SHARE

NA AYOUB HINJO

HAYATI Douglas MacArthur, Jenerali katika jeshi la Marekani, aliyepigana vita zote mbili za dunia, aliwahi kusema, ‘Ni ngumu kusema uongo pindi unapoumia’. Ikikuuma utasema tu. Na utasema ukweli mtupu.

Unai Emery anaumia mno na Mesut Ozil. mashabiki wa Arsenal wanaumizwa sana na Ozil. Kila aliye karibu na Klabu ya Arsenal, anaumizwa na maamuzi ya Mjerumani huyo mwenye asili ya Uturuki.

Bahati nzuri wachezaji wenzake walishindwa kuvumilia na maumivu na kusema kwa lugha ya vitendo, lakini wengine wote wamechagua kuugulia kimya kimya japo naamini watasema siku si nyingi kutoka sasa.

Ozil anaivuruga sana Arsenal. Katika nyakati ambazo klabu inapita kwenye mapito magumu, amejitoa kwenye mstari wa mapambano. Ameamua kuusimamia moyo wake.

Ukiungalia msimamo wa Premier League, hivi sasa utawaona Arsenal walipo mbali na ubingwa. Mbali kweli kweli. Pumzi ya karibu kwao ni kumaliza katika timu nne za juu ‘Top 4’.

Kubeba taji la Premier au kumaliza kwenye nafasi nne za juu unahitaji kuwa na wachezaji bora kabisa katika kikosi chako. Emery analijua hili na ndio maana awali aliweka msimamo wa kukomaa na Ozil hadi mwisho wa msimu.

Itazame Arsenal ambayo haina Ozil inapokuwa uwanjani, kuna mambo mengi ya msingi yanakosekana katika eneo la mwisho. Kuanzia kwenye kiungo mpaka kwa washambuliaji.

Kesi ya mabeki kuvuja mithili ya pakacha ni tatizo lingine, hilo tutalizungumzia wakati ujao japo si geni kwa Arsenal. Lilikuwepo tangu zama za Arsene Wenger, safu ya ulinzi inapitika kwa urahisi kama maji yanayopita kwenye mkondo wake.

Wameruhusu kufungwa mabao 14 katika michezo 10 ya Ligi Kuu England ambayo wamecheza huku wakifunga mabao 15 mpaka sasa. Faida kwao ni bao moja tu.

Binafsi naitazama Arsenal kivingine, naiangalia kama timu ambayo imekusanya wachezaji wengi wenye uwezo mkubwa katika safu ya kiungo na ushambuliaji, lakini kuna kikubwa wanakikosa.

Ubora uliopo kwa akina Pierre-Emerick Aubameyang na Alexandre Lacazette hauna maana kama watakosa huduma ya kiwango cha lami kutoka kwa viungo wao. Ubunifu umekuwa tatizo kubwa kwenye sehemu ya kiungo cha Arsenal.

Tangu Emery achukue nafasi ya Wenger msimu uliopita, Ozil alitoa asisti mbili tu msimu mzima huku akicheza michezo 24 ya Ligi Kuu England. Mbili? Inashangaza kidogo.

Emery si mjinga kumwacha Ozil nje licha ya kiungo chake kuwa na takwimu ndogo za kutengeneza nafasi tangu kuanza kwa msimu huu.

Kuna upande namwelewa Emery lakini kuna upande mwingine nipo tofauti naye. Pamoja na Ozil kuwa na udhaifu mkubwa wa kukaba au kufanya kazi za ulinzi pindi mpira unapokuwa kwa wapinzani bado hakuna mchezaji mwenye uwezo wa kumfikia kiwango chake anapokuwa kwenye ubora wake katika eneo la kiungo.

Ozil anahitaji kuwa huru. Anahitaji kupunguziwa jukumu la kukaba na kuachwa kuwa ‘creative hub’ ya timu.

Emery anahitaji kubadilika ili ambadilishe Ozil, la sivyo ataendelea kugombana na kila mtu. Ni jambo la kuamua tu. Lakini kwa upande mwingine, Unai anaendelea kuishi kwenye mawazo yake licha ya kujua ni vipi Mesut anatakiwa kutumika.

Granit Xhaka, Matteo Guendouzi na Lucas Torreira ni wachezaji ambao wana uelekeo mmoja lakini wana matumizi tofauti, hata ile kasi aliyoingia nayo Dani Ceballos haionekani tena.

Ni wazi Emery alitaka kuwanyamazisha wanaombeza kuhusu Ozil kwa kumtumia Ceballos katika eneo hilo, lakini Mhispania huyo haeleweki, leo atacheza vizuri, kessho atakuwa tatizo uwanjani.

Naamini uliiutazama mchezo waliocheza dhidi ya Liverpool na kumalizika kwa vijana hao wa Jurgen Klopp kushinda kwa mikwaju ya penalti 5-4, baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya mabao 5-5.

Ozil alicheza kwa kiwango chake, alitengeneza nafasi mbili na kutoa asisti moja lakini bado alikuwa tatizo kwa Arsenal sababu mpaka anatolewa alishindwa kupokonya mipira tisa ikiwamo bao lililofungwa na Ox Chamberlain.

Sidhani kama Ozil anajali kuhusu Arsenal, kwake acheze au asicheze sawa tu. Hakuna kingine kinachofurahisha moyo wake zaidi ya pauni 350,000 kwa wiki inayoingia kwenye akaunti yake ya benki.

Katika umri wa miaka 31 atake nini tena? Kwenye ubora wake alishinda Kombe la Dunia, La Liga, Copa del Rey na makombe matatu ya FA.

Moyo wa Ozil sidhani kama unatamaa ya mafanikio makubwa zaidi, ukizingatia anaishi katika pepo yake ndani ya Arsenal, sababu ni mmoja wa wachezaji wanaopendwa zaidi na mashabiki wa kikosi hicho.

Sidhani kama akiondoka Arsenal ataenda au kusajili timu ya daraja la juu zaidi, pengine atakuwa mmoja wa wachezaji wataoenda China au Marekani kuendelea kutunisha msuli wa akaunti yake na kuendelea kuufurahisha moyo wake.

Upande wa pili wa Emery unahukumiwa na kile alichokiamini mwanzo. Baada ya kuingia Arsenal, alimwona Ozil kuwa mkombozi wake, mchezaji pekee ambaye angemfanya aishi katika ndoto zake za kuijenga timu mpya na imara.

Labda alivyomfikiria na alivyomwona ni vitu viwili tofauti. Japo kiasili Ozil anajulikana ni mtu wa aina gani, ni mvivu mwenye ubongo unaofikiri kwa kasi zaidi ya mbio za Usain Bolt.

Kuna mambo mawili ambayo yanaweza kutokea na kurudisha ubora wa Arsenal katika eneo la kiungo ambalo walikuwa na utajiri mkubwa wa viungo mafundi.

Moja, Emery kumrudisha kikosi Ozil na kumtengenezea mazingira kama ilivyokuwa wakati Ule Jose Mourinho anaifundisha Real Madrid.

Timu yote ilimzunguka Ozil, walicheza kwa ajili yake, walikaba na kumpa mipira, hakuonekana kuwa tatizo sababu udhaifu wake ulifichwa na jasho la Lassana Diara na Xabi Alonso.

Hebu fikiria, kumwona Xhaka na Guendouzi au Torreira wkikimbia kilomita nyingi uwanjani kwa ajili ya Ozil ambaye atakuwa na kazi moja tu ya kuunganisha mawasiliano kwa kusafirisha mipira kwenda kwa Lacazette na Aubameyang.

Kuna kitu kikubwa kitakuwa kimetiwa ndani ya timu. Kwanza, safu ya ulinzi itakuwa katika wakati mzuri sababu watalindwa na wachezaji wawili kwa wakati mmoja na kupunduza presha kwao.

Lingine, watakuwa na uhakika wa kufunga mabao mengi, sababu Ozil hajawahi kushindwa kutengeneza nafasi, kutoa asisti au kufunga mabao pale inapombidi.

Mbili, kucheza kama Liverpool ambao hawana viungo wenye ubunifu mkubwa katikati uwanja, wanachofanya ni kupora mipira na kuipeleka juu kwa wachezaji wenye kasi.

Huoni kama watafanikiwa? Sadio Mane, Roberto Firmino na Mohamed Salah, ubora wao unatokana na kazi kubwa inayofanywa na akina Jordan Henderson, James Milner, Fabinho na Gini Wijnaldum.

Arsenal wapo akina Aubameyang ambaye ana uwezo wa kutokea pembeni kulia kama Mane, Lacazette kupewa majukumu ya Firmino na Nicolas Pepe kuwa Salah. Kuna kitu kikubwa watakipata Washika bunduki, lakini kwa sasa, tumwache Ozil aishi na moyo wake na Emery aendelee kuwa mwenye kiburi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here