Home Michezo Kimataifa PEREZ ADHAMIRIA KUWANASA KANE, HAZARD NA DE GEA

PEREZ ADHAMIRIA KUWANASA KANE, HAZARD NA DE GEA

2360
0
SHARE
MADRID, Hispania


KLABU ya Real Madrid imepanga kuvamia kwenye Premier League na kumwaga zaidi ya pauni milioni 300 katika dirisha la usajili wa majira yajayo ya kiangazi, ili kuzinasa saini za Eden Hazard, Harry Kane na David de Gea.

Rais wa klabu hiyo, Florentino Perez, sasa ameamua lazima kikosi chake kirudi kwenye mstari kwa mpango huo kabambe wa kuhakikisha wanasajili ‘galacticos’ na kwa kuanza tu, wamepanga kuwapa Chelsea ofa ya pauni milioni 200 ili wamchukue nyota wa Chelsea, Hazard.

Aidha, Madrid imepanga kutumia pauni milioni 100 kumnasa mlinda mlango mahiri wa Man United, David de Gea na pauni milioni 200 kwa straika hatari wa Tottenham, Harry Kane.

Yote haya yanakuja kutokana na presha waliyonayo katika harakati za kupunguza pengo la pointi 19 baina yao na vinara wa LaLiga, Barcelona.

Rada ya Madrid inaelezwa kuelekea zaidi kwa washambuliaji Hazard na Kane.

Hadi kufikia sasa, bado tetesi za mshambuliaji wa PSG, Neymar kuhamia Bernabeu zinaendelea kurindima, japokuwa wamiliki wake wamesema hawatamuuza, lakini hilo linaendelea kufuatiliwa kama ni kweli watashikilia  msimamo wao.

‘Plan B’ ya Madrid iwapo watamkosa Neymar, ni kuhakikisha Hazard anatua Bernabeu pamoja na Kane, ambaye Perez anamuona kama mchezaji anayemfaa sana kwenye mipango yake ya kuirudisha Madrid kwenye mstari.

Hata hivyo, wasiwasi mkubwa ni kama atakubali kuondoka Spurs hivi sasa, na ikizingatiwa uwanja mpya wa klabu hiyo unakaribia kumalizika.

Aidha, Spurs walisema wazi kwamba, Kane hatauzwa kwa gharama yoyote ile, ingawa iwapo Madrid watafanikiwa kumbeba na kocha Mauricio Pochettino kama tetesi zinavyosema, straika huyo ana kila dalili ya kumfuata kocha huyo Bernabeu.

Kwa Hazard, hofu kuu ni suala la mkataba mpya Chelsea, ambao baba yake mzazi alidai mwanawe alikataa kuusaini. Hazard alikanusha madai hayo.

Madrid pia itaingia sokoni kusaka kipa mwingine, baada ya windo lao la hivi karibuni, Kepa Arrizabalaga wa Bilbao kusaini mkataba mpya ndani ya timu hiyo.

Sasa miamba hao wamehamia tena kwa De Gea na iwapo Man United watazikataa pauni milioni 100 ili wamwachie, watahamisha nguvu zao zote kwa kipa wa Chelsea, Thibaut Courtois.

Hii ni nguvu kubwa ambayo Perez anataka kuitumia, baada ya miaka minne ya kushindwa sokoni dhidi ya timu kama Man United, Man City na PSG.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here