SHARE

NA SALMA MPELI


BAADA ya kutoka sare ya kufungana bao 1-1 dhidi ya Mwadui FC mwishoni mwa wiki iliyopita, Kocha Mkuu wa Azam FC, Hans van der Pluijm, ameweka wazi kuwa wataingia katika mechi zao mbili zilizosalia Kanda ya Ziwa kuhakikisha wanavuna pointi sita.

Awali, mipango yake ilikuwa ni kuhakikisha wanakwenda kusaka pointi tisa katika mechi zao tatu kwenye mikoa hiyo, lakini baada ya kutoka sare dhidi ya Mwadui sasa nguvu zote wanaelekeza katika mechi hizo mbili dhidi ya Biashara ya Mara na Alliance ya Mwanza.

Azam wanatarajiwa kuwa wageni wa Biashara leo katika Uwanja wa Kumbumbuku ya Karume, Musoma ikiwa ni mchezo wao wa pili kwenye Kanda hiyo.

Akizungumzia kikosi chake, Pluijm alisema wachezaji wote wako katika hali nzuri na tayari kiungo mshambuliaji Tafadzwa Kutinyu, ameshajiunga na timu akitokea kwenye majukumu ya timu ya Taifa ya Zimbabwe ‘The Warriors’.

“Tunaingia katika mchezo huo malengo yetu ni kuondoka na pointi tatu kabla ya mchezo wetu mwingine wa Mwanza ili kuhakikisha wanavuna alama tatu nyingine japo soka linamatokeo matatu, kushinda, kutoka sare na kufungwa,” alisema Pluijm.

Katika msimamo wa Ligi Kuu Bara, Azam wapo kwenye nafasi ya pili kwa kujikusanyia pointi saba ikizidiwa pointi moja na JKT Tanzania iliyofikisha nane lakini ikicheza mechi moja zaidi ya matajiri hao kutoka viunga vya Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here