Home Habari Rais Mtaka alipa milioni 4.8 za madeni ya wanariadha

Rais Mtaka alipa milioni 4.8 za madeni ya wanariadha

1432
0
SHARE

ELIYA MBONEA-ARUSHA

RAIS wa Shirikisho la Riadha Nchini (RT), Anthony Mtaka amefanikiwa kutimiza ahadi ya kuwalipa wanariadha wote waliokuwa wanadai shirikisho hilo.

Wanariadha waliolipwa ni pamoja na wasichana sita waliofanya vizuri kwenye mbio za dunia za nyika mwaka 2017 nchini Uganda.

Kiasi cha shilingi milioni 4.8 kimegawiwa mgawo wa shilingi laki nane (800,000) kila mmoja, fedha ambazo zimetolewa na shirikisho la riadha la dunia (ITF).

Wanariadha hao ni pamoja na Failuna Abdi Matanga, Anjelina Daniel Tsere, Magdalena Shauri, Sara Ramadhani, Mayselina Mbua, Siaka Kalinga ambao waliibuka washindi wa sita kwa upande wa timu na kuifanya Tanzania kuzawadiwa kiadi cha dola 6000.

Wengine waliolipwa fedha zao ni wanariadha watatu wa Mbio za Dodoma Marathon mwaka 2016, ambao walikuwa wazawadiwe mabati lakini yalipotea chini ya mikono ya uongozi wa RT.

Wanariadha Gabriel Geay (kwa upande wa wanaume) na Fadhila Salum (Kwa upande wa wanawake) waliokuwa washindi wa pili katika mbio zile alitakiwa kulipwa bati 100 kila mmoja ambapo walifidiwa kiasi cha shilingi milioni moja kila mmoja (1,000,000) huku Catherine Lange aliyeshika namba tatu aliyekuwa anadai mabati 40 amepatiwa shilingi 400,000.

“Katika kuelekea mashindano mapya ya kimataifa, yaliyoko kwenye kalenda ya Shirikisho tumeona tulipe kwanza madeni yote ya wanariadha waliokuwa wanadai maana naona yanaleta maneno maneno mengi na yanaweza kuwa sio mazuri kwa afya ya mchezo wa riadha,” amesema Mtaka


Akitoa sababu za wanariadha hao kucheleweshewa fedha hizo, Mtaka amesema kuwa fedha hizo ziliingizwa na shirikisho la riadha Duniani (ITF) kwenye akaunti isiyo sahihi ya RT, hivyo walilazimika kutoa taarifa wazirudishe kwao na watume tena kwenye akaunti sahihi ya shirikisho hali iliyochukua mda mrefu.


Akipokea fedha hizo mmoja wanariadha hao, Anjelina Tsere amemshukuru Mtaka kwa kutimiza ahadi hiyo ambayo wameshaikatia tamaa ya kuipata tena lakini sasa imani hiyo imerudi kwa shirikisho hilo.


“Kwanza nitumie nafasi hii kukushukuru Rais kwa kutimiza ahadi hii maana ilitugharimu sana nguvu zetu hivyo kimya cha muda mrefu cha viongozi wetu ilitufuta kabisa matumaini ya kupata fedha hizi lakini leo tumepata ni jambo jema na imetutia moyo katika mapambano ya kuelekea mashindano ya nyika ya dunia tunaahidi tutafanya vyema zaidi”


Kwa upande wake kocha mwandamizi wa riadha nchini Zacharia Barie amesema kuwa hatua ya shirikisho hilo kulipa madeni hayo yatarahisisha kazi za makocha watakaopata nafasi ya kunoa kikosi cha timu za taifa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here