Home Michezo kitaifa RASHID MATUMLA VISA NA MIKASA MIAKA 34 ULINGONI…(3)

RASHID MATUMLA VISA NA MIKASA MIAKA 34 ULINGONI…(3)

889
0
SHARE

KARIBU msomaji wa safu hii ya ITS SHOW TIME, bado tunaendelea na simulizi hii ya gwiji wa masumbwi hapa nchini, Rashid Matumla, ambaye kutokana na uwezo wake mkubwa, amekuwa mfano wa kuigwa na mabondia chipukizi.

Kutokana na ubora wake kukua kwa kasi sana, huku akizidi kupanda uzito na kuwa hatari zaidi, ilifika kipindi mkali huyo akajitengenezea jina kubwa hapa nchini.

Wiki iliyopita tuliishia bondia huyo alipotoka katika mashindano ya majeshi nchini Uganda aliposhindwa kubeba medali ya dhahabu mara baada ya kufanyiwa hujuma na majaji, kitu kilichopelekea kuibua fujo mara baada ya matokeo hayo.

Mara baada ya kumalizika kwa mashindano hayo, mkali huyo alipewa likizo fupi kabla ya kuingia kambini kwa ajili ya maandalizi ya mashindano ya kuwania medali ya ubingwa wa Taifa.

Ilikuwa likizo fupi sana kutokana na muda mwingi kuwa kambini kwa ajili ya mashindano mbalimbali, kipindi hicho tulikuwa tukipata nafasi ya kucheza mashindano mengi, ndiyo maana mabondia wa kipindi hicho tulikuwa bora.

Baada ya kumaliza likizo yangu niliingia kambini Ngome moja kwa moja ili niweze kufanya vizuri kutokana na mashindano haya kuwa na mabondia wengi tunaojuana.

Nilikuwa nafanya mazoezi mara tatu kwa siku, jambo lililokuwa likifanya uwezo wangu uwe wa hali ya juu zaidi, huku mwalimu wangu akinitaka kuacha masihara.

Unajua kipindi naingia jeshini kwa mara ya kwanza nilikuwa mdogo, lakini mwenye uwezo mkubwa, hivyo nikawa kipenzi cha Mwalimu Lokens Swai, ambaye alikuwa akinilea kama mtoto wake.

Yalikuwa ni maandalizi ya nguvu sana ambayo kwa bondia wa hivi sasa akifanyishwa mazoezi ya aina ile anaweza kuacha ngumi, kwa kuwa mimi nilikuwa nahitaji heshima nililazimika kutumia nguvu sana ili kumfurahisha mwalimu wangu.

Kipindi hicho nilikuwa namuahidi mwalimu wangu kuwa safari hii lazima nichukue medali ya dhahabu na kufuta machungu niliyopata nchini Uganda katika mashindano ya majeshi.

Ilikuwa inafika kipindi kutokana na ugumu wa mazoezi mabondia mnaleteana maneno ya karaha, wakati mwingine hata kurushiana ngumi.

Kama unavyojua, mabondia wa Ngome mara nyingi wamekuwa wakifanya vizuri kutokana na ubora wa kambi yenyewe, ambapo bondia unapewa kila kitu na hata ukipoteza unapewa lawama ambazo huwezi kuzikimbia.

Nakumbuka mashindano ya mwaka 1986 yalikuwa na msisimko sana, kutokana na kujaa damu changa niliingia katika mashindano nikiwa mnyonge, mara baada ya kuona jina la Pius Msele, miongoni mwa mabondia bora zaidi kwa wakati huo.

Mwalimu aligundua mapema akawa ananitoa wasiwasi kuwa mimi ni bondia mzuri, sipaswi kuwa mwoga na siku zote napaswa kujiamini kuwa mimi ni bora.

Nakumbuka pambano langu la kwanza niliibuka mshindi kwa kumaliza pambano raundi ya pili na kuibua kelele kwa mashabiki ambao walitarajia ningemaliza raundi 12.

Hadi nafika fainali nilikuwa nimeshinda mapambano yote kwa KO na kusababisha mashabiki kuanza kunichukia kutokana na kumaliza mapambano yangu mapema.

Wakati naendelea kushinda mapambano yangu na kwa upande wa Msele kwa wakati ule kila mmoja alijua angefika fainali,  kutokana na ubora wake.

Pambano la fainali lilikuwa likisubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki ambao walikuwa wakitaka kukata mzizi wa fitina kati ya mimi na Msele nani alikuwa bora.

Katika pambano hilo lililokuwa la uzito wa Light Fly, nililimaliza raundi ya nne tu na kuibuka na ubingwa wa Taifa kwa mara ya kwanza na kubeba medali ya dhahabu.

Mara baada ya mashindano haya kumalizika na kutimiza malengo yake aliyojiwekea kwa kubeba medali ya dhahabu, unafikiri nini kilifuata kwa mkali huyo mwenye medali na mikanda lukuki ya uzito tofauti?

Usikose toleo lijalo la DIMBA ili kujua nini kiliendelea mara baada ya mashindano haya kumalizika.

MAONI: 0714925661

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here