Home Makala Omog: Kiu ya Simba ni ubingwa tu

Omog: Kiu ya Simba ni ubingwa tu

774
0
SHARE

NA SAADA SALIM

NI jambo zuri kwa Simba kuingia mkataba wa miaka miwili na Kocha Joseph Omog, raia wa Cameroon ili aifundishe timu hiyo katika michuano mbalimbali msimu utakaoanza siku zijazo.

Simba imeona mbali, kwani Omog anasifika kwa kulifahamu soka la Afrika, pia Ligi ya Tanzania anaijua, kwani aliifundisha Azam FC msimu wa 2013/14 kwa mafanikio makubwa.

Chini ya Omog, Azam ilitwaa ubingwa wa kihistoria, kwani ilikuwa mara yake ya kwanza, pia haikupoteza hata mchezo mmoja, hii inatosha kuamini Simba imepata kocha sahihi. Tatizo linaweza kuwa lilelile la siku zote, yaani kocha kutopewa uhuru na viongozi kuingilia majukumu yake.

Kinyume cha hapo, Simba itabaki palepale, kwani kwa kocha anayejielewa kama Omog hatakubali kuingiliwa kazi na anaweza kuiacha timu. Raia huyo wa Cameroon ameingia  mkataba wa miaka miwili kukinoa kikosi cha Wekundu wa Msimbazi kwa msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Ikumbukwe kwamba Mcameroon huyo aliingia kwenye rada za Simba baada ya kumuweka katika orodha ya makocha inaowataka, imeamua kuachana kabisa na suala la Wazungu na Omog, aliyewahi kuinoa Azam FC na kuipa mafanikio kwa mara ya kwanza.

Hata hivyo, inaonekana chaguo la kwanza la Simba ni Kocha Kalisto Pasuwa, anayeinoa timu ya Taifa ya Zimbabwe. Simba walifanikiwa kufunga safari hadi Zimbabwe kwa lengo la kufanya mazungumzo, hatimaye mpango huo ukakwama.

Baada ya kumkosa Pasuwa, Simba walimfuatilia kocha mwingine kutoka nchini Ghana, Sellas Tetteh, huyo ilikuwa kama ilivyo kwa Pasuwa. Ndipo viongozi hao wakaangukia katika chaguo lao la tatu kwa Omog, baada ya kuridhishwa na rekodi zake alizowahi kufundisha soka kwa mafanikio.

Omog  amekabidhiwa mfupa uliowashinda wazungu, kama ilivyokuwa Azam FC ilipita kwa makocha wengi tangu 2007 hadi 2013/14,  alipokabidhiwa mikoba Mcameroon huyo kwa kutwaa ubingwa.

Kocha huyo aliingia na kukinoa kikosi cha Azam FC akiwa na falsafa zake, hali hiyo inategemewa na mashabiki pamoja na Wanasimba kuona Omog, yule aliyeipa mafanikio ya kutwaa ubingwa Azam iwe zaidi kwa sasa akiwa na kikosi cha Simba.

Jambo la msingi analofanya sasa:

Omog anasema kwa sasa anachokifanya ni kuhakikisha anawafahamu wachezaji wake wote, pia kuwaweka wachezaji wake wawe sawa sawa.

“Kikubwa ni kuhakikisha nawafahamu wachezaji wangu, pili niwajenge kila mmoja awe sawasawa, kisha nitaanza programu yangu kwa ajili ya msimu ujao,” anasema Omog.

Usajili wachezaji wa ndani:

Kocha huyo anasema anahitaji kuona timu hiyo inafanya usajili wa wachezaji watakaoleta matokeo ndani ya kikosi, hivyo kabla ya kutua nchini alipendekeza kuona ripoti iliyoachwa na mtangulizi wake ili kuweza kuifanyia kazi.

“Nilizungumza na Simba kwa kupitia barua pepe kuhusu suala la kuja kuinoa timu yao, nilikubali, baadaye walinieleza suala la kuanza usajili kwa wachezaji wa ndani na kutumia ripoti ambayo ameiacha kocha aliyemaliza msimu na timu,” anasema.

Kocha huyo anasema ameona repoti hiyo na kuelezwa juu ya wachezaji waliosajiliwa, kutoka katika timu nyingine ambapo  baadhi yao alifanikiwa kuwaona akiwa anafundisha Azam FC.

 

Malengo yake Simba:

Anasema lengo lake kubwa ni kurejesha heshima ya klabu hiyo, kwani kuipatia ushindi kwa kila mechi kwa kuhakikisha inafanikiwa kutwaa ubingwa.

“Ubingwa ni kiu kubwa iliyokuwepo kwa Simba, kwani imepoteza heshima yake, nina imani kubwa kwa ushirikiano mzuri wa viongozi, wachezaji, wanachama, mashabiki pamoja na benchi langu la ufundi hili litafanikiwa,” anasema Kocha huyo.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here