Home Makala Raul ndiye mchezaji bora wa muda wote La Liga

Raul ndiye mchezaji bora wa muda wote La Liga

666
0
SHARE
  • Awabwaga vibaya akina Messi, Cristiano Ronaldo

NIHZRATH NTANI NA MITANDAO

PENGINE unajiuliza kuwa ni mchezaji gani katika vizazi vyote kwenye soka la Hispania anayestahili kuwa mwanasoka bora wa muda wote?

Hakuna shaka kuwa Lionel Messi na Cristiano Ronaldo ni baadhi ya wachezaji mahiri na bora kabisa ambao kizazi hiki tumepata bahati ya kuwashuhudia.

Kwa wapenzi wa La Liga na soka kwa ujumla hivi leo tungeambiwa tupige kura ya wachezaji bora wa muda wote wa La Liga, bila shaka majina ya Messi na Ronaldo yasingekosekana katika tatu bora.

Hata hivyo, kwa mujibu wa kituo cha utafiti wa historia na takwimu za soka nchini Hispania majibu yanayokuja ni tofauti.

Hakuna jina la Messi wala Ronaldo katika tatu bora ya wachezaji bora wa muda wote wa La Liga tangu kuanzishwa kwake 1928/1929 hadi matokeo haya yanatolewa mwezi huu. Inashangaza!

 

MCHAKATO ULIKUWA HIVI

Kituo hicho kilifanya utafiti huo kwa kupanga idadi ya alama huku mchezaji aliyecheza dakika nyingi uwanjani akipewa alama ya pointi 24 kwa misimu yote aliyocheza.

Kituo kikatoa alama ya pointi 1 kwa kila goli unalolifunga. Huku mchezaji akipewa alama ya pointi 0.60 kwa kufunga goli la penalti, huku mchezaji akipewa alama ya 0.40 kwa mchezaji aliyesababisha kufungwa kwa goli kwa sababu ya makosa ya timu mfano kujifunga.

Alama ya 1.50 aliipewa mchezaji kwa kusababisha kadi nyekundu kwa mpinzani wako. Kwa vigezo hivi ndipo ambapo gwiji la Real Madrid, Raul Gonzalenz alipoibuka mshindi. Wachezaji 10 bora wa muda wote wa La Liga kwa mujibu wa kituo hicho ni kama ifuatavyo:-

 

10.GUILLERMO GOLOSTIZA (Bilbao na Valencia)

Kizazi cha sasa ni jina geni kwetu. Lakini Golostiza ameacha alama kubwa katika La Liga. Amecheza jumla ya mechi 256 na kutupia goli 178 huku akitwaa mataji 11. Sita kati ya hayo ni mataji ya La Liga, katika misimu 14 aliyocheza katika ligi hiyo.

Mzaliwa huyo wa Santurtz, Biscay katika jimbo la Basque ametwaa tuzo ya ufungaji bora ‘Pichichi’ mara mbili. Pamoja na umahiri wake enzi ya uhai wake, lakini Golostiza alikufa akiwa maskini mno akiwa mlevi kupitiliza katika umri wa miaka 57.

 

  1. CARLOS ALONSO ‘SANTILLANA’ (Racing Santander na Real Madrid)

Carlos Alonso anatajwa kuwa mmoja wa washambuliaji bora kabisa katika historia ya soka la Hispania. Mtu huyu aliyepewa jina la utani la ‘Santillana’ kwa sababu anatokea mji wa Santillana ulio katika Manispaa ya Cantabria ndani ya Hispania.

Amecheza mechi 496 na kufunga magoli 202. Enzi zake alikuwa mshambuliaji hatari mno. Katika misimu 17 ya La Liga alitwaa mataji 9 ya La Liga na manne ya Copa, huku akiwa na mataji mawili ya UEFA kupitia Real Madrid. Hata hivyo, hakuwahi kushinda tuzo ya Pichichi katika La Liga pamoja na uwezo wake huo.

 

  1. FRANCISCO ‘PACO’ GENTO (Racing Santander na Real Madrid)

Gento anatajwa kuwa ndiye mchezaji aliyetwaa mataji mengi zaidi ya ubingwa wa Ulaya akiwa na timu moja pekee. Alifanya hivyo akiwa kwenye kikosi cha timu ya Real Madrid kati ya mwaka 1953-1971, ambako alitwaa mataji sita ya Ulaya.

Gareth Bale hivi leo anatajwa kuwa mchezaji mwenye kasi zaidi duniani, akicheza kama winga wa kushoto. Hata hivyo Bale asingetamba enzi ya Gento. Mtu huyu ndiye mchezaji anayetajwa kuwa alikuwa na kasi zaidi duniani. Angeweza kukimbia kilomita 100 kwa sekunde 11 tu.

Ametwaa mataji 12 ya La Liga. Mzaliwa huyu wa mji wa Guarnizo nchini Hispania, alicheza jumla ya mechi 438 kwa misimu 14 na kufunga goli 130. Anatajwa kuwa winga bora wa kushoto wa muda wote. Nguvu, ubunifu, kasi, muono, mbinu, uwezo wa kufunga na kusaidia magoli. Hii ni sifa ya Gento.

 

  1. ALFREDO DI STEFANO (Real Madrid na Espanyol)

Hakuna maneno mengi unayoweza kumueleza gwiji huyu. Edson Nascrimento ‘Pele’ anamtaja Di Stefano kuwa ndiye mchezaji bora wa mwenye kipaji zaidi ambaye amepata kumuona Argentina. Mtu huyu ndiye mchezaji pekee ambaye amewahi kuchezea mataifa matatu tofauti kwenye michuano ya kimataifa. Amefanya hivyo akiwa Argentina, Colombia na Hispania.

Ni Di Stefano anayetajwa kuwa ndio chanzo cha kuimarika kwa upinzani wa Barcelona na Real Madrid. ‘Saeta Rubia’ alijulikana hivyo kwa utani. Akiwa pembeni ya Gento na Jose Maria Zarraga, kwa pamoja waliiwezesha Real Madrid kutamba barani Ulaya. Historia ya kutwaa mataji ya Ulaya kwa Real Madrid ipo kwenye miguu ya mtu huyu. Kwa misimu yake zaidi ya 12 alifunga magoli 227 katika mechi 329.

 

6.JUAN ARZA (Sevilla na Atletico Almeria)

Ndiye anayetajwa kuwa gwiji la soka katika klabu ya Sevilla. Kuna majina mengi yamepita katika dimba la Juan Sanchez Pijuan, lakini jina la Juan Arza bado lingali linaishi mpaka leo.

Alicheza misimu 16 katika La Liga na kufunga magoli 184 katika mechi 368. Alikufa akiwa na miaka 88 mnamo 17/7/2011. Juan Arza ametwaa taji moja tu la La Liga huku akiwa na tuzo moja ya Pichichi. Wakati mwingine umahiri wa mchezaji hauwezi kupimwa na mataji aliyokuwa nayo.

 

5.ENRIQUE CASTRO QUINI (Sporting Gijon na Barcelona)

Mzaliwa huyu wa Oviedo nchini Hispania. Kizazi cha sasa ni ngumu kumfahamu. Lakini unapotazama idadi ya waliotwaa tuzo ya pichichi katika La Liga. Haraka jina hili litakuwa kileleni kabisa. Ametwaa tuzo ya ufungaji bora mara 7 huku mara 5 akiwa amefanya hivyo katika La Liga na mara mbili akifanya katika Segunda division.

Quin amecheza misimu 12 katika La liga. Akitupia magoli 275 katika mechi 443.Akiwa na miaka 67 sasa mchezaji huyu hajawahi kutwaa taji la La Liga. Lakini uwezo wake unazungumza.

 

  1. LIONEL MESSI (Barcelona)

Ni mshangao, jina lake kuwa nafasi hii. Pengine angepaswa kuwa ndani ya nafasi mbili za juu. Rekodi zake zinazungumza zaidi kuliko kuzitaja. Tunahitaji ukurasa mzima kumzungumzia Lionel Messi na pengine hautatosha.

Jambo rahisi kulizungumzia ndiye mfungaji bora wa muda wote katika La Liga, huku akiwa mfungaji bora pia Barcelona. Kirahisi naweza kusema ana tuzo tano za Ballon D’or. Bahati nzuri kizazi hiki kimemshuhudia zaidi mtu huyu. Hakuna kama yeye.

Messi amefunga magoli 316 katika mechi 353. Ametwaa La Liga 9 na Uefa 4. Ana tuzo tatu za pichichi. Katika misimu 12 sasa akiwa Barcelona.

 

3.TELMO ZARRA (Athletic Bilbao)

Mzaliwa wa Erandio katika Jimbo la Basque. Telmo Zarra ni mfalme katika Uwanja wa San mames, mahala ilipo klabu ya Athletic Bilbao. Huyu ndiye mwanadamu anayechukuliwa kuwa mchana nyavu hatari zaidi aliyepata kuzaliwa katika ardhi ya nchi ya Hispania.

Ametumia misimu 15 katika La Liga, akifunga magoli 251 katika mechi 277. Ametwaa tuzo ya Pichichi mara 6. Mbele ya mtu huyu si Messi wala Ronaldo aliyefanya hivyo. Bado anashikilia rekodi ya kufunga magoli mengi katika Copa Del Rey. Ilimchukua zaidi ya mechi 20 kwa Lionel Messi kuvunja rekodi ya Telmo Zarra katika La Liga. Unaweza kuwaza tu Telmo Zarra alikuwa wa aina gani?

Alifariki 24 Februari, 2006. Kutokana na umahiri wake chama cha soka cha Hispania kikaanzisha tuzo ya ZARRA, ambayo hutolewa kwa Mhispania aliyefunga goli nyingi kwa msimu wa La Liga.

 

  1. CESAR RODRIGUEZ (Barcelona na Granada)

Ametumia misimu 16 katika La Liga. Ni katika uzi ule wa Barcelona alipotwaa mataji matano ya La Liga. Cesar Rodriquez alifunga magoli 213 katika mechi 311. Alikuwa mahiri hasa.

Mzaliwa huyu wa mji wa Leon alifariki Machi 1, 1995 akiwa na miaka 74 katika Jiji la Barcelona. Alichokifanya katika La Liga bado ingali nafasi yake.

 

  1. RAUL GONZALENZ BLANCO (Real Madrid)

Kwa mujibu wa kituo hicho cha utafiti. Kijana huyu kutoka katika mitaa ya San Cristobal de Los, nje kidogo ya Jiji la Madrid ndiye mchezaji bora wa muda wote wa La Liga.

Raul Gonzalenz ametumia misimu 16 katika La Liga akiwa ndani ya jezi nyeupe za Real Madrid. Raul ni mmoja wa wachezaji muhimu katika historia ya Real Madrid. Amefunga magoli 228 katika mechi 550, huku akitwaa mataji sita ya La Liga na matatu ya ubingwa wa Ulaya.

Gwiji huyu nje na ndani ya uwanja alikuwa mfano wa kuigwa. Mpole, mtaratibu na mwenye haya nyingi. Hata hivyo alizaliwa kuwa kiongozi na mmoja wa wachezaji wachache zaidi wenye nidhamu ya ajabu mno.

Raul hajawahi kupata kadi nyekundu mpaka anastaafu. Unaweza kuhesabu kadi zake za njano na zikafikia nusu ya alizokuwa nazo Lionel Messi. Raul ametwaa tuzo mbili za pichichi na nne za Zarra.

Pengine anastahili. Cristiano Ronaldo amekamata nafasi ya 23, huku Iker Casillas, Ronaldinho Gaucho, Ronaldo De Lima, Roberto Carlos wakiwa nje ya 50 bora. Ajabu ilioje!

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here