SHARE

SANTA CATARINA, Brazil

‘OH JESUS’ ni neno la mwisho alilolitoa rubani Miguel Quiroga kwa mwongoza ndege wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jose Maria Cordova.

Hii ni kabla ya ndege ya Shirika la Ndege la LaMia iliyokuwa imewabeba wachezaji wa klabu ya soka ya Chapecoense kuanguka kwenye milima ya mji wa Medellin, nchini Colombia.

Quiroga alitoa kauli hiyo ya kukata tamaa baada ya kuambiwa kuwa ndege yake ilikuwa umbali wa maili 8.2 kutoka kwenye Uwanja huo wa ndege, huku mafuta yakiwa yamemuishia na akiwa hana uhakika tena wa kumaliza safari hiyo salama.

Rubani huyo, ambaye pia ni sehemu ya wamiliki wa ndege hiyo, anatajwa kuwa chanzo cha ajali hiyo kutokana na uamuzi wake wa kutosimama kujaza mafuta katika mji wa Cobija, nchini Bolivia kama ilivyokuwa imepangwa, kitendo kilichosababisha ndege hiyo kuishiwa mafuta angani na kuanguka.

Ajali hiyo iliyotikisa ulimwengu wa soka imesababisha vifo vya watu 71, kati yao wamo waandishi wa habari za michezo, wachezaji na viongozi wa timu ya Chapecoense ya nchini Brazil ambayo ilikuwa ikienda kucheza fainali ya michuano ya Copa Sudamericana dhidi ya Atletico Nacional ya Colombia.

Lakini, licha ya ajali hiyo kusababisha vifo vingi, bado kuna watu sita waliopona kwenye ajali hiyo na kati yao wapo wachezaji watatu wa Chapecoense ambao bado wako hospitali kutokana na hali zao kuwa si nzuri.

Kwa upande wa wachezaji waliofariki ni pamoja na kipa namba moja Marcos Danilo Padilha (31), mabeki Filipe Jose Machado (32), Willian Thiego de Jesus (30), Guilherme Gimenez de Souza (21), Dener Assuncao Braz (25), Marcelo Augusto Mathias da Silva (25), Mateus Caramelo (22).

Viungo Cleber Santana Loureiro (35), Sergio Manoel Barbosa Santos (27), Matheus Biteco (21), Jose Gildeixon Clemente de Paiva (29), Josimar Rosado da Silva Tavares (30), Arthur Brasiliano Maia (24); Washambuliaji Bruno Rangel (34), Tiaguinho (22), Lucas Gomes da Silva (26) Everton Kempes dos Santos Goncalves (34), Ananias Eloi Castro Monteiro (27) na Ailton Canela (22).

Licha ya kuondokewa na idadi kubwa ya wachezaji, bado timu hiyo ina wachezaji tisa ambao hawakuwa safarini kutokana na sababu mbalimbali, hivyo wamepona, ukiongeza na wale watatu waliopona kwenye ajali jumla wamebakia wachezaji 12 katika kikosi hicho cha Chapecoense.

Makala haya yanakuletea sababu za kusisimua zilizosababisha wachezaji hawa tisa wasisafiri na wenzao kwenda kwenye mechi hiyo muhimu kwa historia ya klabu yao na hatimaye kuokoka na ajali iliyowakuta wenzao.

Walionusurika

Jakson Ragnar Follmann, 24, (kipa)

Follmann anatajwa kuumia vibaya zaidi ya majeruhi wote waliookolewa, lakini ripoti ya madaktari inasema anaendelea vizuri tangu alipofika hospitali.

Kipa huyu mwenye miaka 24 amekatwa mguu mmoja na kuna uwezekano mkubwa wa kukatwa na mguu wa pili unaoonekana kuumia vibaya.

Baba yake, Paulo, alisema alipokuwa akihojiwa na waandishi wa habari wa Brazil, “Kwa namna ajali ilivyokuwa, uwezekano wa kuamini kama kuna watu wengeweza kupona ulikuwa mdogo sana. Lakini mwanangu ametoka hai kwa nguvu zake Mungu.”

Alan Luciano Ruschel, 27, (beki wa kushoto)

Ruschel amefanyiwa operesheni ya uti wa mgongo punde tu baada ya kufikishwa hospitali.

Taarifa ya klabu inasema beki huyu amepoteza mawasilano ya mwili wake kati ya sehemu za juu na chini, lakini bado madaktari wanapambana ili kumuokoa asiweze kupooza.

Mchumba wake, Marina Storchi, alisema kuwa alishindwa kusafiri na mpenzi wake kwa sababu pasi yake ya kusafiria ilipotea kwenye mazingira ya kutatanisha nyumbani kwao.

Helio Hermito Zampier Neto, 31, (beki)

Neto bado yuko kwenye chumba cha watu mahututi akiwa na majeraha makubwa kwenye fuvu la kichwa, koromeo na mapafu.

Kwa mujibu wa taarifa ya klabu, beki huyu alikuwa mtu wa mwisho kuokolea kutoka kwenye ndege, anaendelea na matibabu na kuna uwezekano mkubwa wa kupata nafuu japo anaweza asicheze tena soka.

Hawa hawakusafiri na timu, unajua kwanini?

Miongoni mwa picha iliyoumiza wengi kwenye mitandao ya kijamii ni ile iliyoonyesha wachezaji watatu wakiwa kwenye vyumba vya kubadilishia nguo na taarifa zikasema kuwa hawakusafiri na timu.

Lakini ukweli wa taarifa ya klabu hiyo unasema kuwa ni wachezaji tisa ambao hawakusafiri na timu nchini Colombia.

Nao ni Alejandro Martinuccio, Nenem, Demerson, Marcelo Boeck, Andrei, Hyoran, Nivaldo, Moises na Rafael Lima.

Kipa Marcelo Boeck hakusafiri na timu kwa sababu aliomba abaki nyumbani asherehekee siku yake ya kuzaliwa.

Wakala wa kipa huyu aliweka wazi kuwa ni kawaida kwa Boeck kusherehekea birthday yake na ndugu zake, hivyo klabu ikaona hamna shida, ikamruhusu abaki Brazil.

Alejandro Martinuccio kwa upande wake alitakiwa kuwemo kwenye safari, lakini aliachwa dakika za mwisho baada ya kupata majeraha.

Kipa mkongwe Nivaldo kwa upande wake hakuchaguliwa kwenye safari kwa kuwa aliomba abaki nyumbani ili aweze kujiandaa kucheza mchezo wake wa 300 wa ligi, uliokuwa uchezwe leo dhidi ya Atletico Mineiro.

Baada ya ajali, kipa huyu mwenye miaka 42 aliamua kustaafu soka, lakini baadaye alibadili maamuzi na kupanga kucheza mchezo wa mwisho kwa ajili ya kuwaaga rafiki zake.

“Najua wanataka tucheze mechi moja ya kuwaaga,” alisema kipa huyo. “Kiukweli sijui namna nitakavyokuwa uwanjani na mashabiki wakianza kutaja jina moja moja la marafiki zangu waliokufa, itakuwa ngumu sana lakini ni lazima tucheze pambano hilo la mwisho.”

Matheus Saroli, mtoto wa kocha wa Chapecoense, Luiz Carlos Saroli, naye ni miongoni mwa watu waliotakiwa kuwa kwenye msafara, lakini alibaki baada ya kupoteza pasi yake ya kusafiria.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here