Home Habari SALAMU KWENU AZAM FC

SALAMU KWENU AZAM FC

1256
0
SHARE

NA MAREGESI NYAMAKA

MAZOEZI ya nguvu wanayoyafanya na ari waliyonayo Simba, inatosha kusema kwamba wanatuma salamu kwa Azam FC kuelekea mchezo wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara, unaotarajiwa kuchezwa Jumamosi ya wiki hii Uwanja wa Azam Complex.

Wekundu hao wa Msimbazi watakuwa wageni wa Wanalambalamba hao katika mchezo unaosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa pande zote kila upande ukitamba kuibuka na ushindi.

Simba wanajua kwamba wanakwenda kuchezea Uwanja wa Azam Complex, ambao hawajawahi kuuchezea mchezo wowote wa ligi kuu na sasa wamejipanga kuhakikisha wanawazima wenyeji wao hao wakiwa nyumbani kwao.

Mabingwa hao wa Ngao ya Jamii, jana walijifua vilivyo kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, jioni huku wachezaji wake wakionekana kupania kuibuka na ushindi kutokana na namna walivyoonekana kuyazingatia yale waliyokuwa wakielekezwa na kocha wao mkuu Joseph Omog.

Kivutio kikubwa katika mazoezi hayo ni kutokana na wachezaji waliokuwa wakiichezea Azam FC walivyokuwa wakijituma, hiyo ikiashiria kwamba wanajua wanalo jukumu zito la kuhakikisha wanawapatia furaha mashabiki wa Simba.

Kurejea kwa John Bocco ambaye alikuwa majeruhi na kulazimika kuukosa mchezo wa kwanza dhidi ya Ruvu Shooting, kumelifanya benchi la ufundi kutabasamu hasa kutokana na jinsi alivyokuwa akijituma mazoezini jana akishirikiana na wenzake.

Erasto Nyoni ambaye pia alitokea Azam FC, kama kawaida yake alionyesha utulivu wa hali ya juu anapopata mipira na anakuwa makini kutoa pasi za uhakika, huku pia Aishi Manula naye akifanya yake golini hiyo ikitoa picha tosha kwa mashabiki wa Simba kwamba vijana wao wapo kamili kwa mapambano.

Haruna Niyonzima, kama kawaida yake alikuwa akisambaza mipira kila kona ya Uwanja, huku mshambuliaji wao, mpya Nicholas Gyan, naye akionyesha uwezo mkubwa akishirikiana na akina Shiza Kichuya, Said Ndemla, Mzamiru Yassin na wengine.

Katika mazoezi hayo ambayo yalihudhuriwa na kaimu makamu wa Rais wa Klabu hiyo, Iddi Kajuna, yalianza kwa Omog kuwapigisha kata zito la fiziki na baadaye kugeukia kuuchezea mpira, zoezi ambalo lilifanyika kwa ustadi mkubwa.

Kwa sasa kinachosubiriwa ni akina Emmanuel Okwi pamoja na Jjuuko Murshid, ambao walikuwa na timu yao ya Taifa ya Uganda ‘The Cranes’ kuwasili na kuungana na wenzao kwa ajili ya kuiwinda Azam FC hiyo Jumamosi.

Simba wameianza ligi kwa ushindi wa mabao 7-0 dhidi ya Ruvu Shooting na sasa wanataka kuendeleza wimbi hilo la ushindi, huku Azam nao wakiibamiza Ndanda FC bao 1-0 na wao wakitaka kwenda na mwendo huohuo wa ushindi, kitu ambacho kinaufanya mtanange huo kutabiriwa kuwa mkali.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here