Home Makala Sasa tunasubiri kuuona mwanzo wa mwisho wa Mbappe

Sasa tunasubiri kuuona mwanzo wa mwisho wa Mbappe

1476
0
SHARE

NA AYOUB HINJO

NYAKATI zimekwisha. Hakuna jambo lisilo na mwisho. Miguu ya Cristiano Ronaldo na Lionel Messi, tayari imeanza kutuonesha taa nyekundu japo inawezekana ukajiuliza mbona bado wanaonekana kuwa katika kiwango cha juu.

Ni kama binadamu anapopigania nyakati za mwisho za uhai wake. Hapana shaka, kilele cha soka lake kinaelekea kufika mwisho, mwisho kabisa. Ni huzuni iliyoje!

Ifikapo Februari 5 mwakani, Ronaldo atakuwa anatimiza miaka 35, ametuonesha umahiri wake wa soka kwa miaka 15. Inatosha, lakini katika akili ya staa huyo wa Ureno bado anaamini anaweza kukimbia uwanjani mpaka atakapofika miaka 40.

Wala sipingani naye, ukizingatia mifano ya mastaa waliocheza soka katika umri wao, hivi karibuni alikuwepo Ryan Giggs, aliyetundika daluga zake akiwa na miaka 41, lakini jambo ni moja tu, hakuwa kama alivyokuwa zamani.

Kasi kubwa akitokea pembeni huku akikimbiza mabeki kuanzia mstari wa kati mpaka kwenye lango lao, siku za uzee wake alitengenezewa mazingira ya kucheza kiungo wa kati, eneo ambalo linahitaji akili zaidi kuliko nguvu.

Naye Messi, itakapofika Juni 24 mwakani atakuwa na miaka 33, unadhani tutamwona kama yule aliyekuwa na uwezo wa kukokota mpira kuanzia kwenye lango lake mpaka la wapinzani? Sidhani, itakuwa ajabu.

Itafika mahali ataonekana anawakaba wenzake uwanjani, kwa sababu mwili wake utagoma kwenda sambamba na akili yake, mwisho unakaribia, wala si mbali sana.

Nina hakika baada ya misimu mitatu ijayo, tutaanza kusoma historia zao kupitia kwenye vitabu na kutazama umahiri wao kupitia kwenye ‘santuri’ huku mmoja akiwa mfanyabiashara mkubwa au mwigizaji na mwingine akiwa balozi au kocha. Nyakati zinakwisha.

Kisha kila mmoja wetu tutajiuliza tuliwapatia walichostahili? Ghafla watatuonesha makabati yao na tutaona medali nyingi za mataji mbalimbali ngazi ya klabu na timu ya Taifa, yaliyopambwa na tuzo zao za Ballon d’Or.

Kuna kundi la wachezaji limeibuka hivi karibuni, wapo wengi sana ambao wanatajwa kuja kuziba nafasi za mastaa hao wawili waliocheza kwa kiwango cha juu zaidi ya miaka 10.

Kila mmoja anaamini kile anachokiona kutoka kwa wachezaji hao, ingawa hakuna aliyefanikiwa kucheza kwa kiwango cha juu kwa misimu mitatu mfululizo, wote wanapishana kwa kupeana nafasi.

Hakuna aliyefanikiwa kucheza kwa kiwango cha juu hata kwa michezo 10 tu, watafanya vizuri mitano na mingine watakukera hilo ndilo kundi la wachezaji ambao wapo na wamekuja kwa kasi.

Tangu akiwa na miaka 17, Kylian Mbappe, amefanikiwa kubadilisha uelekeo wa mazungumzo ya soka kwa kuzungumzwa yeye tu.

Kwa sasa ndani ya kikosi cha Ufaransa unaanza kumtaja yeye kisha akina Paul Pogba, Antoine Griezmann wanafuata, amekuwa mkubwa ghafla.

Ndani ya PSG wapo akina Neymar, Edinson Cavani, Angel di Maria na mastaa wengine lakini jina la Mbappe limechomoza juu zaidi ya hao, bahati iliyoje!

Ndiyo, utakapomwona uwanjani, utafurahishwa jinsi anavyojaribu kufanya kila kitu kwa kutumia maarifa na akili aliyobarikiwa.

Lakini ulishajiuliza ni lini tutauona mwisho wa Mbappe? Iko hivi, kwa asilimia kubwa ya wachezaji waliofanikiwa katika umri wake walishindwa kumaliza soka vizuri, itafika mahali mwili wake utachukia soka.

Itafika mahali hatahitaji kukimbia kilomita nyingi wala kugusana na mabeki wa timu pinzani mara kwa mara, mboni ya macho yetu ilianza kumwona Neymar akiwa na miaka 16 ndani ya kikosi cha wakubwa cha Santos huko Brazil.

Februari 5 mwaka huu alitimiza miaka 27, pengine mafanikio makubwa aliyowahi kuwa nayo ni kuingia kwenye kinyang’anyiro cha Mchezaji Bora wa Dunia mwaka 2015.

Sidhani kama ana mafanikio makubwa zaidi ya hayo labda kushinda mataji akiwa na Barcelona na sasa PSG, siwezi kusema kama Neymar hapendi soka lakini soka halimpendi staa huyo, linamkimbia taratibu.

Miaka kadhaa nyuma, Liverpool waliibuka na Michael Owen, aliyekuwa na miaka 16. Alitisha kila alipokutana na mabeki wa timu pinzani, hakuna aliyetamani kukutana naye.

Hata hivyo, wakati akielekea katika umri ambao angecheza soka kwa kiwango cha juu zaidi, alishindwa sababu mwili wake ulikuwa na kila aina ya jeraha, hakuweza kudumu na mwisho wa siku ulimwengu uliishia kusikitika tu.

Miaka nane iliyopita, Arsene Wenger, aliionyesha dunia kipaji kipya, Jack Wilshere, ambaye hivi sasa katika umri wa miaka 27 amekuwa mchezaji wa kawaida sana, yote kwa sababu alikuwa tegemeo akiwa mdogo.

Wakati ule anachipukia alitabiriwa kufanya makubwa lakini tangu hapo ameishia kubadilisha vitanda vya wodi ya wagonjwa tu, yupo West Ham hivi sasa.

Pamoja na ustaa wa Ronaldo, alianza kuwa tishio zaidi kuanzia mwaka 2007 alipokuwa na miaka 21, hakurudi nyuma, alipunguza baadhi ya mambo na kuamua kuifuata ndoto yake.

Licha ya Messi kupewa nafasi akiwa kijana mdogo ndani ya kikosi cha Barcelona, lakini bado hakufanikiwa kuwa tegemeo ndani ya kikosi hicho.

Uwezo wake ulionekana katikati ya wachezaji bora waliomzunguka ndani ya Barcelona, lakini baadaye kidogo kila kitu kiliangukia kwenye mabega yake.

Binafsi nasubiri kuuona mwanzo wa mwisho wa Mbappe huyu ambaye anatajwa kuwa mchezaji bora zaidi chipukizi kwa sasa.

Katika umri wa miaka 19 alifanikiwa kushinda Kombe la Dunia mwaka jana, ni mafanikio makubwa zaidi katika soka, bado tegemeo ndani ya kikosi cha PSG.

Wote tunasubiri kuona kama soka litamchukia Mbappe kama ilivyotokea kwa Neymar, Owen na Wilshere japo ipo mifano mingi zaidi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here