Home Makala OMARY MPONDA: TSHABALALA NI BEKI BORA TANZANIA

OMARY MPONDA: TSHABALALA NI BEKI BORA TANZANIA

948
0
SHARE

NA MARTIN MAZUGWA,

UNAPOTAJA majina ya washambuliaji waliofanya vizuri kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara kwa wakati huu, ni lazima jina la mshambuliaji wa kati wa timu ya Ndanda ya Mtwara, Omary Mponda, litakuwa miongoni mwao, baada ya kufikisha mabao saba akiwa nyuma ya Shiza Kichuya, mwenye mabao tisa.

Uwezo wake umechangia kwa sehemu kubwa klabu zenye uwezo wa kifedha, ikiwamo Simba, Yanga na Azam kuanza kumfikiria kwenye mipango yao ya siku za usoni.

Nyota huyu, ambaye alikuwa mmoja kati ya vijana waliochaguliwa katika kikosi cha Taifa Stars Maboresho, kabla ya kuvunjika na kujiunga na Ndanda, ilipokuwa daraja la kwanza ambayo amedumu nayo mpaka hivi sasa.

Dimba lilimtafuta nyota huyu na kufanya naye mazungumzo mafupi juu ya mambo mbalimbali ambayo yamekuwa yakimsaidia kufanikiwa katika mipango na kazi zake za kila sikuk, jambo linalomfanya kuwa tofauti, licha ya kuwepo kwa ushindani mkubwa kwenye ligi ya msimu huu.

DIMBA: Kuna taarifa kuwa upo kwenye mazungumzo na Yanga, kuna ukweli wowote katika hili?

Mponda: Mimi sijafanya mazungumzo ya aina yoyote na Yanga, ila nimekuwa nasikia fununu tu, ila hakuna taarifa rasmi ambayo imekuja kwangu au kwa watu wanaonisaidia kwamba nahitajika kwenye klabu hiyo kongwe Tanzania.

DIMBA: Umekuwa katika kiwango bora, nini siri ya kufanya kwako vizuri msimu huu?

Mponda: Msimu uliopita haukuwa mzuri kwangu kutokana na ugeni, lakini pia sikuwa na uzoefu na ligi kubwa, jambo ambalo msimu huu halipo tena, kwani uzoefu niliopata msimu uliopita umenijenga kwa sehemu kubwa.

DIMBA: Ni beki gani alikupa wakati mgumu mzunguko wa kwanza?

Mponda: Beki aliyenipa wakati mgumu zaidi mzunguko wa kwanza ni mlinzi wa kati wa klabu ya Simba raia wa Uganda, Jjuuko Murushid, ndiye alikuwa beki bora zaidi kwangu katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

DIMBA: Mpaka sasa ni timu gani umefanya nayo mazungumzo?

Mponda: Sijafanya mazungumzo na timu yoyote mpaka.

DIMBA: Mpaka sasa umepachika mabao saba kwenye mzunguko wa kwanza, unahisi unaweza kutwaa kiatu cha mfungaji bora?

Mponda: Hakuna kitu kinachoshindikana chini ya jua, naamini nina uwezo huo, ninachoomba ni uzima tu.

DIMBA: Unafikiri Ndanda wanafaa kushika nafasi ya kumi katika msimamo?

Mponda: Si nafasi sahihi kwetu, naamini makosa yaliyojitokeza mzunguko wa kwanza yaliyosababisha tupoteze michezo mingi mwalimu ameyaona, naamini atayafanyia kazi na tutarudi kivingine katika mzunguko wa pili.

DIMBA: Iwapo utapata nafasi ya kucheza Yanga, unadhani mchezaji gani anafaa kuwa pacha wako?

Mponda: Katika mpira hutakiwi kuchagua, kwani mwalimu ndiye mwenye maamuzi ya mwisho.

DIMBA: Kitu gani hutokisahau kilichotokea mzunguko wa kwanza?

Mponda: Siku tumetoka sare na JKT Ruvu ni mchezo ulioniuma, kwani nilishindwa kumaliza dakika 90 mara baada ya kupata majeraha.

DIMBA: Ulijisikiaje mara ya kwanza ulipoitwa katika kikosi cha timu ya Taifa?

Mponda: Kwanza sikuamini, nilisikiliza redio zaidi ya tatu ili kuhakikisha kama kweli ni mimi, lakini kama unavyojua kuwepo kwenye timu ya taifa tu ni heshima kubwa, kwa sababu wachezaji wapo wengi, hivyo mwalimu kuamua kukuona na kukuita si jambo dogo wala la kubeza, ila ni heshima kubwa wamekupa.

DIMBA: Ni mchezaji gani anayekuvutia hapa Tanzania?

Mponda: Navutiwa na uchezaji wa mlinzi wa kushoto wa klabu ya Simba, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, ni mchezaji mwenye nidhamu nzuri nje na ndani ya uwanja.

DIMBA: Umewahi kutumia kilevi chochote kabla ya kuingia uwanjani?

Mponda: Sijawahi kutumia kilevi chochote kutokana na misingi niliyolelewa na familia yangu, ambapo wamenilea katika misingi ya dini, ambayo ninaifuata hadi sasa.

DIMBA: Muda wako wa mapumziko unautumiaje?

Mponda: Mara nyingi muda wa mapumziko huwa nautumia kwa kurudi nyumbani kukaa pamoja na wazazi wangu, ambao bado nahitaji ushauri kutoka kwao.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here