SHARE

LIGI Kuu Bara imeanza kutimua Jumamosi wiki iliyopita, huku timu 16 zinazoshiriki michuano hiyo zikitupa karata zao za kwanza kwenye michuano hiyo.

Mabingwa watetezi wa Ligi hiyo, Yanga SC, wameanza vibaya michuano hiyo kwa kutoka sare ya bao 1-1 na Lipuli FC ya Iringa, huku watani wao wa jadi, Simba, wakianza kwa kutoa kichapo cha mabao 7-0 dhidi ya Ruvu Shooting ya Pwani.

Wakati wadau wa soka nchini wakianza kufurahia michuano hiyo kwa msimu huu mpya wa 2017/18 na kushuhudia mchezo mmoja tu kutoka kwa kila timu, tayari Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limepangua ratiba hiyo, ambapo wikiendi hii hakutakuwa na mechi za Ligi hiyo.

Hatua hiyo imekuja baada ya ratiba hiyo kuingiliana na ratiba ya kalenda ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), ambapo mwishoni mwa wiki hii kutakuwa na mechi za timu za Taifa, kwa ajili ya mechi za kirafiki.

Kutokana na hatua hiyo, wadau wa soka wameanza kulalamikia kusimamishwa kwa Ligi hiyo, kwani hali hiyo inapoteza ladha ya mashindano husika kusimamishwa kila wakati.

Wengine wameitaka TFF kupitia Bodi ya Ligi hiyo, kupanga ratiba ya mashindano hayo huku wakiwa wanafuatilia na kalenda ya FIFA, ili kuepusha kuingiliana kwa ratiba hiyo.

Ukiwa kama mdau wa soka nchini, unazungumziaje suala hilo?

Tuma maoni yako ukianzia na jina lako kamili na mahali uliko.

 

*********

MAJIBU YA WIKI ILIYOPITA

Wiki iliyopita kulikuwa na mada inayohusiana na kuwa nani atamaliza ‘Top four EPL’?

Ligi Kuu ya England ilianza kutimua vumbi katikati ya mwezi huu, ambapo mabingwa watetezi wa Ligi hiyo, Chelsea, walianza kwa kichapo kutoka kwa Burnley, wakiwa kwenye uwanja wa nyumbani.

Wakati Chelsea ikipokea kichapo hicho, Tottenham walianza kwa kuisambaratisha Newcastle kwa mabao 2-0 na Arsenal wakiibuka na ushindi wa mabao 4-3 kwa mabingwa wa zamani, Leicester City.

Liverpool walibanwa kwa sare ya mabao 3-3 dhidi ya Watford, huku Manchester City waliibuka kifua mbele kwa mabao 2-0 dhidi ya Brighton, ambao ni wapya kwenye Ligi hiyo.

Man U walianza kwa ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya West Ham na kufanya matokeo hayo ya vigogo wa Ligi hiyo kuibua hisia tofauti kwa mashabiki wa soka, huku wakijiuliza ni nani anaweza kuibuka ‘Top four’ kwenye michuano hiyo?

Wasomaji wengi walituma maoni yao juu ya suala hilo, ambapo kila mmoja anaonekana kuvutia upande wake, lakini wengi wakiamini kuwa, Man U, Liverpool, Man City na Chelsea wanaweza kumaliza wakiwa kwenye nafasi nne za juu.

 

*********

Naitwa Ayoub Haji wa Tabata, Ligi inaonyesha wazi kabisa, Mashetani wekundu wataongoza ligi na wengine watafuata.

 

********

Naitwa Cosmas Elibariki wa Arusha, Ligi bado mbichi, lakini kwa maoni yangu naona kama timu za Chelsea, Man U, Manchester City na Liverpool zitamaliza top four.

 

*******

Naitwa Martin Thomas wa Mwanza, michuano bado mapema sana, Ligi ndiyo kwanza imeanza, hivyo ni ngumu kubashiri timu zitakazomaliza nafasi nne za juu.

 

*******

Mimi ni Khamis Hassan wa Tanga, Chelsea kama kawaida itatetea taji lake, huku wengine wakifuata, Manchester City, Arsenal, Liverpool na Man U.

 

******

Naitwa Mohamed Yahaya wa Dar, mimi maoni yangu naona bado mapema kujadili suala hilo, tusubiri kuona Ligi inavyokwenda, kwani mpira hautabiriki.

 

******

Naitwa Zai wa Chelsea, wenye Ligi yao lazima waendeleze ubabe kwenye michuano hiyo, na wenye nafasi zao za pili, tatu na nne wanajijua wenyewe.

 

*******

Jina langu ni Jumanne Jamali wa Morogoro mjini, team Man U itaongoza Jahazi, Chelsea wanafuata, Arsenal na Liverpool ndio watakaomaliza nafasi nne za juu.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here