Home Habari RUFAA YA YANGA YATINGA TFF

RUFAA YA YANGA YATINGA TFF

1744
0
SHARE

NA MAREGESI NYAMAKA,

YANGA wana akili nyingi sana aiseee.  Uongozi wa mabingwa hao watetezi huenda ukawafurahisha mashabiki wao baada ya kumkatia rufaa katika Shirikisho la Soka nchini (TFF) mshambuliaji wa African Lyon, Ludovic Venance, kwamba alichezeshwa kimakosa katika mechi ya mwishoni mwa wiki walipotoka sare ya bao 1-1 na African Lyon.

Wanajangwani hao walijikuta wakiambulia sare hiyo ya bao 1-1 mwishoni mwa wiki dhidi ya African Lyon, katika mchezo uliopigwa  Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam na hivyo kugawana pointi moja moja, lakini sasa kama rufaa yao itakubaliwa watapewa pointi zote tatu.

Katika mtanange huo, Yanga wanadai mchezaji  Ludovic Venance hakuwa mchezaji halali wa African Lyon, kutokana na kutokuwa na leseni ya kuitumikia timu hiyo, ambapo  mwajiri wake halali ni Mbao FC ya mkoani Mwanza,  aliyoitumikia tangu mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo.

Katibu wa Yanga, Baraka Deusdedit, alilithibitishia DIMBA jana kuwa ni kweli wamepeleka malalamiko yao kwa TFF kupinga kitendo cha kuchezeshwa na Ludovic na kwamba wanayo matumaini makubwa kuwa haki itatendeka.

Akizungumza kwa kifupi, katibu huyo alisema: “Ni kweli tumepeleka  barua yetu ya malalamiko TFF tangu Jumamosi, kwani ni mchezaji halali wa Mbao FC na wala si African Lyon.”

Hata hivyo, gazeti hili lilipowasiliana na Ofisa Habari wa Shirikisho hilo, Alfred Lucas, alisema bado hawajaiona barua hiyo kufika mezani kwao, lakini kama Yanga wataifikisha bila shaka itafanyiwa kazi mapema iwezekanavyo.

“Hatujapokea barua ya aina hiyo kutoka Yanga, labda kama walipeleka Bodi ya Ligi, naamini ikifika mahali hapa tutaipokea na kuifanyia kazi, kwani tupo hapa kwa ajili ya kutenda haki,” alisema.

Juhudi za kumpata Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Boniface Wambura, ziligonga mwamba baada ya gazeti hili kupiga simu yake zaidi ya mara tano lakini haikupatikana hewani.

Kwa upande wa Mbao FC, wao walisema kupitia kwa Ofisa Habari wao, Chrisant Malinzi, kwamba wanavyofahamu mchezaji huyo bado ni mali yao na wanashangaa ni kwa nini anaichezea African Lyon.

“Tunavyofahamu sisi Venance bado ni mchezaji wetu halali, tunashangaa alivyoonekana akiichezea African Lyon, tutalifuatilia suala hili,” alisema Malinzi.

Kwa mujibu wa msemaji wa TFF, Alfred Lucas, iwapo suala hilo litafikishwa mezani watalipeleka kwa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ili lifanyiwe kazi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here