SHARE
MADRID, Hispania

WAKATI winga wa Real Madrid, Gareth Bale, anahusishwa kutakiwa na Manchester United miezi kadhaa iliyopita, hakuna aliyeshtushwa kwa kuwa ubora wake unajulikana wazi.

Hiyo haikuwa mara ya kwanza tangu Bale atue Madrid kwa uhamisho ulioweka rekodi ya dunia ya pauni milioni 85.3 miaka minne iliyopita, alitajwa sana kutakiwa tena England.

Lakini, Bale mwenyewe hajawahi kusema kama angependa kurejea England.

Jibu lake hadi leo ni kwamba ana furaha akiwa Hispania na wakala wake, Jonathan Barnett, mara kwa mara amekuwa akinukuliwa akisema tetesi za mteja wake kuondoka Bernabeu ni za ‘kipuuzi’.

Lakini, ukweli ulio wazi ni kwamba hatima ya Bale ndani ya viunga vya Madrid inaning’inia kwenye uzi mwembamba sana kutokana na kuumia kila mara.

Bale kutoikacha Bernabeu katika kipindi hiki hakuondoi uwezekano wa winga huyo kufungasha virago miezi michache ijayo.

Ni timu gani kwa sasa inamfaa Bale zaidi ya Man United? Bila shaka hakuna. Ukiachana na suala la kuumia kwake mara kwa mara, bado Bale ni chaguo sahihi la United, kutoa pauni milioni 85 si shida kwao.

Mashabiki wengi wa soka huwa hawapendi kusikia staa wao akipata majeraha kila kukicha na Bale anawaweka katika wakati mgumu mno mashabiki wa aina hiyo.

Hata hivyo, hata kama kuna machaguo mengine kwenye soko la usajili, bado hakuna winga mwenye ubora wa Bale.

Na ni vyema kwa mashetani wekundu hao wakapambana kuipata saini yake mwezi huu.

Hakuna chaguo sahuhi zaidi ya Bale

Kabla msimu huu haujaanza, kocha wa Man Utd, Jose Mourinho, alieleza nia yake ya kusajili wachezaji wapya wanne.

Alifanikiwa kuwapata Romelu Lukaku, Victor Lindelof  na Nemanja Matic, lakini alishindwa kusajili winga kama alivyopanga.

United ilihusishwa kumfukuzia winga wa Inter Milan, Ivan Perisic, lakini mazungumzo baina ya klabu hizo mbili yalivunjika kutokana na Inter kusisitiza kwamba wanahitaji angalau pauni milioni 49 na Anthony Martial kwa mkopo.

Perisic ambaye aliwahi kuitumikia Borussia Dortmund, ni mchezaji mzuri na bila ubishi ndiye aliyekuwa mchezaji bora wa Inter msimu uliopita. Uwezo wake unaweza kuwa kitu muhimu sana kwa mfumo wa United unaotaka winga zote ziwe ni halisi.

Lakini, kiwango chake hakijafikia kile cha Bale.

Bale ni bingwa mara tatu wa Ligi ya Mabingwa Ulaya; katika mechi yake ya 106 ya La Liga amefunga mabao 58, idadi ambayo kwa kawaida ni kiwango cha straika aliye kwenye timu inayosaka makombe.

Nani ambaye hafahamu kasi yake ya ajabu, mashuti makali na yaliyonyooka kwa kutumia mguu wake wa kushoto, balaa lake kwenye mipira iliyokufa sambamba na uchangamfu wake kwenye eneo la mwisho?

Kama wewe ni mpenzi wa muvi za Hollywood, Bale ni sawa kabisa na kile kisu maalumu cha kivita kinachotumiwa na makomandoo wazoefu. Kile kisu hukipati kokote zaidi ya Uswisi. Bale ni aina ya wachezaji wasiopatikana kirahisi duniani.

Pia ni mnyumbulifu kwenye mifumo mbalimbali, anacheza winga zote au kama namba 10, mzuri wa mashambulizi ya kushtukiza pia akiwa ni mbunifu wa kupangua ‘mabasi’ kwa zile timu zinazopenda kujilinda.

Mourinho anachelewaje kumchukua huyu mtu?

Kingine, kama hayo yote hayatoshi, Bale ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa wa kuibeba timu kwenye mgongo wake hata kama mchezo ni mgumu vipi.

Tujikumbushe kidogo, mwaka 2016 Bale alikuwa ni chachu ya kuivusha timu yake ya Taifa ya Wales hadi nusu fainali kwenye michuano ya Euro kule Ufaransa, akifunga mabao matatu na kwa kweli alikuwa ni supastaa wa timu.

Aliondoka England mwaka 2013 akiwa na tuzo ya mchezaji bora wa Premier League. Na kama atarejea, bado atakuwa ni mchezaji bora vilevile.

Kwa kuzingatia hoja za kimpira, United haihitaji kufikiria sana kumchukua mtu kama Bale. Ubora na uzoefu wake ni nguzo muhimu kwa timu yoyote ile inayotaka mafanikio.

Kinachomharibia ni majeraha tu. Msimu uliopita alicheza mechi 27 tu kutokana na kusumbuliwa na misuli. Msimu mmoja tena kabla alicheza mechi 31. Msimu huu ameonekana dimbani mara 11 tu.

Kuna mashaka kwamba, kwa umri wake wa miaka 28, upo uwezekano mdogo wa majeraha yake kutotokea tena mara kwa mara, hivyo kufanya miaka yake ya mwisho mwisho ya kucheza soka kurudi kwenye hali ya utulivu.

Msimu uliopita ilidaiwa kwamba, Bale aliwahishwa sana kucheza baada ya kupona kwa kuwa alitaka kuonesha thamani yake, lakini alikutana na Isco aliye kwenye ubora wake.

Haikuwa jambo sahihi, kwa mchezaji wa aina yake, utulivu ni kitu muhimu ili kumsaidia kurudisha kiwango chake.

Iwapo United watachangamkia suala la kumsajili na wakampa mechi 30 muhimu za kucheza, atawapa vingi vizuri.

Akichaguliwa mechi za maana na kupumzishwa pale inapobidi, mchango wake kwenye mechi za Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa utaibadilisha sana United na Mourinho.

Wataalamu wa soka wanasema Bale ana uwezo wa kufanya mambo mengi makubwa ndani ya mechi 30 kuliko wachezaji wengi wanaocheza mechi 60 kwa msimu.

Ni hatari kumsajili mchezaji mwenye rekodi ya kutisha ya kuumia, tena kwa gharama ya pauni milioni 85.

Lakini, United inapaswa kutambua, isiogope kujitoa mhanga na itumie fursa ya kuusogeza ubora wa Bale ndani ya viunga vya Trafford.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here