Home Habari OMOG ATAJA WIKI TATU ZA JASHO NA DAMU

OMOG ATAJA WIKI TATU ZA JASHO NA DAMU

378
0
SHARE

NA EZEKIEL TENDWA,

KOCHA Mkuu wa Simba, Joseph Omog, amezitaja siku tatu walizokuwa Kanda ya Ziwa kwamba zilikuwa ngumu sana kwake na kwamba hatakuja kuzisahau.

Katika wiki hizo tatu, Simba walicheza michezo mitatu dhidi ya Kagera Sugar, ya Mkoani Kagera, Mbao FC pamoja na Toto Africans zote za jijini Mwanza.

Katika michezo hiyo, Simba walianza kwa kufungwa mabao 2-1 na Kagera Sugar, wakashinda mabao 3-2 dhidi ya Mbao FC na kutoka suluhu ya 0-0 dhidi ya Toto Africans, hiyo ikimaanisha kuwa katika Kanda hiyo ya Ziwa, walijikusanyia pointi nne, wakidondosha nne.

Hata hivyo, huenda wakarejeshewa pointi dhidi ya Kagera Sugar, kwani walikata rufaa wakidai kuwa Wakata Miwa hao walimchezesha Mohamed Fakhi akiwa na kadi tatu za njano kinyume cha sheria za soka, na maamuzi yanaweza yakatolewa leo na Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji.

Akizungumza na DIMBA, Omog alisema wiki hizo tatu zilikuwa ngumu sana kwake, ikizingatiwa kuwa alikutana na timu ambazo baadhi yao zinapambana kuepuka mkasi wa kushuka daraja.

“Zilikuwa wiki ngumu sana ambazo tulikuwa nje ya Dar es Salaam, kwani timu ambazo tulicheza nazo baadhi zinapambana kutokushuka daraja, sasa kwa hali hiyo lazima michezo iwe migumu,” alisema.

Katika hatua nyingine, kikosi hicho kinatarajiwa kuanza kujifua leo kujiwinda na michezo mitatu ya Ligi Kuu iliyobakia, huku pia wakisubiri nani ambaye watapangwa naye hatua ya nusu fainali michuano ya FA, ambapo leo ndio droo inachezeshwa.

Michezo mitatu ya Ligi ambayo Simba wamebakisha ni dhidi ya African Lyon, Stand United pamoja na Mwadui, yote ikichezwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here