SHARE

NA JOHANES RESPICHIUS

TANGU vita kuu ya pili ya dunia mwaka 1945, mataifa mbalimbali ulimwenguni yamekuwa na mikakati ya tofauti yenye lengo la kuhakikisha maisha ya mtoto wa kike yanakuwa salama na hatimaye kutimiza ndoto zake.

Kwa mantiki hiyo, Jumuiya za kimataifa zimekuwa zikilipa kipaumbele suala la haki za watoto hususani wa kike kupitia mikataba ya makubaliano ambayo imeridhiwa kuhusu haki za mtoto kama mkataba wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 1989 kufuatia tamko la haki za mtoto la mwaka 1959.

Ulianza kutumika kisheria mwaka 1990 katika zaidi ya nchi 20 zilizoridhia kabla ya Tanzania kuutilia saini mwaka 1991 na kuwa sehemu ya sheria za nchi. Mkataba huo umeeleza haki za mtoto katika kuishi, kulindwa, kuendelea na kushirikishwa, ukitanabaisha kuwa mtoto ni kila binadamu mwenye umri chini ya miaka 18.

Licha ya mikataba kimataifa kutambua mtoto yule mwenye chini ya miaka 18 lakini imeshindwa kutekelezwa kutokana na baadhi ya nchi nyingi kuwa na sera na sheria zinazokinzana hasa linapokuja suala la umri wa chini wwa kuolewa na uoa.

Mfano, sheria ya ndoa no.5 ya mwaka 1971 ya Tanznaia kifungu cha 13 na 17 inamruhusu mtoto wa kike kuolewa akiwa na umri wa miaka 14 kwa ridhaa ya wazazi na miaka 15 kwa ridhaa ya mahakama licha ya kuwa ni mtoto.

Hali inayochangia mimba na ndoa za utotoni kutokana na kupata ujauzito kabla ya umri wa miaka 18 jambo ambalo limekuwa likihatarisha maisha ya watoto hao kisaikolojia, kimwili na hata kusababisha vifo.

Hali ikoje

Takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) zinaonesha kila mwaka watoto wa kike milioni 7.3 wa chini ya miaka 18 duniani hupata mimba ambapo katika ukanda wa Afrika Mashariki Sudani kusini inaongoza kwa kuwa asilimia 52 ya mimba za utotoni, Uganda asilimia 40 na Tanzania asilimia 31 huku Niger ikiongoza Afrika kwa asilimia 64.

Utafiti wa Taifa kuhusu vichocheo na madhara ya Ndoa za Utotoni nchini Tanzania uliofanywa mwaka 2016 na Sera ya Utafiti kwa Maendeleo, REPOA, kwa kushirikiana na Children’s Dignity Forum (CDF), Foundation for Women Health Research and Development (FORWARD), Plan International na Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Idadi ya Watu (UNFPA) katika mikoa 10 yenye viwango vya juu, kati na viwango vya chini vya ndoa za utotoni.

Aidha, utafiti wa Demografia na Afya Tanzania wa 2016 (TDHS) unaonyesha asilimia 36 ya wasichana wenye umri wa kati ya miaka 20 na 24 waliolewa kabla ya kufikia umri wa miaka 18, huku Mkoa wa Shinyanga ukiongoza kwa asilimia 59, Tabora (58), Mara (55) na Dodoma (51) wakati ambapo Iringa na Dar es Salaam ikiwa na ueneaji mdogo kwa asilimia 8 na 17.

Lakini takwimu hizo za TDHS 2016 zinaonyesha ongezeko la asilimia tano ya ndoa za wasichana wenye kati ya miaka 15 na 19 ukilinganisha na za 2010 hali inayodhihirisha kwamba tatizo linaendelea kuwa kubwa hivyo mtoto bado yuko kwenye hatari kufikia ndoto yake.

Kwanini zinaendelea kuwapo

Umaskini umetajwa kama kichocheo kikuu cha ndoa za utotoni kwani familia nyingi zimekuwa zikiwageuza watoto wakike vitegauchumi hivyo kuamua kuwaozesha mabinti ili kuweza kupata mahari ambapo kwa kiasi kikubwa huwa ni fedha taslimu na mifugo. Hivyo uamua kumlazimisha binti aolewe ili wapate mahari bila kujali amelidhia au la.

Na utafiti huo unaonyesha kuwa kiwango kikubwa cha ndoa za utotoni ni miongoni mwa familia zenye kipato cha chini ya Sh 100,000 ambako katika mikoa ya Manyara na Mtwara ni asilimia 78, Tabora na Lindi (77) ikifuatiwa na Mara (74) na Iringa (72).

Aidha mila na desturi za utamaduni wa jamii zimeendelea kuwa changamoto kubwa ya ndoa za utotoni kupitia sherehe za kufundwa katika makabila mbalimbali, ngoma za kimila, ukeketaji wanawake nakadharika. Mfano ‘Samba’ na ‘Chagulaga’ za jamii ya wasukuma na Wanyamwezi zinazoongoza kwa ndoa na mimba za utotoni.

Taratibu ambazo uwaingiza wasichana kwenye umama kutokana na kupewa mafunzo ya utu uziwa wang’ali wadogo jambo ambalo husababisha kuanza kujiingiza katika masuala ya ngono na hatimaye kuolewa mwisho kuzaa wakiwa na umri mdogo.

Aidha, ukosefu wa fursa za elimu husababisha ndoa za utotoni… tafiti mbalimbali zinasema kwa kadiri mtoto wa kike anavyokaa kwa kipindi kirefu shuleni ana asilimia kubwa ya kukwepa ndoa na mimba za umri mdogo kwa sababu hutumia muda mwingi katika masomo hivyo ni vigumu kuingia katika vishawishi vya kuolewa au kupata ujauzito.

Lakini pia hatua ya Rais John Magufuli, kupiga marufuku kurudi shule kwa msichana aliyepata ujauzito akiwa shuleni, bila kujali changamoto anazozipa mtoto wa kike inaweza kusababisha kuendelea kuongezeka kwa mimba za utotoni. Kauli hiyo inapingana na Katiba ya Tanzania inayompa kila Mtanzania haki ya kupata elimu.

Suala ya ubaguzi wa kijinsia yaani kukosekana kwa sawa kijinsia na uwiano wa madaraka kati ya mwanamke na mwanaume majumbani, kwenye ngazi za maamuzi na taasisi mbalimbali linahamasisha ndoa za utotoni, kwa namna hiyo wasichana wanalelewa ili kuwa walezi na kufanya shuguli zisizokuwa na malipo jambo ambalo linawaondolea thamani ya kiuchumi huku wavulana wakichukuliwa kuwa wawekezaji wa kiuchumi ambao wataisaidia famalia kifedha.

Madhara yake

Kuna madhara mengi ya mtoto kuolewa akiwa na umri mdogo ukiachilia mbali mimba za utoto lakini kwa kiasi kikubwa wengi wanaozwa kwa wanaume wenye wakubwa ambapo kwa mujibu wa utafiti huo katika mikoa yote zaidi ya asilimia 50 ya ndoa za utotoni inahusisha wanaume ambao wasichana kwa umri wa miaka mitano hadi 14 kuliko wanaowaoa.

Hili limejitokeza hivi karibuni nchini, Sudan Kusini, msichana Noura Hussein (19) alihukumuhiwa kifo baada ya kukutwa na hatia ya kumuua kwa kumchoma kisu mumewe ambaye alilazimishwa na binamu yake kuolewa naye angali ana miaka 16 alipotaka kumlazimisha kufanya mapenzi (kumbaka).

Pia kuna umwezekano mkubwa wa kupata magonjwa ya uambukizo kwa ngono kama Ukimwi, vifo vya mama na mtoto, huzuni kihisia, kupata fistula, mimba kuharibika, shinikizo la juu la damu na matatizo mengine wakati wa kujifungua.

Mbali changamoto za kimaisha na afya, mara nyingi ndoa hizo uchangia watoto huacha shule hivyo kuwa na uwezekano mdogo wa kujiendeleza kitaalamu na stadi za ufundi… wananyimwa haki ya elimu na kiafya na hata haki ya kuamua waolewe na nani na lini pamoja na kuutawala mwili wao wenyewe.

Nini kifanyike

Margaret Mussai ni Mkurugenzi wa Idara ya Watoto kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, pamoja na kukiri ongezeko la ndoa za utotoni anasema kuwa Serikali inaendelea kufanya jitihada kuhakikisha tatizo hilo linatoweka.

Anasema utafiti uliofanywa na wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) unaonyesha ongezeko la asilimia 27 ya mimba za utotoni nchini kwamba kutokana na hali hiyo Asasi, taasisi na mashirika mbalimbali yanatakiwa kuungana kwa pamoja kupambana na hali hiyo.

“Ni kweli tatizo ni kubwa lakini Serikali haiwezi kutokomeza janga hili peke yake ndiyo maana tuliamua kuandaa mpango kazi wa kupamba na mimba za utotoni hasa kupitia kampeni ya ‘Mimi ni msichana Najitambua Elimu ndio mpango mzima’ iliyoanzishwa na wizara.

Aidha anasema hatua ya taarifa za Jeshi la Polisi mwaka 2017 kuonyesha kuwa yaliripotiwa matukio ya ukatili zaidi ya 13,000 ni hatua kuwa kwani inawezekana jamii imepata uelewa wa kutosha wa kuripoti vitendo hivyo vya unyanyasaji kwa watoto.

Kwa upande wake Meneja Programu za Mikoa na Afya ya Umma, Mamoletsane Khati kutoka Taasisi isiyo ya kiserikali yenye makazi yake nchini Zambia, Panos Institute Southern Africa (PSAf), anasema nchi nyingi kma Tanznaia ndoa za utotoni zinaonekana ni halali kutokana na kukosa sheria madhubuti zinazotaja umri wa chini wa kuolewa kuwa ni miaka 18.

Anasema sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 inayoruhusiwa wasichana kuolewa wakiwa na miaka 14 kwa ridhaa ya mahakama, wavulana lazima wawe na miaka 18 licha ya sheria nyingi kuzuia ndoa za utotoni hivyo sheria hiyo haifai tena ni kandamizi.

Aidha jamii ielimishwe kuhusu athari mbaya za ndoa za utotoni ili kuelewa ndoa hizo sio suluhu ya umaskini hivyo ziangalie namna nyingine ya kuweka mikakati ya kufanya shughuli nyingine za kuzalisha kipato.

Pia ni vyema serikali ikalipa kipaumbele suala la elimu kwa mtoto wa kike hasa kuwaruhusu waliopata ujauzito wakiwa shule kurudi katika masomo yao kwani wengi wao wanafanya hivyo wakiwa katika umri mdogo ambao anakuwa bado hajawa na ufahamu au nguvu ya kujiamulia jambo. Alikadharika elimu ya afya ya ujinsia na uzazi iendelee kutolewa kwa kiasi kikubwa kwa wasichana mashuleni.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here