Home Michezo Kimataifa Ni kweli Zidane alikuwa anabebwa na Ronaldo Madrid?

Ni kweli Zidane alikuwa anabebwa na Ronaldo Madrid?

1641
0
SHARE

MADRID, Hispania

ZINEDINE Zidane atafanikiwa kuitambua timu yake aliyoiacha kwa kipindi cha miezi tisa iliyopita? Ni kama mzazi aliyekwenda sokoni kununua vitu, lakini ghafla watoto wameharibu kila kitu, huwezi kukasirika ila utaumia moyo kwa masikitiko.

Zidane aliondoka Real Madrid huku akiacha mafanikio tele ndani ya kikosi hicho katika zama hizi ngumu za sasa, ilikuwa ngumu kutetea mataji makubwa, lakini alifanikiwa kufanya hivyo Ulaya kwa kushinda mataji matatu mfululizo ya Ligi ya Mabingwa.

Jambo usilolijua ni kwamba, Zidane alifanikiwa kushinda mataji hayo makubwa pengine kuliko hata muda ambao alikaa ndani ya kikosi hicho mpaka alipoondoka Santiago Bernabeu, alikaa kwa miaka miwili na nusu, lakini alishinda mataji matatu ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Lakini mambo yalianza kubadilika tangu pale alipoondoka, taji la UEFA Super Cup lilitua mikononi mwa wapinzani wao, Atletico Madrid, huo ulikuwa mchezo wa kwanza wa Julien Lopetegui, ambaye alifukuzwa Oktoba mwaka jana kwa matokeo mabaya.

Anga jeusi na ukungu uliotanda ndani ya Santiago Bernabeu ulipelekea timu hiyo kupoteza matumaini ya kutwaa taji la Ligi Kuu ya Hispania, La Liga, mapema sana.

Hivi karibuni walikuwa kwenye hali mbaya baada ya kukubali vichapo mfululizo kutoka kwa Barcelona, huku wakiondolewa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya katika hatua ya 16 bora na Ajax.

Kama Zidane akifanikiwa kurudisha hali ya ushindi, atakuwa amefanya maajabu kweli, atakuwa mtu wa ajabu ambaye amerudisha furaha iliyopotea kwa miezi tisa kiasi cha makocha wawili tofauti kuondoka kwa kushindwa kufanya hivyo.

Wakati kocha huyo raia wa Ufaransa anaondoka ndani ya kikosi cha Real Madrid alisema kuwa haamini kama anaweza kuwafundisha wachezaji hao tena, huku akidai kuwa nyota hao wanahitaji sauti mpya.

“Nafikiri ni muda sahihi, wachezaji wanahitaji mabadiliko, unaangalia na kutambua kuwa mambo yanatakiwa kubadilika,” alieleza Zidane.

Lakini imebainika kuwa kocha huyo alikuwa anajua matatizo ambayo yanaweza kutokea huko mbele, hasa kwa wachezaji wake kushindwa kuwa kwenye viwango vya juu.

“Sina hakika kwa asilimia 100 kama tunashinda michezo yetu kwa njia inayotakiwa, nafikiria kuondoka sababu itakuwa ngumu kushinda mataji, tumeliona hilo kwenye La Liga na Copa del Rey msimu huu (uliopita), kumekuwa na milima na mabonde,” aliongeza Zidane.

Zidane ni mtu mwenye maono kama mchezaji, wala hawezi kufumbia macho jambo ambalo litaharibu kazi yake, Real Madrid ni kikosi kilichojaa wachezaji wenye umri mkubwa na jambo muhimu kwa wote, Cristiano Ronaldo aliondoka na kujiunga na Juventus.

Real Madrid ilikuwa timu ambayo ilijaa matukio matamu, lakini ilikuwa ngumu kufanya maajabu kila mwisho wa wiki, hawakuwa kwenye mwendelezo wa kiwango kizuri.

Msimu uliopita walimaliza nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu, La Liga, yaani pointi 17 pungufu kwa vinara waliotwaa taji hilo, Barcelona.

Hiyo ilikuwa moja ya sababu ambayo ilimfanya akaondoka, lakini ni sababu ambayo inamfanya kwanini arudi tena ndani ya kikosi hicho. Je, atafanikiwa?

Kwa sasa hatuwezi kuzungumzia kuhusu Zidane kupeleka mataji ndani ya klabu hiyo ikiwa tayari wapo kwenye hali mbaya ndani ya La Liga, huku siku kadhaa zilizopita wakitolewa kwenye Ligi ya Mabingwa na Copa del Rey.

Zimebaki mechi 12 kabla ya La Liga kumalizika, lakini kubwa linaloonekana ni Real Madrid kufanya vizuri ili kumaliza juu ya Alaves wakiwa na faida ya pointi 10, wameshuka ghafla, ilikuwa ngumu kwa Solari, sasa tumsubiri Zidane.

Pamoja na hayo yote kutokea, kubwa ambalo linatazamiwa ni jinsi gani kocha huyo ataweza kukiongoza kikosi hicho bila uwepo wa Ronaldo, ambaye alifanya kazi kubwa ya kufunga mabao kwa kipindi chote alichokuwapo Zidane.

“Nahitaji wachezaji kufanya vizuri uwanjani, huwa napenda kuona wakipambana na kushinda, sasa nitafanya nini ikiwa tayari wamenilipa nilichohitaji,” aliwahi kusema Zidane.

Baada ya wiki ya mechi mbili za El Clasico na moja ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, ndoto zao zilifutika, huwezi kuficha kitu. Je, Zidane atakuwa shujaa wa Real Madrid kwa mara nyingine bila Ronaldo?

CHEKI REKODI ZA RONALDO CHINI YA ZIDANE

Kwa mara ya kwanza, Zidane alitangazwa kuwa kocha wa muda wa Real Madrid, Januari 4, 2016, baada ya timu hiyo kumfukuza Rafael Benitez, aliyekuwa akipata matokeo mabaya tangu mwanzoni mwa msimu wa 2015/16.

Zidane alikiongoza kikosi cha Real Madrid kwa mara ya kwanza Januari 9, katika mchezo wa La Liga dhidi ya Deportivo la Coruna na kushinda mabao 5-0 kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu.

Ulikuwa mchezo wa kwanza kwa Ronaldo kuwa chini ya Zidane, hata hivyo staa huyo wa Ureno hakubahatika kufunga bao zaidi ya kutoa asisti mbili kwa wenzake.

Lakini Ronaldo hakuchukua muda mrefu kuanza kuzifumania nyavu chini ya Zidane, Januari 17, 2016 alipachika mabao mawili katika ushindi wa 5-1 dhidi ya Sporting Gijon kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu.

Ukurasa wa staa huyo aliyetwaa tuzo za Ballon d’Or tano ulifungaliwa hapo na kumaliza na mabao 21 aliyofunga chini ya Zidane ndani ya La Liga, huku akiweka mengine sita katika Ligi ya Mabingwa Ulaya na kufanikiwa kutwaa taji hilo.

Ndani ya miezi mitano ya kwanza chini ya Zidane, Ronaldo alifanikiwa kufunga mabao 26 na kutoa asisti sita katika michezo 25 aliyocheza.

Lakini alifanikiwa kufunga jumla ya mabao 51 na kutoa asisti 15 katika michezo 48 aliyocheza msimu mzima.

2016/17

Msimu huu Ronaldo chini ya Zidane alipachika mabao 42 katika michezo 46 aliyocheza kwa msimu mzima na kuwa kinara wa kufunga mabao ndani ya Real Madrid, ambayo ilifanikiwa kutwaa taji la La Liga na kuandika historia mpya ya kutetea taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya kwanza.

Mchanganuo wa mabao hayo upo hivi, La Liga alifunga mabao 25 baada ya kucheza mechi 29, Ligi ya Mabingwa Ulaya alipachika mabao 12 ndani ya michezo 13.

Hakuishia hapo, ndani ya michezo miwili aliyocheza ya Klabu Bingwa Dunia alifanikiwa kufunga mabao manne, huku akifunga bao moja kwenye mechi mbili za Copa del Rey.

2017/18

Msimu ambao Real Madrid waliandika historia ya kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya mara tatu mfululizo, Ronaldo alifanikiwa kufunga mabao 44 katika michezo 44 aliyocheza.

Nahodha huyo wa timu ya Taifa ya Ureno alifunga mabao 26 katika mechi 27 alizocheza La Liga, Ligi ya Mabingwa Ulaya aliweka kambani mara 15 ndani ya michezo 12.

Ronaldo aliendelea kupachika mabao baada ya msimu huo kufunga mabao mawili katika michezo miwili ya Klabu Bingwa Dunia na lingine moja kwenye Ngao ya Jamii nchini Hispania.

JUMLA

Kwa kipindi cha miaka miwili na nusu ya Zidane ndani ya Real Madrid, Ronaldo alifanikiwa kufunga mabao 112, kutoa asisti 25 katika michezo 115.

Iko hivi, La Liga alifunga mabao 72, Ligi ya Mabingwa Ulaya aliweka wavuni mabao 32, Klabu Bingwa Dunia aliziona nyavu mara sita, Copa del Rey alifunga moja na Ngao ya Jamii alifanya hivyo mara moja.

Hakuna aliyefanikiwa kufunga mabao mengi chini ya Zidane zaidi ya Ronaldo, ambaye hivi sasa anaiwakilisha Juventus, kila mmoja anasubiri kuona jinsi kocha huyo na Mchezaji Bora wa Dunia wa zamani atakavyofanikiwa bila uwepo wa staa huyo wa Ureno.  

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here