SHARE

NA MAREGES NYAMAKA,

LICHA ya kocha wa Simba, Joseph Omog, kutibuliwa rekodi na African Lyon mwishoni mwa wiki iliyopita kwa kukubali kichapo cha kwanza kabisa tangu kuanza kwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu huu, lakini bado Mcameroon huyo amembwaga kocha wa Yanga, Hans van der Pluijm.

Africa Lyon walitibua rekodi ya Simba baada ya kuwafunga bao 1-0 mchezo wa Ligi Kuu Tanznaia Bara uliochezwa Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam na kuharibu mipango ya Omog aliyetaka kumaliza mzunguko wa kwanza bila kufungwa.

Hata hivyo, kocha huyo wa Wekundu hao wa Msimbazi ameendelea kuwafunika makocha wenzake wa kigeni wanaovinoa vikosi vya ligi hiyo akiwamo kocha wa mabingwa watetezi Yanga na hadi sasa ameiongoza Simba ikiwa ni timu pekee iliyofungwa mabao machache.

Simba imeruhusu kufungwa mabao manne, tofauti na mpinzani wake wa karibu Pluijm ambaye walinda milango wake wameruhusu mabao saba, huku Omog akimtumia kipa mmoja tu, Vincent Angban na Yanga ikiwatumia makipa wote watatu; Ally Mustapha ‘Barthez,’ Deogratius Munishi ‘Dida’ pamoja na Beno Kakolanya.

Pia, Omog amefanikiwa kuwa na kinara wa mabao kwenye timu yake ambaye ni winga Shiza Kichuya, mwenye mabao tisa, mawili nyuma ya straika wa Pluijm, Amissi Tambwe, ikisubiriwa kama kutakuwa na mabadiliko michezo ya leo na kesho mzunguko wa kwanza utakapokamilika.

Vile vile, Mcameroon huyo amekuwa shujaa wa kukusanya pointi tisa michezo ya ugenini akiwafunga Stand United bao 1-0, akawafunga Mwadui FC mabao 2-0 na ushindi kama huo dhidi ya Mbeya City wakati Simba wakiokota pointi hizo mikoani.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here