Home Michezo Kimataifa NYOTA HAWA WALIPITA NJIA NGUMU LAKINI WAKAREJEA KWENYE UBORA

NYOTA HAWA WALIPITA NJIA NGUMU LAKINI WAKAREJEA KWENYE UBORA

563
0
SHARE

LONDON,England

BAADA ya kukaa nje ya dimba kwa muda mrefu na baadaye kurejea tena uwanjani hivi karibuni, nyota wa Manchester City, Yaya Toure, alidhihirisha kwamba yeye bado wamo, baada ya kuonyesha kiwango chake kile kile cha awali, hali iliyomlazimu kocha wa klabu hiyo, Pep Guardiola, kufungua kinywa chake  na kummwagia sifa.

Tukio hilo limekuwa kama somo jingine la uvumilivu kwa wachezaji wanaosaka mafanikio kote ulimwenguni.

Vita baridi kati ya Guardiola na Toure, haikuanzia kwenye jiji la Manchester, kwani ilianzia katika jiji la Barcelona, pale tu Guardiola alipotambulishwa mbele ya kamera za waandishi wa habari kuwa ndiye kocha mkuu wa klabu ya Barcelona.

Msimu wa kwanza wa Guardiola ndani ya Barcelona, 2007/008, aliondoa majina ya wachezaji waliokuwa mastaa, huku jina la Toure likiwekwa katika mstari mwekundu.

Msimu huo ukaisha kwa timu hiyo kupata mafanikio kwa kushinda mataji makubwa barani Ulaya. Licha ya Barcelona kuvuna mafanikio hayo, maisha hayakuwa mepesi kwa Toure.

Raia huyo wa Ivory Coast hakuwa sehemu ya kikosi cha kwanza na akipata nafasi hachezi katika eneo lake ambalo dunia imemfahamu. Dunia inamfahamu Toure akicheza eneo la kiungo wa kuzuia.

Guardiola hakumuamini Toure, bali alimuamini zaidi kijana aliyekuwa naye timu B ya Barcelona, Sergio Busquet. Msimu uliofuata Guardiola, aliamua kabisa kumuuza Toure kwenye klabu ya Manchester City.

Kuondoka kwa Toure kukafanya baadhi ya wachambuzi wa masuala ya soka duniani kusema Guardiola ni mbaguzi, huku wakilinganisha na shangilia ya aliyekuwa mshambuliaji wao, Samuel Eto’o, alipofunga bao katika mchezo wa fainali ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Manchester United, jijini Rome.

Lakini hivi sasa hali imekuwa tofauti kati ya wawili hao, kwani kwa siku za hivi karibuni kumekuwepo ushirikiano wa kutosha baada ya Toure kumuomba radhi bosi wake huyo kutokana na kauli tata zilizotelewa na wakala wake, Dimitri Seluk.

Kitendo chake cha kurejea tena dimbani na kuonyesha kiwango cha hali ya juu kimemwongezea kiungo hiyo thamani ndani ya  klabu  hiyo na kuwa miongoni mwa wachezaji tegemeo wasiokuwa wepesi wa kuathirika kwa jambo fulani.

Makala hii inakuletea nyota waliokumbana na misukosuko tofauti iliyowaweka nje ya dimba na baadaye waliporejea dimbani wakaendeleza makali yao kama kawaida.

David de Gea

Agosti 2015, Kocha wa Manchester United, Loius Van Gaal, baada ya kubaini nguvu ya Real Madrid ilikuwa kubwa kumvuta kipa wake huyo kuondoka mahali hapo, aliamua kwa makusudi kumweka benchi kipa huyo kama adhabu.

Unajua ilikuwaje? Van Gaal aliamua kumnunua kipa mwingine, Sergio Romero na kumsugulisha benchi Mhispania huyo, huku utimamu wake wa mwili ukionyesha kuwa hakuwa sawa.

Van Gaal alikuwa amemsajili Romero kama mbadala wa de Gea, lakini Makamu Mtendaji Mkuu wa Manchester United aliingilia kati suala hilo na kuwapigia simu upande wa pili wa Real Madrid kuwaeleza kuwa kwa wakati huo hawakuwa tayari kumuachia nyota wao huyo aende Hispania na badala yake wakamshawishi kuongeza mkataba wa kuendelea kuwapo viunga vya Old Trafford.

Presha ilipungua kwa Mhisipania huyo na kocha kuanza kumtumia tena katika kikosi cha kwanza, ambapo baadaye alionyesha ubora mkubwa na kila mara akiibuka nyota wa mchezo.

Carlos Tevez

“Sitarajii kabisa kurejea jiji la Manchester.”  Hayo yalikuwa maneno ya straika Muargentina, Carlos Tevez, akiiambia televisheni ya nchini kwao, kutokana na changamoto alizokumbana nazo jijini Manchester England, alipokabiliana na mazingira magumu mno wakati akikipiga katika klabu ya Manchester City mwaka 2011.

Katika kipindi hicho majira ya kiangazi, kocha wa Man City enzi hizo, Roberto Mancini, alimvuta straika mwingine, Sergio Aguero, aliyemtoa katika klabu ya Atletico Madrid, hatua iliyopelekea Tevez kusugua benchi katika kikosi cha kwanza, akinyang’anywa namba na Muargentina mwenzake huyo.

Hata hivyo, kutokana na mchango mkubwa alioutoa Aguero ndani ya klabu hiyo, ilisababisha kuzuka kwa mahusiano mabovu kiasi fulani kati ya Teves na Mancini na kumfanya straika huyo kuondoka katika viunga hivyo vya Etihad msimu wa 2013 na kutimkia katika klabu ya Juventus ya Italia.

Hata hivyo, baadaye aliamua kurejea na kumwomba radhi kocha wake huyo na kurejeshwa dimbani ambapo aling’ara vilivyo kama ilivyokuwa katika kipindi cha awali.

Emmanuel Adebayor

Baada ya kocha Andre Villas-Boas kuwasili Tottenham mwaka 2012 akitokea Chelsea, straika Mtogo Emmanuel Adebayor alikuwa mmoja wa wachezaji tegemeo kwenye mipango yake ambapo kila mara alikuwa akimmwagia sifa kutokana na uwezo wake mkubwa wa kuchana wavu.

Adebayor alifanikiwa kung’ara kwa kiasi kikubwa chini ya kocha huyo Mreno, takwimu zikionyesha katika michezo 50 aliyocheza katika kipindi kifupi aliingia kimiani mara 22, huo ulikuwa ni wastani mzuri kweli kweli kwa straika.

Lakini miaka miwili baadaye mambo yalibadilika ghafla, kutokana na uimara mkubwa wa Gareth Bale pamoja na usajili mpya wa Roberto Soldado, ambavyo vilimfanya Adebayor kujikuta akisugua benchi.

Yalikuwa maumivu mengine kwa Mtogo huyo, aliyekuwa anakipiga mahali hapo kwa mkopo akitokea Real Madrid, alikoanzia akipelekwa na klabu yake ya Manchester City.

Mvua ya mabao  6-0 waliyoipata Spurs mbele ya Manchester City na siku kadhaa wakikumbana na wimbi kama hilo kutoka kwa Liverpool ambayo iliwabamiza mabao 5-0, vikawa ni mwanzo wa kufunguliwa kwa mlango wa kutokea wa kocha Villas-Boas na mikoba yake ikichukuliwa na Tim Sherwood, aliyeamua kumrejesha tena Adebayor kikosini.

Adebayor hakumuangusha kocha huyo, kutokana na jinsi alivyoonyesha uhodari mkubwa tangu katika mechi ya kwanza tu, alipofanikiwa kuchana nyavu za Southampton mara mbili, huku wastani wake wa kufunga ukiwa maradufu, ambapo katika michezo 20 aliyopangwa kucheza, alifunga jumla ya mabao 11.

Ikumbukwe kuwa, moja ya vivutio vilivyoonyesha kwamba Adebayor alikuwa mwenye kufurahia kutimiza majukumu yake ni staili ya ushangiliaji aliyokuwa akiitumia ya kupiga saluti mbele, kama ishara kwamba lilikuwa chaguo sahihi kikosini, hiyo ilikuwa ni baada ya kuwatungua Sunderland mabao 5-1.

Xabi Alonso

Xabi Alonso unaweza kumuita shujaa. Baada ya kuondoka Liverpool miaka saba iliyopita akiwa na kikosi cha Real Madrid, mara nyingi alikuwa akikumbuka matukio kadhaa ya mahusiano mabovu kati yake na beki Mwingereza, Jamier Carragher, ikichagizwa na kukosa kwake kufunga penalti muhimu katika moja ya mechi kali 2005.

Katika msimu wake wa kwanza pekee, Alonso alifanikiwa kuwa mmoja wa wachezaji tegemeo kwenye kikosi cha kwanza cha Liverpool kilichotwaa taji la Ligi ya Mabingwa barani Ulaya pamoja na Kombe la FA.

Lakini kiungo huyo alisota nje ya dimba kwa muda kiasi akiuguza majeraha yake msimu wa 2007/08 na kumfanya kukosa michezo 11 kati ya 18 ya Ligi Kuu England.

Raia huyo akiwa chini ya kocha Rafa Benitez katika hiyo michezo aliyocheza, akitokea majeruhi hakuwa kwenye kiwango kizuri sana na hapo ndipo alielezwa na kocha wake aongeze juhudi zaidi.

Mwaka uliyofuata nyota huyo aliachiwa na ‘The Reds’ kutimkia Real Madrid, mahali ambako alifanikiwa kiasi kikubwa kutwaa mataji, kabla ya kuvutwa na Bayern Munich 2014 kama mchezaji huru.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here