Home Uncategorized Ronaldo na Messi nani anakubalika zaidi kwa mashabiki?

Ronaldo na Messi nani anakubalika zaidi kwa mashabiki?

552
0
SHARE

Ronaldo-MessiHATUA ya kwanza ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya ilianza rasmi jana Jumanne kwa mechi mbili kupigwa, huku nyingine mbili zikitarajiwa kupigwa leo usiku.

Jana kulikuwa na mechi mbili kali ambapo mabingwa watetezi, FC Barcelona walikuwa katika Uwanja wa Nou Camp, kucheza na Wahispania wenzao, Atletico Madrid huku vigogo wa Ujerumani, Bayern Munich wakiwakaribisha Benfica katika dimba la Allianz Arena jijini Munich.

Leo Jumatano pia kutakuwa na mechi nyingine mbili ambapo matajiri wa Ufaransa, Paris St-Germain, wapo kwao jijini Paris, kukipiga na Manchester City ya England, huku Wolfsburg ya Ujerumani ikiwa mwenyeji wa Real Madrid.

Timu hizo zitarudiana tena wiki ijayo kutafuta washindi watakaokwenda kucheza nusu fainali ambapo washindi wawili watakutana katika mechi ya fainali itakayopigwa kwenye dimba la San Siro nchini Italia hapo Mei 28.

Kwa kifupi, hii ndiyo michuano mikubwa zaidi barani Ulaya ngazi ya klabu na inayotazamwa na watu wengi zaidi huku ikikusanya ‘mafundi’ wa kila aina.

Achana na rekodi za timu tofauti tofauti zinazoshiriki michuano hiyo. Achana na viungo wenye uwezo wa kupiga chenga za kila aina na kugawa mipira. Achana na uwezo wa makipa wa timu mbalimbali, kuna watu wawili muhimu sana wanaotazamwa na mashabiki ulimwenguni kote kuona ni vipi watazisaidia timu zao. Hapa nawazungumzia nyota wawili ulimwenguni akina Cristiano Ronaldo na Lionel Messi.

Siku nne tu zimepita tangu wakali hao wawili wakutane katika mechi ya El Clasico iliyopigwa kwenye Uwanja wa Nou Camp huko Barcelona. Katika mechi hiyo licha ya Messi kung’ara katika masuala ya kupiga chenga na kutoa pasi zenye macho, lakini Ronaldo alimfunika kwa kuipigia timu yake bao muhimu la ushindi dakika za mwisho na kuiwezesha Madrid kuibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Tukija kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, mpaka sasa Ronaldo ndiye anayeongoza kwa kupachika mabao kati ya wachezaji wote wa muda wote. Mreno huyo amekwishatupia nyavuni jumla ya mabao 90, huku akiwa ametoa pasi za mwisho 43 wakati mwenzake Messi ana mabao 83 na pasi za mwisho 41. Takwimu zinaongea zenyewe.

Utafiti wa haraka haraka uliofanywa unaonyesha kuwa Messi anaongoza kwa kupendwa na mashabiki wengi zaidi katika nchi za Eritrea ambako ana asilimia 100, Equatorial Guinea (100%), New Caledonia (88%), Bahamas (86%) na nyumbani kwao Argentina (85%).

Ronaldo yeye anaongoza kwa kupendwa na mashabiki wengi zaidi katika nchi za Lithuania (97%), Oman (89%), Kyrgyzstan (82%), Puerto Rico (78%) na Luxembourg (77%).

Nchini Hispania ambako zilipigwa kura 5,261 asilimia 59% walionekana kumkubali Messi huku zilizobaki zikimkubali Ronaldo wakati nchini England, Ronaldo alionekana kukubalika kwa asilimia 63 dhidi ya Messi.

Kwa hapa Tanzania, je, wewe unamkubali nani?

 

MATOKEO SWALI LILILOPITA

Vardy, Kane wanatosha kumuweka benchi Rooney England?

Katika suala hili tulipokea meseji nyingi zikitoa maoni, lakini kwa asilimia kubwa zilisema kuwa Vardy na Kane hawawezi kumuweka benchi Rooney kutokana na mchezaji huyo kuwa na heshima yake ya kipekee kwenye kikosi cha timu hiyo.

Zifuatazo ni baadhi ya meseji za wasomaji wetu katika kuchangia hili.

Kiukweli hata kama atapona majeraha yake, Rooney atakuwa mchezaji wa akiba tu kwani mchezaji huyo hajaisaidia sana timu yake ya Taifa tangu amalize kuichezea, Juma Mohamed.

Prince wa Dar es Salaam, mimi naona Rooney kiwango chake kimeshuka sana tofauti na Vardy.

Naitwa, Babu Dullah wa Miembeni Mtwara, kwa sasa naona zama za Rooney zimefikia mwisho kutokana na vijana wengi wa Kiingereza wanafanya vizuri sana siku hizi na sijaona nafasi yake katika kikosi cha England labda abebwe na kocha tu.

Naitwa Maundi Mustafa wa Mbagala Rangi Tatu, kwa kweli sasa Rooney anahitajika kukaza msuli atakaporejea uwanjani kinyume na hapo ukweli ataishia kusoma namba yake mbele ya Vardy na Kane, la msingi kwake ni kurudisha makali yake kama zamani ila mimi nina imani bado nafasi ya Rooney ipo katika timu ya England lakini akizubaa benchi limamuhusu.

Rashid Kenyabasi wa Kibaha, si kwamba  Rooney hana nafasi katika kikosi hicho, Vardy na Kane na hata akina  Dele Ali na Sterling wana uwezo wa hali ya juu, lakini Rooney bado mchango wake unahitajika kutokana na uzoefu alionao.

Katika mafowadi hao wawili kama Rooney anakuwa mzima hakuna anayeweza kufanya anachofanya  ila kama Rooney hafai kwa sasa basi tu ila watajilaumu kwa yatakayowakuta kwa kumkosa Rooney mimi Dullah wa Mbande.

Mimi Idd Mkindi wa Moshi, kwangu naona huu ni muda wa Rooney kupumzika timu ya taifa apishe sura mpya abaki na klabu yake kwani hana kiwango cha Kane na Vardy wewe unaona atacheza wapi?

Katika wachezaji hao wote hamna mtu ambaye ataweza kumweka benchi Rooney, maana Rooney akipona lazima moto wake urejee kama zamani, naitwa Mohamed Mayuni ‘Chogo’ wa Mnyangara Lindi Vijijini.

Naitwa Rajabu Kiuluti wa Makangaga Kilwa, hivi kwa mawazo yao Vardy, Kane na Dele Alli wanaweza kumweka benchi Rooney? Hizo ni moja ya dharau kuwahi kutokea katika ulimwengu huu wa soka. Maana Rooney anaheshima yake kubwa sana nchini England, nina imani hao vijana wanaweza lakini Rooney akipona mmoja atakaa benchi.

Mimi naona zama za Rooney ndio zimefikia hatima yake, kutokana vijana wengi wa Kiingereza wamekuwa wanacheza soka la hali ya juu sana siku hizi, hivyo nina imani kwa Uingereza Rooney anapotea mimi Said Kilonji wa Mbezi jijini Dar es Salaam.

Acheni masihara Rooney anajua, siyo mtu wa kumfananisha na wachezaji wachanga  kama akina Vardy na Kane, Rooney yupo juu mimi Mathias Canal wa Iramba Singida.

Unapowazungumzia wachezaji ambao wamecheza katika kiwango bora kabisa katika timu ya England huwezi kusita kumzungumzia Rooney ambaye anamaliza rekodi tu za magwiji waliokuwa wanashikilia miaka ya nyuma katika taifa hilo, sasa akina Vardy, Kane pamoja na Dele Alli wana kazi za ziada kufikia mafanikio ya Rooney mimi Mwanahafa Mpima wa Lindi.

Inawezekana Rooney akapotea ila siyo katika muda huu ambao akina Vardy ndio kwanza wanaanza kupata majina kutokana na Rooney hajachuja bado ila majeraha ndio yanamfanya kushindwa kucheza ila akirudi moto utawaka, mimi Ashura Selemani wa Masasi, Mtwara.

Mimi ni Salumu Mohamed wa Tandika, kwangu naona kumtoa Rooney katika watu muhimu kwenye timu ya taifa la England ni kumshushia heshima yake, ndio akina Vardy wanajua ila inabidi wakaze sana kumtoa Rooney katika kikosi cha kwanza.

Rooney bonge la mchezaji na hakuna mtu ambaye anamnyima namba pale England tatizo kubwa alilonalo sasa ni anapitia katika mazingira ya mpito tu ila akipona atarudi kwenye uwezo wake.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here