SHARE

MERSEYSIDE, Liverpool


HAKUNA ubishi, katika kipindi cha hivi karibuni mchezaji ambaye mashabiki wa Liverpool wanampenda sana ni kiungo wao Mbrazil, Philippe Coutinho.

Ni kwa sababu moja kuu, Coutinho ana kipaji cha kufurahisha sana cha kusakata soka.

Lakini, ndani ya muda wa miezi michache tu, mashabiki hao hao wameshahamisha mahaba yao na sasa hawasikii la kuambiwa kwa Sadio Mane.

Bila shaka sababu kubwa ya mahaba kuhamia kwa Mane ni sekeseke la Coutinho kuomba kujiunga na Barcelona, huku Mané akiwa hajawahi hata kumwambia Roberto Firmino kuwa amepachoka Liverpool.

Lakini pia, sababu nyingine ni jinsi gani Msenegali huyo anavyojituma vilivyo uwanjani kwa sasa, ukizingatia Coutinho hajacheza mchezo hata mmoja wa ligi msimu huu.

Lakini nani ambaye ni mchezaji bora wa Liverpool? Hebu twende sawa hadi mwisho wa makala haya.

Raundi ya kwanza: Ufungaji

Kitu cha kwanza kinachobadili mchezo ni mabao na mshambuliaji atajadiliwa kwa hoja hiyo, kwani ni uwezo wa thamani sana, na wote kwa pamoja, Mané na Coutinho wanao: Msimu uliopita wote walitupia mabao 13 ya ligi pekee.

Coutinho ana rekodi ya kufunga mabao mengi msimu uliopita nje ya boksi (6), lakini kwa upande wa uwiano mzuri kati ya mashuti na mabao, Mane ni mtu mwingine kabisa.

Msimu uliopita Coutinho alipiga mashuti 69 (ukitoa yale yaliyozuiliwa) na kufunga 13, uwiano wa asilimia 19. Si mbaya. Wakati mwenzake alifunga mabao 13 katika mashuti 38 tu na kuwa na uwiano wa 34%. Kitu kinachofanya Mane awe mshindi kwenye sekta hiyo.

 

Raundi ya pili: Ubunifu

Ni wazi jambo la pili muhimu baada ya ufungaji, ni kutengeneza nafasi kwa wenzako nao waweze kucheka na nyavu. Mchezaji mwenye uwezo wa kuona wapi ulipo uwazi wa kupenyeza mipira ya hatari au kupenya yeye kama yeye huwa ana umuhimu sana.

Mané na Coutinho ni wachezaji wabunifu, lakini Mbrazil ndiye mwenye balaa zaidi. Kwanza anaweza kucheza kama winga wa kushoto au kiungo wa kati, akiifanya Liverpool itulie. Msimu uliopita alitengeneza nafasi 65 na kutoa pasi saba za mabao, huku Mané akitengeneza 44 (asisti tano), pia akijaribu mipira ya mbali 16 na kufikisha saba. Ni kiungo mbunifu mzuri kabisa, ndiyo maana Barcelona wanamhitaji.

 

Raundi ya tatu: Kipaji

Kuna wakati mabao na asisti huwa hazitoshi. Kuna kitu cha ziada unatakiwa kuwa nacho, ambacho si kikubwa sana, lakini kiwafurahishe tu mashabiki.

Kuwa na kipaji cha kuibomoa safu ya ulinzi kwa kasi na chenga za mwili kwa wakati maalumu, Mane ni habari nyingine. Coutinho naye anaziweza, ila Mané ni mkali kwenye kubinua mipira, anaweza kukimbia na wachezaji hata watatu wa timu pinzani kwa kuwachanganya kama anakwenda kulia, kumbe anakuja kushoto bila kuupoteza mpira na anapoupoteza basi lazima awe amechezewa rafu.

 

Raundi ya nne: Ukabaji

Mané na Coutinho ni wachezaji wa kwanza wanaotakiwa kutimiza majukumu ya kukaba kuanzia kwenye maeneo yao. Hicho ni kitu muhimu sana ambacho kocha wa Liver, Jurgen Klopp, anataka kukiona. Wachezaji wote wacheze kwa umoja na kuchapa kazi haswa.

Nyota hao wawili kwa sababu ni wepesi, basi huwapa wakati mgumu sana mabeki wa upande wa pili na mwisho wa siku ‘huiba’ mpira na kusonga nao kwa kasi. Mané ni mzuri, ila Coutinho hapa ni bora zaidi, msimu uliopita alifanikiwa kupokonya mpira mara 23 na kuingilia mara 14 (Mané- 16 na nane).

 

Raundi ya tano: Umuhimu wa kiufundi

Kila mchezaji unayemuona katika kikosi cha Liverpool ana umuhimu wake wa kiufundi kutokana na mfumo anaoutumia Klopp. Ila ili mfumo ufanye kazi, inabidi wale muhimu zaidi wawepo.

Wakati Coutinho akiwa ni mchezaji mbunifu, kukosekana kwa Mané kipindi alipokwenda Afcon kulipelekea Liverpool iboronge sana. Licha ya Coutinho kuwepo, ila Mane ndiye muhimu na alishikilia kitu fulani ambacho hakuna yeyote aliyekuwa na uwezo wa kukifanya.

 

Matokeo ya mwisho

Sadio Mané 3-2 Philippe Coutinho

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here