SHARE

NA MAREGES NYAMAKA

ZIMEPITA siku mbili tu tangu mtanange ulioisimamisha dunia kati ya mahasimu wa jadi wa Ligi Kuu ya England (EPL), Liverpool na Manchester United, upigwe katika dimba la Anfield.

Katika mchezo huo mkubwa uliovuta hisia za wengi duniani ndani ya dakika 90, pia kulikuwa na nyota kadhaa kutoka bara la Afrika kama straika Sadio Mane, raia wa Senegal na beki Muivory Coast, Eric Bailly.

Makala hii inakuletea orodha ya wachezaji wanane waliozichezea klabu hizo mbili zenye mafanikio makubwa katika soka la England.

Eric Djemba-Djemba

Nyota raia wa Cameroon aliyewahi kuichezea Manchester United kuanzia mwaka 2003 hadi 2005, chini ya kocha mwenye mafanikio makubwa, Sir Alex Ferguson.
Hata hivyo, kiungo huyo hakudumu sana katika viunga hivyo vya Old Trafford, kwani baadaye aliamua kutimkia katika klabu ya Aston Villa, akiwa ameshuka dimbani mara 28 na kufunga bao moja pekee.

Mame Biram Diouf

Mame Biram Diouf alijiunga na Manchester United mwaka 2009, lakini ikawa nadra sana kumuona katika kikosi cha kwanza cha Mashetani hao Wekundu.
Kutokana na kushindwa kumshawishi Kocha Sir Alex Ferguson, aliamua kumfungulia milango mwaka 2012 akaenda kukipiga katika klabu ya Hannover 96 ya Ujerumani na baadaye mwaka 2014 aliamua kurejea katika Ligi Kuu ya England ndani ya klabu ya Stoke City.

Eric Bailly

Kabla ya mchezo wa juzi alipokabiliana na washambuliaji matata wa Liverpool, kina Sadio Mane, Roberto Firmino na Adam Lallana, Eric Bailly alikuwa tayari ni shupavu kikosini hapo. Muivory Coast huyo ni miongoni mwa nyota wachache wapya waliosajiliwa na kocha Jose Mourinho msimu huu.
Umahiri wake wa kuushika kwa haraka mfumo wa Mounrinho na kuhimili pia mikikimikiki ya ligi hiyo, vimemfanya aweze kuteuliwa kuwa mchezaji bora wa mwezi Septemba, huku akimwagiwa sifa na wachambuzi kadhaa wa soka nchini England ambapo baadhi humfananisha na beki wa zamani wa Mashetani hao Wekundu, Rio Ferdinand.

Sadio Mane

Ni winga Msenegali ambaye alihamia kwa Majogoo wa Anfield, Liverpool, akitokea katika viunga vya St Mary’s ndani ya klabu ya Southampton, lakini sasa tayari amekuwa mahiri katika safu ya ushambuliaji ya klabu hiyo ndani ya mfumo wa kocha Jurgen Klopp, anayependelea zaidi mtindo wa ‘Geggenpressing.’ Kabla ya mchezo huo wa juzi, tayari Mane alikuwa amekwishaingia nyavuni mwa timu pinzani mara tatu katika michezo sita aliyokuwa ameshuka dimbani.

Quinton Fortune

Ni kiungo raia wa Afrika Kusini aliyesajiliwa na Manchester United mwaka 2000 na kufanikiwa kukichezea kikosi hicho kwa miaka sita chini ya utawala wa Kocha Sir Alex Ferguson.
Katika muda huo wote aliokuwa katika viunga hivyo vya Old Trafford alifanikiwa kucheza jumla ya michezo 120 na kufunga mabao 10.
Ubora wake uwanjani ulimfanya kuwa na jina kubwa duniani, akiitangaza vema Afrika, huku pia akiipandisha thamani ya Ligi Kuu England katika bara la Afrika kwa ujumla.

Arthur Riley

Mwafrika mwingine, ingawa yeye alicheza upande wa pili kwa Liverpool ni Arthur Riley.
Mzaliwa huyo wa mji wa Boksburg aliitumikia Liverpool Agosti 1925, chini ya Kocha Matt McQueen na kufanikiwa kuwachezea Majogoo hao wa Anfield michezo 338 na baadaye kuondoka kwa heshima, huku akitajwa kama mlinda mlango bora.

Berry Nieuwenhuys

Huyu pia ni Mwafrika mwingine raia wa Afrika Kusini ambaye aliwahi kuichezea safu ya ushambuliaji katika klabu ya Liverpool kati ya mwaka 1933 hadi 1947 na kuwa kivutio kwa mashabiki wa Majogoo hao.

Mohamed Sissoko

Mohamed Sissoko anatajwa kama mmoja kati ya viungo wenye nguvu na uwezo mkubwa wa kumiliki mipira pindi anapokuwa dimbani.

Kabla ya kutua Liverpool mwaka 2005, alikuwa tayari na mafanikio ya hali ya juu, mojawapo ikiwa ni kufanikiwa kutwaa taji la Ligi Kuu ya Hispania msimu wa 2003-2004, huku pia akicheza fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka huo huo katika kikosi cha timu ya Valencia, kilichokuwa kikinolewa na kocha Rafael Benitez.
Kutokana na kusumbuliwa kwake na majeraha ya mara kawa

mara, alijikuta amekwishapokonywa namba na Javier Macherano na kumfanya 2008 kupata uhamisho wa kwenda Juventus na baadaye Paris Saint-Germain (PSG), mahali ambako aliweza kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ‘Escudetto’ na kuisaidia timu ya taifa ya Mali kushika nafasi ya tatu katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika 2013.

Rigobert Song

Rigobert Song, raia wa Cameroon anayesumbuliwa na ugonjwa wa kiharusi, aliichezea Liverpool kwa msimu mmoja pekee mwaka 1999/2000, akicheza michezo 34, huku akishindwa kupata mafanikio makubwa ndani ya Anfield. Klabu nyingine aliyoichezea England ni West Ham United kuanzia mwaka 2000 hadi 2002.

Bruce Grobbelaar

Huyu ni golikipa raia wa Zimbabwe aliyekaa langoni kwa muda wa miaka 13 na kuingia kwenye vitabu vya kumbukumbu ya wachezaji raia wa Afrika waliocheza kwa mafanikio. Akiwa mchezaji tegemeo kwa Majogoo hao wa Anfield, aliiwezesha klabu yake hiyo kushinda mataji ya Ligi Kuu sita, Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 1984.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here