Home Makala NANI MFUNGAJI BORA WA MUDA WOTE WA LIGI KUU SOKA TANZANIA...

NANI MFUNGAJI BORA WA MUDA WOTE WA LIGI KUU SOKA TANZANIA BARA?

1185
0
SHARE

SWALI: Naitwa Ramadhani au Ramizo wa Mbondole, Kivule naomba mnikumbushe mfungaji wa muda wote wa Ligi Kuu Tanzania Bara ni nani? 0628231622.

JIBU: Rekodi ya kufunga mabao mengi inashikiliwa na Mohammed Hussein ‘Mmachinga’, aliyefunga mabao 24 katika ligi hiyo mwaka 1994.

SWALI: Kwanza nakupongeza mtaalamu kwa majibu mazuri unayotupa katika ukurasa huu kila Jumapili, nina maswali mawili, kwanza; naomba unitajie kikosi cha timu ya taifa ya Ghana kilichofika robo fainali za michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2010 nchini Afrika Kusini. Swali la pili, nawaulizia wachezaji wawili wa zamani wa timu ya Yanga, Boniface Ambani na Ben Mwalala, wako wapi na wanafanya nini hivi sasa? 0715167039.

JIBU: Kikosi cha Ghana kilichocheza robo fainali ya Kombe la Dunia 2010 na kutolewa na Uruguay kwa penalti 4-2 baada ya sare ya bao 1-1 katika dakika 120 kilikuwa; Richard Kingson, John Paintsil, Hans Sarpei, Isaac Vorsah, John Mensah (nahodha), Anthony Annan, Samuel Inkoom (Stephen Appiah), Kwadwo Asamoah, Kevin-Prince Boateng, Asamoah Gyan na Sulley Muntari (Dominic Adiyiah).

Swali la pili, baada ya kustaafu soka la uwanjani, Boniface Ambani, kwa hivi sasa anainoa timu ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 ya AFC Leopards wakati Ben Mwalala yeye pia ni kocha anayeifundisha timu ya Nzoia United aliyoipandisha kucheza Ligi Kuu ya Kenya (KPL) msimu ujao.

 

SWALI: Najitokeza kwa mara ya kwanza nikiwa msomaji wa gazeti la Dimba, napenda kuwauliza walipo beki wa zamani wa timu ya Simba, Victor Costa ‘Nyumba’ na Christopher Alex Massawe? Ameuliza msomaji mwenye simu no 0754428482.

JIBU: Baada ya kustaafu soka, Victor Costa ‘Nyumba’ kwa hivi sasa anaishi Kitunda jijini Dar es Salaam akifanya shughuli zake za kibiashara, lakini Christopher Alex yeye ni marehemu aliyefariki Februari mwaka juzi mkoani Dodoma baada ya kuugua kwa muda.

SWALI: Naomba unitajie orodha ya wachezaji watano bora wanaoshikilia rekodi ya wafungaji wanaoongoza kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya (UEFA). Elikana Mathayo wa Dodoma. 0767008474.

JIBU: Straika wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo, ndiye anayeongoza kwa kufunga mabao muda wote katika michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya akiwa amecheka na nyavu mara 95 katika mechi 13, akifuatiwa na Lionel Messi ambaye ametupia mara 93 katika mechi 111, huku Raul akishika nafasi ya tatu kwa mabao 71 katika mechi 142. Ruud Van Nistelrooy alifunga mabao 56 katika mechi 73 wakati Thierry Henry alicheka na nyavu mara 50 katika mechi 112.

SWALI: Naomba leo niulize swali langu na mnijibu. Ni hivi, msanii Dully Sykes anayo studio ya muziki au hana? Na kama anayo inaitwaje? Jimi Kisutu 0652762813.

JIBU: Dully Sykes alikuwa na studio mbili, moja ikiitwa Dhahabu Studio na nyingine 4.12 studio. Lakini hivi karibuni aliamua kuibadilisha matumizi Dhahabu Studio ambapo sasa itakuwa ni Academy ya muziki, huku studio yake ya 4.12 ndiyo ambayo itakuwa inahusika na masuala ya kuandaa muziki.

SWALI: Mimi ni shabiki mkubwa wa Manchester United. Unaweza kunifahamisha historia fupi ya klabu hii imeanzishwa mwaka gani? Na pia katika historia yake iliwahi kufungwa na Arsenal bao 5-0 katika mechi za ligi au michuano yoyote ile? Naitwa Ally Shomari au Baba Man U. 0652748974.

JIBU: Manchester United ilianzishwa rami mwaka 1878, ikijulikana kama Newton Heath LYR Football Club na kubadilisha jina kuwa Manchester United mwaka 1902 kabla ya kuhamia Old Trafford mwaka 1910. Rekodi inayoonyesha Arsenal kuifunga Man United idadi ya mabao matano ni Aprili 23, 1960 iliposhinda 5-2 na Oktoba 21, 1961 ambapo iliibuka na ushindi wa mabao 5-1.

SWALI: Naomba kuuliza alipo mchezaji wa zamani wa Simba, Emmanuel Okwi, naitwa Manyama wa Dodoma Matumbulu. 0654556606.

JIBU: Emmanuel Okwi kwa hivi sasa anacheza soka la kulipwa katika klabu ya SonderjyskE ya Denmark alikohamia tangu mwaka juzi 2015.

SWALI: Namuulizia mshambuliaji wa zamani wa Simba, Dua Said. Naitwa Carlos Kato wa Cheyo, Tabora. 0684029515.

JIBU: Baada ya kustaafu soka, Dua Said aliamua kuwa mfanyabiashara jijini Dar es Salaam ambapo anamiliki malori ya kusambaza maji safi akiwa anaishi Tabata, jijini Dar es Salaam.

SWALI: Je, aliyekuwa straika wa zamani wa Arsenal, Thierry Henry, aliwahi kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa barani Ulaya alipohamia Barcelona? Ahsante kwa ufafanuzi. Ameuliza msomaji mwenye simu namba 0715913704.

JIBU: Thiery Henry alitua Barcelona kuanzia Juni 25, mwaka 2007 hadi 2010. Akiwa huko Barcelona iliweza kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa barani Ulaya Mei 27, 2009 baada ya kuichapa Manchester United mabao 2-0 yaliyofungwa na Samuel Eto’o na Lionel Messi. Katika mechi hiyo iliyopigwa katika dimba la Olimpico, jijini Roma Italia, Henry alichezeshwa kama winga wa kushoto ingawa alikuja kutolewa dakika ya 72 na kumpisha Seydou Keita.

SWALI: Naomba kuuliza, hivi Arsenal imewahi kuchukua Kombe la Ligi ya Mabingwa barani Ulaya? Naitwa Tamimu Huruka wa Mbagala, Dar es Salaam.

JIBU: Arsenal haijawahi kutwaa taji la michuano hiyo zaidi ya kuishia fainali mwaka 2006 ilipofungwa na Barcelona.

SWALI: Naomba kujua wachezaji wa Real Madrid na Barcelona waliotwaa tuzo ya mchezaji bora wa dunia kuanzia mwaka 1994-2015. Ni mimi Timothy Mlelwa a.k.a Mlelwa Jr wa Iringa. 0756013864.

JIBU: Kila timu imetoa wachezaji wanne waliotwaa tuzo hizo ingawa Barcelona wametwaa mara nyingi zaidi kwa maana ya mchezaji mmoja kutwaa tuzo hiyo mara nyingi. Waliotwaa kwa upande wa Barcelona ni Hristo Stoichkov 1994, Rivaldo 1999, Ronaldinho 2005 na Lionel Messi ambaye ametwaa mara tano katika miaka ya 1999, 2010, 2011, 2012 na 2015.

Kwa upande wa Real Madrid walioinyakua ni Luis Figo 2000, Ronaldo de Lima 2002, Fabio Cannavaro 2006 na Critiano Ronaldo aliyefanya hivyo mara tatu katika miaka ya 2013, 2014 na 2016.

SWALI: Naomba kujua kikosi cha Arsenal kilichochukua ubingwa bila kufungwa. Fred Gideon wa Banana, Dar. 0683681068.

JIBU: Kikosi hicho kilikuwa, makipa; Jens Lehmann, Graham Stack, mabeki; Ashley Cole, Martin Keown, Lauren, Gael Clichy, Sol Campbell, Efstathios Tavlaridis, Kolo Toure, Justin Hoyte, Frank Simek na Pascal Cygan.

Viungo: Ray Parlour, Giovanni van Bronckhorst (aliondoka), Edu, Patrick Vieira, Robert Pires, Fredrik Ljungberg, Gilberto Silva, David Bentley, Jerome Thomas na Cesc Fabregas.

Washambuliaji walikuwa Nwankwo Kanu, Jeremie Aliadiere, Michal Papadopulos, Francis Jeffers (aliondoka), Jose Antonio Reyes, Dennis Bergkamp, Sylvain Wiltord, John Spicer, Quincy Owusu-Abeyie na Ryan Smith.

SWALI: Mbona kila siku nikiuliza maswali yangu huwa sijibiwi? Hivi timu ya Simba iliyofika fainali za Kombe la CAF ilikuwa ni mwaka gani na ilikuwa chini ya uongozi gani na kocha yupi? Mshamu Tungupu wa Morogoro, Ifakara Town. 0783176411.

JIBU: Hatuna kawaida ya kutojibu maswali ila ukiona swali lako halijibiwi ujue zamu yako haijafika tu katika utaratibu wa kawaida. Kuhusu Simba iliyofika fainali ya Kombe la CAF, ilikuwa ni mwaka 1993 chini ya uongozi wa Amir Ally Bamchawi ambaye alikuwa ni Mwenyekiti, Makamu wake Saleh Ghulum, Katibu Mkuu alikuwa ni Privatus Mtemanyenje, Katibu Msaidizi Khalfani Matumla na Mweka Hazina alikuwa ni Ayoub Semvua.

SWALI: Timu ya kwanza kuichezea Cristiano Ronaldo wa Real Madrid ni timu gani? Naitwa Vicent Abdallah a.k.a. Chabo wa Mwandege 0782448255.

JIBU: Si nia yetu kutojibu maswali ya wasomaji wetu bali tunajibu maswali kulingana na jinsi yanavyokuja ingawa tuna changamoto ya maswali mengi kuliko ukubwa wa ukurasa wetu. Ronaldo alianza kuichezea kwanza klabu ya Sporting Lisbon ya Ureno aliyoichezea msimu mmoja tu wa 2002–2003 akahamia Manchester United 2003–2009 kabla ya kutimkia Real Madrid kuanzia mwaka 2009 hadi sasa.

SWALI: Naitwa Hassan Mzozo, nipo Tandale Muhalitan, naomba kujua tangu Yanga ianzishwe mwaka 1935 iliwahi kushuka daraja? 0620729158.

JIBU: Tangu Yanga ilipoanzishwa mwaka 1935 na kuanza kushiriki ligi ya taifa mwaka 1965, haijawahi kushuka daraja zaidi ya kutwaa taji la ubingwa mara 26 ikifuatiwa na mahasimu wao Simba waliofanya hivyo mara 19.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here