Kibongo na leo tukiitazama kazi nzuri inayoitwa ‘Najua kuoa.’

Filamu hii imechezwa na wasanii mbalimbali wakiwemo Rehema Ally ‘Riyama’, Amri Athumani  ‘Mzee Majuto’, Ally Nogi (aliyecheza nafasi ya mume wa Riyama) na wengineo wengi.

Inaanza kwa kuonyesha hali ya kutoelewana baina ya Riyama na mumewe (Nogi), jambo linalosababisha kushindwa kufanya jambo lolote lenye manufaa katika familia.

Riyama anaonekana kumchukia mumewe kutokana na tamaa  zake za kimwili baada ya kuvutiwa na  kijana kutoka mjini anayeitwa Hamza.

Hamza alikwenda katika kijiji anayochoishi Riyama kuwasalimia wazazi wake na katika pitapita yake anakutana  na Riyama.

Riyama anaonekana kumpenda kiasi cha kuwa tayari hata kuvunja ndoa yake ili wakaishi pamoja mjini.

Pasipo kujali nafasi ya mumewe, Riyama anaamua kuweka wazi mahusiano  yake na Hamza, jambo lililoleta gumzo kijijini kwao, huku kila kukicha akimfanyia mumewe visa mbalimbali kwa lengo la kutaka apewe talaka.

Mume wa Riyama  baada ya kuona hakuna maelewano mazuri  kati yake na mkewe, anaamua kwenda kwa mzee Majuto (Mzee wa kijiji) kuomba ushauri ambaye  naye anamwambia asiwe na haraka ya kuandika  talaka kwani dini haitaki hivyo.

Mume wa Riyama anaamua kumwambia ukweli mkewe kuwa yeye anajua kuoa hajui kuacha, jibu linalomchukiza Riyama na kumwahidi kumfanyia jambo litakalosababisha  aandike  talaka mwenyewe.

Siku moja mchana, Riyama anaingia jikoni kumwandaliwa chakula mumewe, aliporudi na kukikuta mezani kwanza alishangaa kwa kuwa si kawaida yake lakini hakutaka kuhoji na badala yake alikaa na kuanza kula.

Wakati anakula ugali, anagundua mboga  aliyopikiwa ni rosti la mdudu aina ya jongoo, ndipo anapomuita mkewe na kumuuliza kwanini ameamua kumfanyia  hivyo.

Bila kujali kuwa anayezungumza naye ni mumewe, Riyama  anamjibu  kwa dharau na kejeli huku akimtaka kama anaona kero amwandikie talaka ili akaanzishe maisha mapya na mwanamume anayempenda, kauli hiyo inamuumiza mumewe.

Kwa hasira anamtaka Riyama akalete karatasi  na kalamu ili amwandike  talaka anayotaka, kitu kinachomfurahisha na kwenda haraka kuvinunua.

Anaporudi na kumkabidhi, mumewe anaandika lakini kabla ya kumpa, anachukua kiberiti na kuichoma moto huku akimwambia kuwa hajui kuacha.

Riyama anachukizwa na jambo hilo na ili kumkomesha, anaamua kupanga njama za kumuua kwa kumuendea kwa mganga.

Huko akiwa na yule mwanamume anayempenda, wanapewa dawa na kwenda kuweka katika chakula na hatimaye mume wa Riyama anafariki.

Baada ya kifo chake, ndugu wanaingia na mashaka juu ya mabadiliko ya Riyama kwani siku chache anaenda kufunga ndoa na yule kijana anayempenda na hivyo familia ya Nongi nao wanakwenda kwa mganga.

Familia ya Nongi wanagundua ndugu yao kauawa na mkewe, nao wanaamua kulipiza kisasi kwa kumfanya mpenzi mpya wa Riyana kuwa chizi huku wifi yao wakimpa ulemavu wa kupooza mwili.

@@@@@@@@@@@@@@@

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here