Home Michezo Kimataifa REAL MADRID ASANTENI, TUTASUBIRI NYAKATI MPYA ZA ZIDANE

REAL MADRID ASANTENI, TUTASUBIRI NYAKATI MPYA ZA ZIDANE

1560
0
SHARE

NA NIHZRATH NTANI

ALASIRI ya Jumatatu ya Aprili 30, 1945. Ni ndani ya eneo la Fuhrerbunker katika mji wa Berlin, nchini Ujerumani. Mlio wa risasi unasikika, ghafla habari kubwa ni kifo cha Adolf Hitler.

Kifo chake kinatajwa kimetokana na kujiua. Pamoja na ubabe wake uliopitiliza, akitajwa ndiye binadamu katili zaidi aliyepata kuishi katika ulimwengu huu.

Kifo cha Adolf Hitler kilihitimisha miaka 12 ya utawala wenye kuzalisha kashkashi, huzuni, mshtuko, machozi na damu miongoni mwa wanadamu wengi duniani, wakiwamo Wajerumani wenyewe.

Aliondoka duniani akiwa na miaka 56, akiacha nyuma simulizi iliyojaa hasira dhidi yake, mazuri yake machache yalifichwa na mabaya yake mengi.

Kifo cha Hitler kilihitimisha mwisho wa utawala wa kimabavu. Hatimaye tabasamu likachanua kwa wananchi wengi siyo tu nchini Ujerumani, bali ulimwengu mzima.

Kuna misemo inayosema, ‘Ngoma ikilia sana mwishowe hupasuka’, ‘Hakuna marefu yasiyo na ncha’.

Kila zama zina mbabe wake, hivi ndivyo unavyoweza kuzungumza baada ya utawala wa Adolf Hitler kumalizika.

ANGUKO LA REAL MADRID LILITARAJIWA

Ni kama mwisho wa utawala wa kidikteta wa Adolf Hitler. Ndivyo tulivyouona mwisho wa utawala wa Real Madrid barani Ulaya.

Ni usiku wa Jumanne ya Machi 5, 2019, utawala wa Real Madrid katika michuano ya Ulaya ulifia katika akili ya kocha wa Ajax, Erik Ten Hag.

Kipigo cha goli 4-1 kutoka kwa Ajax Amsterdam ndani ya dimba la Santiago Bernabeu, tena mbele ya mashabiki wao wapatao 70,000.

Kipigo hicho kilimaanisha kuhitimisha mafanikio ya kutwaa taji hilo mara tatu mfululizo kwa Real Madrid, mwisho wa enzi.

KWANINI REAL MADRID IMEANGUKA?

Kuondoka kwa Zinedine Zidane na Cristiano Ronaldo inaweza kuwa ni sababu? Ndiyo, hapana. Hawa ni watu wawili muhimu katika mafanikio ya kutwaa mataji matatu ya Ulaya mfululizo, hata hivyo, kuondoka kwao si sababu ya kuanguka kwao.

Bado ningali nasisitiza, kumuuza Cristiano Ronaldo kwenda Juventus ulikuwa moja ya uamuzi bora kwa kila upande, Real Madrid ilifaidika na mauzo hayo kwa upande mwingine.

Ukifikiria umri wa Cristiano Ronaldo uliokuwa unakaribia miaka 34 wakati huo, amefanya kila kitu mahali hapo.

Ungekuwa ni wendawazimu kwa Real Madrid kukataa kiasi kilichowekwa mezani na Juventus kwa ajili ya Ronaldo, bila shaka, hakuna klabu iliyofaidi kipaji cha Ronaldo kama Real Madrid.

Kwa upande wa Ronaldo, ulikuwa wakati sahihi wa kuondoka. Hakuna wakati mwingine mzuri kama nyakati zile, ameondoka mahali ambako alikuwa bado anahitajika. Mwisho wa nyakati.

Real Madrid walikosea hapa; Kwanza katika uteuzi wa kocha aliyechukua nafasi ya Zinedine Zidane klabuni hapo na hili linaweza kuwasuta baada ya kurejea tena kwa kocha huyo!

Kuajiriwa kwa Julen Lopetagui ambaye alikuwa muumini wa falsafa ya soka la kuburudisha katika staili ya “tiki taka” kulimaanisha Real Madrid ilikuwa inatoka katika falsafa ya soka lao la kutumia mashambulizi ya kushtukiza, ambalo bila shaka itakuwa ndiyo kazi ya kwanza ya Zidane katika kikosi hicho.

Lopetagui hakuwa kocha sahihi kwa Real Madrid. Anguko la Real Madrid likaanzia hapo. Ghafla Real Madrid wakamteua Santiago Solari.

Huyu naye akaanza kuweka matabaka miongoni mwa wachezaji magwiji wa klabu hiyo, akiwamo mlinzi wa kushoto Marcelo na kiungo maridhawa Isco.

Huku akimtupa benchi Keylon Navas, watatu hawa walikuwa watu muhimu katika kikosi cha mafanikio cha Zinedine Zidane. Kiuhalisia Real Madrid ilishaanza kuanguka tangu msimu uliopita.

Walimaliza nafasi ya tatu kwenye ligi kwa alama 17 nyuma ya Barcelona. Walitolewa na Leganes kwenye kombe la Copa Del Rey. Hawakuwa na msimu mzuri chini za Zidane. Hata hivyo, kutwaa kwao ubingwa wa Ulaya kulificha udhaifu huo.

Sera yao ya usajili ilikuwa sababu nyingine iliyochangia kuanguka kwa Real Madrid. Walipomuuza Cristiano Ronaldo, hii ilimaanisha Real Madrid walimwondoa mchezaji aliyekuwa anawapa zaidi ya mabao 50 kwa msimu.

Katika safu ya ushambuliaji wakabakia Karim Benzema na Gareth Bale. Wawili hawa kwa pamoja hawana uwezo hata wa kufikisha mabao 50 kwa msimu.

Badala yake wakamleta Mariano Diaz kama mbadala wa Cristiano Ronaldo. Hili lilikuwa jambo la kuchekesha.

Madrid ilipaswa kumleta mbadala sahihi kariba ya Ronaldo. Usajili wa washambuliaji Mauro Icardi au Harry Kane ungeweza kuwapa wanachokikosa sasa. Wakabakia wale wale.

Jambo jingine ni kuwa, timu inatakiwa ifumuliwe na kutengenezwa upya. Wachezaji wao muhimu wapo katika umri wa ukingoni mwa soka lao.

Wametwaa kila kitu mahali hapo. Ile hali, morali ya kupigania mafanikio ya mataji ndani ya uzi wa Real Madrid haipo tena.

KIKOSI HIKI CHA DHAHABU NI BUDI KIHESHIMIWE.

Inaweza kuchukua karne au nusu karne nyingine kuja kushuhudia mafanikio ya klabu nyingine kufanya haya waliyoyafanya Real Madrid ndani ya miaka mitatu iliyopita.

Miongoni mwetu hatukuweza kuwashuhudia Real Madrid iliyoitingisha Ulaya katika miaka ya 1956 hadi 1960. Wengineo tunasoma historia kuhusu Ajax na Bayern Munich walipotwaa taji la Ulaya mara tatu mfululizo katika miaka ya 1970.

Ila tangu michuano hii ilipobadilishwa jina mnamo mwaka 1992 hakuna klabu iliyowahi kutwaa taji hili mara tatu mfululizo zaidi ya Real Madrid chini ya Zinedine Zidane.

Tusubiri marejeo ya Zinedine Zidane, aliyeutamanisha umma wa Madrid kurudi kwenye kilele cha mafanikio. Siku zitazungumza.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here