Home Makala PWEZA AKIMENDI RODRIGUEZ ANAVYOWAPA HOMA MASHABIKI WA MAN UNITED

PWEZA AKIMENDI RODRIGUEZ ANAVYOWAPA HOMA MASHABIKI WA MAN UNITED

499
0
SHARE

NA NIHZRATH NTANI

UTABIRI ni ufundi wa kihisia kwa kile kinachotabiriwa. Jinsi au namna ya kusema jambo lenye kubashiri kitakachotokea siku zijazo.

Sayansi ya utabiri wa kihisia ilikuwa imeshamiri mno katika jamii yetu enzi hizo. Kizazi hadi kizazi kimejikuta kikirithi sanaa hii na kuendeleza kwa manufaa ya jamii hata baada ya kushamiri kwa maendeleo ya teknolojia bado sanaa hii ingalipo.

Kwa miaka ya karibuni sanaa ya utabiri imeshamiri katika ulimwengu wa soka. Baadhi ya mashabiki wamekuwa wakijiingiza katika sanaa ya utabiri kupitia kwenye makampuni mbalimbali maarufu kwa jina la ‘Kubeti.’

Hata hivyo, wapo watu, wanyama hata jamii nyingine za viumbe hai nao pia wanatumika katika kujaribu kubashiri mambo mbalimbali katika jamii. Wadudu kama ‘kakakuona, pweza, tembo na jamii ya binadamu nao hawako mbali katika sanaa hii.

Katika michuano ya Euro 2008 iliyofanyika katika nchi za Austria na Uswisi, aliibuka kiumbe jamii ya pweza nchini Ujerumani aitwaye ‘Pweza Paulo’, ambaye alitumika kufanya utabiri wa mechi za timu ya taifa la nchi hiyo na alitabiri mechi sita huku mechi nne zikitoa matokeo sahihi na mbili utabiri wake haukutimia.

Mpaka kufikia 2010 katika fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika Afrika Kusini, pweza huyu ‘Paulo’ alikuwa maarufu sana midomoni mwa wapenzi wa soka ulimwenguni kote, baada ya kufanya utabiri wa mechi 13, huku mechi 11 utabiri wake ukikamilika kwa kutoa matokeo chanya, ikiwa ni sawa na asilimia 85 kufanikiwa.

Baada ya kuisha kwa michuano ya Kombe la Dunia mwaka huo. Miezi michache tu baadaye ‘Pweza Paulo’ alikutwa amekufa katika sehemu aliyohifadhiwa Oktoba 26, 2010. Mwisho wa Pweza Paulo. Huzuni iliyoje hii!

Desemba mwaka jana, katika nchi ya Mexico, aliibuka mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la utani la ‘Akimendi Rodriguez’. Mtu huyu alitoa tabiri zake 15 zilizokuja kushangaza wengi. Baadhi ya tabiri zake zilionekana kama moja ya maajabu ya dunia kutokea kwa nyakati hizo. Lakini zilikuja kutimia na moja ya tabiri zake zilikuwa hizi:-

 

RAFA BENITEZ KUFUKUZWA REAL MADRID NA ZIDANE KUCHUKUA NAFASI YAKE NA KUIPA TIMU HIYO UBINGWA

Ulikuwa utabiri wa kuchekesha. Kwamba kocha Rafa Benitez angetimuliwa Real Madrid na Zidane angechukua nafasi yake na kuipa timu hiyo ubingwa. Zilihitajika akili za uwendawazimu hasa kuweza kuliamini jambo hili. Ndio ni mwendawazimu pekee angeamini kuwa Real Madrid wangeweza kutwaa ubingwa wa Ulaya 2016.

Chini ya Benitez, Real Madrid walionekana wakiwa na kiwango duni cha soka, huku klabu za Barcelona, Bayern Munich, Atletico Madrid hata Juventus zikionekana kuwa hatari zaidi uwanjani.

Januari 4, 2016 kabla ya msimu kuisha. Rafa Benitez alikuja kufukuzwa Real Madrid na siku moja baadaye Zinedine Zidane alitangazwa kuchukua nafasi yake. Kama ilivyotabiriwa Real Madrid ilikuja kutwaa ubingwa wa Ulaya huku Zidane akiwa kocha mkuu wa klabu hiyo. Utabiri ukatimia.

 

CRISTIANO RONALDO ANGEVAA MEDALI YA DHAHABU KWA URENO KUTWAA UBINGWA WA MICHUANO YA ‘EURO’ 2016

Ni utabiri ulioonekana kama dhihaka kwa wakati huo katika ulimwengu wa soka. Hakuna shabiki aliyewahi kufikiri kuwa Ureno ingekuja kutwaa ubingwa wa michuano ya Euro 2016. Kizazi chao bora kilichostahili kutwaa taji hili kilishapita miaka mingi iliyopita. Kizazi cha akina Rui Costa, Jorge Costa, Pauleta, Nuno Gomez, Figo, Deco, Victor Baia na wengine wengi.

Kwa mshangao wa wengi, hakuna aliyeamini Ureno ilikuja kutwaa ubingwa wa michuano ya Euro katika moja ya matokeo ya kushangaza zaidi katika soka. Nina hakika kwamba hata Cristiano Ronaldo ama Wareno wenyewe hawakuwahi kufikiri kuwa wangeweza kutwaa taji la Euro mwaka huu. Ni mwanamume mmoja tu Akimendi Rodriguez aliyeamini hili.

 

LEICESTER CITY WANGEFUZU KUCHEZA MICHUANO YA ULAYA NA ARSENAL WANGEPOTEZA MECHI ZOTE MBILI DHIDI YA BARCELONA

Wakati Akimendi Rodriguez akitoa tabiri hizi, Manchester City ilikuwa kileleni mwa Ligi Kuu ya England huku Leicester City wakikamata nafasi ya pili kwa tofauti ya uwiano wa magoli ya kufunga na kufungwa.

Mpaka kufikia Mei, 2016 Leicester City ilikuwa si tu imefuzu michuano ya Ulaya bali pia imetwaa taji hilo kwa mara ya kwanza katika historia. Ni maajabu ya soka.

Vile vile Barcelona na Arsenal walikuja kukutana katika hatua ya pili ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Historia inamwelezea kocha wa Arsenal kuwa ni mgumu sana kupoteza mechi zote mbili ya nyumbani na ugenini katika hatua ya mtoano kwa michuano ya Ulaya.

Hata hivyo, alikuja kupoteza mechi zote mbili alizocheza dhidi ya Barcelona na kuufanya utabiri wa Akimendi Rodriguez kutimia.

 

LIONEL MESSI ANGETWAA TUZO YA BALLON D’OR NA PELE ANGEWEZA KUFA MWAKA HUU

Kwa Lionel Messi tunaweza sema ulikuwa utabiri rahisi mno. Lionel Messi alikuja kutwaa tuzo yake ya Ballon D’or siku chache baadaye akimshinda mpinzani wake mkuu, Cristiano Ronaldo na Xavi.

Kumtabiria mfalme wa soka duniani, Edson Nascrimento maarufu kama Pele wa Brazil kuwa anaweza kufa 2016, ilishangaza. Mpaka makala haya inatoka bado Pele yupo hai akiwa na afya njema kwao Brazil, lakini bahati mbaya bado mwaka haujaisha. Ni tabiri yenye kuogopesha.

 

JOSE MOURIHNO KUWA KOCHA WA MANCHESTER UNITED NA ATAFELI MSIMU WAKE WA KWANZA

Mpaka kufikia Desemba mwanzoni, 2016. Jose Maurinho, alikuwa bado kocha wa Chelsea. Pamoja ya kuwa alikuwa katika wakati mgumu lakini hakuna mtu aliyekuwa na fikra za kuwa angefukuzwa na miezi michache angeteuliwa kuwa kocha wa Manchester United.

Wakati huo huo, Louis Van Gaal, alikuwa katika benchi la Manchester United. Hakuna yeyote aliyefikiri kuwa Louis Van Gaal angefukuzwa mwishoni mwa msimu kutokana na hulka ya klabu hiyo kuvumilia sana makocha hasa akiwa na jina kubwa kama alivyo Van Gaal.

Mpaka kufikia Juni, 2016, tayari Louis Van Gaal alishafukuzwa Manchester United huku miezi michache iliyopita, Jose Mourihno, naye alishatimuliwa Chelsea. Bila shaka utabiri ulikuja kutimia baada ya Mourinho kutangazwa kuwa kocha mkuu wa Manchester United. ‘Shikamoo’ Akimendi Rodriguez!

Hata hivyo, hadi sasa Manchester United bado haijawapa matumaini mashabiki wake. Wanakamata nafasi ya sita katika ligi wakiwa na pointi 18 katika michezo 11, pointi 8 dhidi ya Liverpool wanaoongoza ligi hiyo.

Mashabiki wa Manchester United kila wakitazama mwenendo wa timu yao na utabiri wa Akimendi Rodriguez wanajikuta wakiwa wanapoteza matumaini ya kupata mafanikio msimu huu chini ya Mourinho.

Pamoja na tabiri zake nyingi kutimia, Akimendi Rodriguez, katika tabiri zake nyingine hazikuweza kutimia. Kama vile alivyosema Arsenal wangetwaa ubingwa wa England 2016, Neymar angeondoka Barcelona kwa ada ya rekodi ya dunia.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here