Home Habari SAKATA ‘MO’ LATUA KWA RAIS MAGUFULI

SAKATA ‘MO’ LATUA KWA RAIS MAGUFULI

418
0
SHARE

NA CLARA ALPHONCE

KAMA ulifikiri suala la klabu ya Simba kuingia katika mfumo wa hisa linakaribia kwisha, basi sikia hii; Wazee wa klabu hiyo wamelishikia bango suala hilo ili kuhakikisha halitimii baada ya kuandika barua kwa Rais Dk. John Pombe Magufuli, kumuomba asitishe mchakato huo.

Mratibu wa wazee wa klabu hiyo, Felix Makuwa, ameliambia DIMBA Jumatano kwamba, wamemuandikia barua Rais Magufuli, wakiomba kuonana naye ili wamueleze juu ya kundi la watu wachache wanaotaka kuipora klabu hiyo kwa kutumia nguvu za fedha walizonazo.

Makuwa alisema wao kama wazee wa klabu hiyo wanamuomba Rais aingilie kati mchakato huo, kwani umejawa na harufu ya rushwa na tayari kuna uchunguzi unaofanywa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana Rushwa (Takukuru) ili kubaini ukweli.

Itakumbukwa Julai 31 mwaka jana, uongozi wa klabu hiyo uliitisha mkutano Mkuu wa wanachama ambao kwa kauli moja uliridhia kuingia katika mfumo wa hisa kwa kupitisha marekebisho ya katiba.

Maazimio hayo yalizingatia kumrahisishia mfanyabiashara bilionea Mohammed Dewji ‘Mo’ kumiliki hisa za klabu hiyo asilimia 51, huku wanachama wakimiliki 49.

“Tumemuandikia Rais Magufuli barua kupitia kwa Waziri wake wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe kuomba atusaidie kusitisha mchakato huu uliojaa harufu ya rushwa, kwani bado kuna uchunguzi unafanywa na Takukuru na baadhi ya watu wameanza kuhojiwa, akiwamo Rais Evans Aveva,” alisema Makuwa.

“Sisi hatupingi mabadiliko, lakini tunaona jambo hili kwanini linaharakishwa na kundi la watu fulani wenye masilahi nalo, tunajua kwamba fedha zimetumika kuwahonga baadhi ya wanachama ili kutaka Dewji amiliki hisa za klabu,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here