Home Habari NGOMA, PLUIJM SIRI NZITO

NGOMA, PLUIJM SIRI NZITO

267
0
SHARE
Hans van der Pluijm

NA EZEKIEL TENDWA,

WAKATI Singida United wakiendelea kufanya usajili wao wa wachezaji wa kimataifa kwa ajili ya kujiwinda na Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu ujao, siri nzito imegundulika kati ya Kocha Mkuu wa kikosi hicho, Hans van der Pluijm na straika wa Yanga Mzimbabwe, Donald Ngoma.

Singida United, ambayo imepanda daraja msimu huu baada ya kusota kwa muda mrefu, imeanza kufanya usajili wa fujo, ikiwa ni muda mfupi tu baada ya kumnyakua Pluijm kutoka Yanga na kisha kuwasajili nyota wengine kutoka Zimbabwe ambao ni Elisha Muroiwa na Wisdon Mussa.

Timu hiyo imemchukua Pluijm kwa msaada mkubwa wa Waziri wa Mambo ya Nje ya Nchi na Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba, ambaye anamhusudu sana kocha huyo kutokana na kazi yake nzuri aliyoifanya akiwa na Yanga.

Kocha huyo baada ya kupewa tu mkataba wa miaka miwili, haraka sana akapendekeza wasajiliwe wachezaji hao kutoka Zimbabwe, akiamini kuwa wanaweza wakawasaidia msimu ujao kuipaisha timu hiyo.

Sasa sikia hii. Taarifa za ndani kabisa zinadai kuwa, Pluijm amewapata wachezaji hao kutokana na msaada mkubwa wa Straika wa Yanga, Donald Ngoma, ambaye ni raia wa Zimbabwe, kutokana na urafiki wa wawili hao.

Kama ulidhani hiyo inatosha utakuwa upo nyuma, kwani taarifa nyingine zinadai kuwa, kama Yanga wataendelea kujivuta wakati huu mkataba wa Ngoma ukielekea ukingoni, wanaweza wakajikuta wanampoteza mchana kweupe.

Taarifa hizo zinadai kuwa, Pluijm anavutiwa sana na uchezaji wa Ngoma, hivyo anaweza akamsajili, kwani kikosi chake hicho kipya, fedha kwao si tatizo na kiburi hicho wakikipata kutokana na uwezo wa Waziri Nchemba, ambaye amedhamiria kuinua Soka la Singida.

DIMBA lilifanya jitihada za kumtafuta Waziri Nchemba, ili kuzungumzia suala hilo la yeye kuhusishwa na kumwaga fedha za usajili kwa kushirikiana na uongozi na matajiri wengine wenye mapenzi mema na timu hiyo kwa ajili ya kufanikisha usajili wa Ngoma, lakini simu yake haikupatikana.

Hata pale alipotafutwa Pluijm ili kuzungumzia uswahiba wake na Ngoma, kama inaweza kuwa chanzo cha yeye kutaka kumvuta kwenye makazi hayo mapya, hakupatikana ambapo taarifa zinadai kuwa yupo nje ya nchi kwa mapumziko ya muda.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here