Home Michezo kitaifa OMEGA AMFUATA FARID MUSSA HISPANIA

OMEGA AMFUATA FARID MUSSA HISPANIA

1632
0
SHARE

NA CLARA ALPHONCE

KIUNGO wa timu ya Lipuli FC ya Iringa, Omega Seme, anatarajia kuondoka nchini wakati wowote kuanzia sasa kuelekea Hispania, kwa ajili ya majaribio ya wiki mbili katika klabu ya CD Tenerife inayoshiriki Ligi Daraja la Pili nchini humo (LaLiga2).

Mwenyekiti wa Lipuli FC, Ramadhan Mahano, alisema klabu ya Tenerife imemuhitaji mchezaji huyo na imewaandikia barua kumuomba Omega Seme ili kwenda kufanya majaribio na kama akishafuzu ndio wanaweza kuanza mazungumzo ya uhamisho wake.

“Ni kweli tumepokea maombi ya Omega kwenda Tenerife kwa muda wa wiki mbili kwa ajili ya majaribio, sisi kama klabu tumekubaliana na ombi hilo na tumeshamruhusu mchezaji ili aweze kwenda kujiandaa na safari yake.

“Tuna imani kwamba kufanikiwa kwake ni mafanikio pia kwa soka la Lipuli, Iringa na Tanzania kwa ujumla wake. Uongozi unamtakia kile la kheri katika safari yake hiyo aweze kufuzu na kufanikiwa katika majaribio yake,” alisema Mahano.

Lipuli ilimsajili Omega kwa ajili ya mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara na Kombe la FA, baada ya kuitumikia Ndanda msimu wa mwaka jana, ambapo aliingia moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza cha Kocha Amri Said.

Tenerife ndiyo timu anayoitumikia kiungo wa zamani wa Azam FC na timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars), Farid Mussa ambaye bado hajaweza kupata nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha Kocha Josep Lluis Marti raia wa Hispania.

Dirisha la usajili wa dirisha dogo nchini Hispania limefunguliwa tangu Januari mosi mwaka huu, ambapo linatarajiwa kufungwa Januari 31, mwaka huu, ingawa taarifa ambazo DIMBA limezipata ni kwamba, mpango wa Tenarife ni kumsajili nyota huyo wa zamani wa Yanga na Ndanda katika usajili wa dirisha kubwa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here