Home Habari NJOMBE WACHOMOA KUVAANA NA SIMBA

NJOMBE WACHOMOA KUVAANA NA SIMBA

6590
0
SHARE
NA MAREGES NYAMAKA   |

SIMBA ilikuwa icheze mechi yake ya kiporo ya Ligi Kuu Tanzania Bara na Njombe Mji, Aprili 3, mwaka huu kwenye Uwanja wa Sabasaba, mjini Njombe.

Lakini Njombe wakaitazama mechi na kuiangalia ratiba yao kisha wakaamua ‘kuchomoa’ na kudai hilo haliwezekani kwa sasa kwani ratiba imewabana mno.

Hatua hiyo inakuja baada ya kuwepo kwa taarifa kwamba watahitajika kucheza dhidi ya Simba katika tarehe hiyo, hivyo kuivuruga ratiba yao inayoonyesha kuwa wana michezo mitatu mfululizo katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Katibu wa timu hiyo, Obeid Mwakasungura, aliliambia DIMBA kuwa wanashangaa kuenea kwa taarifa hiyo kwani hakuna barua iliyowafikia kutoka Bodi ya Ligi wala kupigiwa simu, kitendo kinachowafanya kuendelea na majukumu yao ikiwamo maandalizi ya safari ya kwenda Shinyanga kesho Jumatatu.

“Ni uzushi hakuna kitu kama hicho, hata kanuni zenyewe ziko wazi kama inapotokea kuna mabadiliko ya ratiba wahusika ambao ni klabu wanapewa taarifa siku 14 kabla, Njombe Mji haijapokea taarifa kama hiyo,” alisema Mwakasungura.

“Hii itakuwa njia ya kutuondoa kwenye ligi, haiwezekani tukacheze Shinyanga siku mbili halafu turudi Njombe kisha turudi tena Shinyanga siku mbili baadaye. Kanuni inataka tupate taarifa siku 14 kabla, leo hata tukipewa kesho basi siku hizo hazikidhi kwa mujibu wa kanuni,” alisema.

Upande wa Simba kupitia kwa Mratibu wake Abas Ally, alisema hawana taarifa yoyote kuhusu hilo, bado wanasuburi mwongozo kutoka Bodi ya Ligi ili kupanga mikakati yao hasa safari yenyewe kama ni Mrogoro au Njombe.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi hiyo ya Ligi, Baniface Wambura, alisema atakuwa na mkutano na waandishi wa habari kesho Jumatatu katika ofisi za Shirikisho la Soka nchini (TFF), saa tano asubuhi kutangaza tarehe za michezo hiyo na ratiba nzima kwa ujumla.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here