Home Habari Pluijm:Yanga kwanza tusahau yaliyopita

Pluijm:Yanga kwanza tusahau yaliyopita

420
0
SHARE

NA EZEKIEL TENDWA

BAADA ya kutengua uamuzi wake wa kujiuzulu kuifundisha Yanga, Kocha Mkuu wa Wanajangwani hao, Hans van der Pluijm, amewaambia mashabiki kusahau yaliyopita na sasa waungane kuitetea timu yao.

Pluijm alifikia uamuzi wa kuandika barua ya kujiuzulu baada ya kusikia taarifa za timu yake hiyo kumleta kocha mpya raia wa Zambia, George Lwandamina.

Lwandamina, ambaye anaifundisha Zesco ya Zambia, alitua nchini mwishoni mwa wiki iliyopita ambapo licha ya jambo hilo kufanywa siri, DIMBA linajua kuwa alikutana na baadhi ya viongozi wa Yanga na kufanya nao mazungumzo kabla ya kurejea Zambia.

Baada ya taarifa hizo kumkuta Pluijm, aliamua kuandika barua ya kujizulu ambapo alishindwa kukaa kwenye benchi Yanga walipocheza na JKT Ruvu na Juma Mwambusi alikaimu nafasi hiyo kwa muda wakiibuka na ushindi wa mabao 4-0.

Aliyeingilia kati suala hilo na kumfanya Pluijm kuamua kurejea kwenye kibarua chake ni Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba, ambaye ni mwanachama mwaminifu ya Yanga.

Akizungumza baada ya mazungumzo hayo na Waziri huyo, Pluijm alisema yaliyopita yamepita na sasa mashabiki wa Yanga wanatakiwa kuyasahau na kufungua ukurasa mpya.

“Nimefanya majadiliano chanya na Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani (Mwigulu Nchemba), yeye ndiye ambaye amechangia kwa kiasi kikubwa mimi kubadili maamuzi.

“Niwaambie tu Wanayanga wote kwamba hayo yamepita na sasa tuangalie namna ya kutetea ubingwa wetu, kwani safari bado ni ndefu, naamini kwa kushirikiana tunaweza kufanya jambo kubwa,” alisema.

Mholanzi huyo alimaliza mazungumzo yake na Waziri Nchemba juzi Ijumaa na jana Jumamosi akaanza kazi rasmi, ambapo leo anatarajiwa kukiongoza kikosi chake dhidi ya Mbao FC.

Wanajangwani hao watakuwa wenyeji wa kikosi hicho cha Mbao ambacho huu ni msimu wake wa kwanza kushiriki Ligi Kuu, mchezo utakaochezwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

SHARE
Previous articleYanga: Tuna hasira
Next articleOkwi hali ngumu Denmark

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here