SHARE

NA ABDUL MKEYENGE

ILIWAHI kutokea kwa Pep Guardiola kutawala soka la Ulaya akiwa na Barca. Pep aliisumbua Ulaya kwa soka murua lenye muunganiko wa walinzi walaini na viungo mahiri. Kila timu iliiogopa. Dunia iliwahi kuliona hili.

Wakati vijana wa Pep wakiwa kwenye kilele cha ubora wao msimu wa 2011/02, walimtetemesha vidole Sir Alex Ferguson, kocha aliyefanikiwa kwenye soka la Uingereza.

Nini useme juu ya Ferguson kwenye ardhi ya Malkia? Ferguson ameshinda kila kitu ndani ya Uingereza na nje ya Uingereza. Tukio la mikono yake kunaswa ikitetemeka kwa soka murua la Pep na vijana wake, ni moja ya tusi kubwa kwa Waingereza kuona hili likitokea kwenye ardhi yao uwanja wa Wembley. Huo ulikuwa mchezo wa fainali ya Ligi Mabingwa baina ya Barca na Manchester United.

Kila zuri la Pep na vijana wake walilowahi kufanya huko nyuma imebaki sehemu ya historia ndani ya vitabu vyetu vya kumbukumbu tulivyovifunga hivi sasa.

Ghafla Barca ile iliyomtisha kila kocha imeenda kugeuka timu ya kawaida na isiyotisha. Ule utatu mtakatifu wa Messi, Iniesta na Xavi umeparaganyika.

Hivi sasa Pep yuko Manchester City, Andres Iniesta kabaki jina, Xavi Hernadez yuko Uarabuni. Ni Messi aliyebakia klabuni. Messi amezungukwa na wachezaji wazuri wenye viwango vya kawaida.

Wiki iliyopita Barca walifungwa mabao matano (5) kwenye michezo miwili na wapinzani wao Real Madrid. Barca hawajafungwa kwa bahati mbaya. Walistahili kufungwa.

Ni kama wakati ule ambao Barca ilivyokuwa ikistahili kuishinda kila timu inayokutana nayo. Nyakati zimebadilika. Hivi sasa kila kitu kiko tofauti.

Wakati Barca wakizidi kujiuliza nini kimewatokea na kukosa majibu, Zidane ameitengeneza Madrid bora bila kutumia gharama kubwa kama ilivyozoeleka.

Michezo miwili waliyofungwa Barca, walifungwa kwa uwezo. Barca walitawaliwa kila eneo. Wametawaliwa hadi kwenye eneo la kiungo ambalo ndiyo ilikuwa silaha yao muhimu muongo mmoja uliopita.

Kila nikirudisha kumbukumbu zangu sikumbuki lini Barca walizidiwa kwenye umiliki wa mpira eneo la kiungo, lakini chini ya Mardid ya Zidane nimeliona hili wiki iliyopita kwenye uwanja wa Santiago Bernabeu.

Zidane ameibadilisha Madrid. Ameibadilisha kuanzia mambo ya usajili hadi uchezaji ndani ya uwanja. Tangu Zidane aichukue timu misimu miwili iliyopita, timu haijafanya usajili wa kutisha. Madrid yenye jina la Galacticos si hii. Hii inatumia gharama ndogo sokoni, lakini ndani ya uwanja inapiga mpira mwingi.

Ilikuwa ngumu kwa dirisha la usajili kufunguliwa kama sasa bila kumuona Rais wa Madrid, Frolentino Perez, akipambana na matajiri wa timu nyingine kumtaka nyota wa timu ili amlete Madrid. Lakini wakati huu wa Zidane kila kitu kimebadilika.

Zidane ameweka uwiano mzuri kwenye vitabu vya Madrid. Anatumia gharama ndogo sokoni kuiletea mafanikio makubwa klabu. Unadhani tajiri gani wa timu asingemtaka mwanadamu wa aina hii kikosini kwake?

Kupitia Zidane na Madrid yake, kwa mara ya kwanza tumeona timu ikishinda taji la Ulaya mara mbili mfululizo. Kwenye hili hata nami nimekuwa sehemu ya historia kulishuhudia hili. Ilikera kuona timu ikishinda taji la Ulaya alafu msimu ujao inashindwa kulitetea. Hii  ilikera!

Lakini katika utawala wa Zidane, kutawala soka la Ulaya tumeliona hili na hata nikizitazama timu nyingine kuelekea msimu ujao wa ligi hiyo, bado naiona Madrid ikienda kushinda taji hili. Timu yao iko vizuri ina mchanganyiko wa wakongwe na vijana wenye vipaji vya hali ya juu.

Hiki kinachofanyika sasa ndani ya Madrid ni fikra za Zidane. Ni Zidane mwenye fikra za tofauti kuifanya Madrid ifanye hiki inachokifanya kwenye soka la Ulaya.

Siku moja ndani ya kurasa hii ya Ligi Ndogo, nilikuja na mawazo ya tofauti juu na Zidane. Nilimshangaa kwa baadhi ya mambo aliyokuwa akiyafanya, leo nikiri kupitia andiko lile nilimkosea Zidane na namuomba radhi rasmi.

Muungwana ni yule anayejua kafanya kosa na akaomba radhi. Namuomba radhi Zidane kwa mara nyingine. Muda huu niliochuchumaa chini kumuomba radhi Zidane ni wakati wa watu wengine kumuelewa na Madrid yake.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here