SHARE

NA SALMA MPELI,

TIMU ya Taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys, mwishoni mwa wiki iliyopita ilitolewa kwenye michuano ya Mataifa ya Afrika kwa vijana wa umri huo inayoendelea nchini Gabon.

Serengeti ilitupwa nje ya michuano hiyo baada ya kukubali kichapo cha bao 1-0 dhidi ya Niger, katika mchezo wao wa tatu kwenye Kundi B.

Serengeti Boys imetolewa ikiwa na pointi nne sawa na Niger na wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa, hivyo wapinzani wao wamesonga mbele kutokana na ushindi huo walioupata katika mechi kati yao.

Hivyo kwa matokeo hayo, Niger anafuzu Kombe la Dunia ambalo fainali zake zitafanyika Oktoba mwaka huu, nchini India na pia kwenda nusu fainali ya michuano hiyo.

Niger anaungana na Mali, iliyoongoza kundi hilo kwa pointi saba, baada ya kushindi mechi mbili na sare moja, wakati Tanzania na Angola zote zinatolewa katika kundi hilo.

Mbali na Mali na Niger, timu nyingine zilizofuzu nusu fainali ya michuano hiyo ni Ghana na Guinea kutoka Kundi A, huku Cameroon na wenyeji Gabon wakiaga mashindano hayo pia.

Serengeti walionyesha mwanga wa kufanya vema kwenye michuano hiyo baada ya kufanya vizuri katika mechi zake za kirafiki, ambapo kati ya mechi saba walizocheza, walishinda tano, wakitoka sare moja na kufungwa mechi moja, jambo linaloifanya kuwa na dalili nzuri za kubeba taji hilo.

Ndoto za vijana hao zinaonekana kama zimekatika mapema, baada ya kutopenya kwenye michuano hiyo, lakini sitaki kukubaliana na jambo hilo, kwani vijana hao tayari wamejengewa misingi bora katika soka, hivyo tusikubali kuwapoteza kirahisi.

Isije kuonekana baada ya kutoka Gabon sasa vijana hao wapotee bila kujulikana wameishia wapi na tusione mwendelezo wao.

Timu hiyo iliandaliwa vizuri ili hapo baadaye ije kuwa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 23, Ngorongoro Heroes na hata Taifa Stars ya baadaye, hivyo ikiachiwa hapa ilipo sasa tutakuja kuulizana ilipotelea wapi kutokana na misingi na mikakati ambayo imejengewa.

Kabla ya kwenda Gabon kwenye michuano hiyo, Serengeti Boys ilicheza mechi za kujipima nguvu dhidi ya Burundi mara mbili katika Uwanja wa Kaitaba, Kagera, ambapo waliibuka na ushindi wa 3-0 Machi 30, mwaka huu, kabla ya kuipiga 2-0 mchezo wa Aprili mosi, mwaka huu.

Vijana hao walionyesha ukomavu na upambanaji mkubwa katika mchezo mwingine wa kujipima nguvu uliopigwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam dhidi ya Ghana, baada ya kusawazisha dakika za majeruhi na kuambulia sare ya mabao 2-2.

Baada ya mechi hizo walikwenda mjini Rabat, Morocco, kuweka kambi, baadaye walicheza mechi mbili na Gabon na kuibuka na ushindi wa 2-1, huku mabao ya mechi ya kwanza yakifungwa na Kelvin Nashon Naftali na Ibrahim Abdallah Ally, huku yale ya mchezo wa pili yakiwekwa wavuni na Assad Juma na Abdul Hussein.

Mechi mbili za mwisho ilikuwa dhidi ya Cameroon, ambapo mechi ya kwanza walishinda 1-0, likifungwa na Ally Ng’anzi, kabla ya kurudiana na kuchapwa 1-0.

Kwa matokeo hayo waliyoyapata dhidi ya timu ngumu kama Cameroon na Ghana, inaonyesha wazi kwamba uwezekano wa kufanya vizuri kwenye michuano ya Gabon upo wazi na kuendeleza kauli mbiu yetu iliyokuwa inasema ‘Gabon hadi kombe la dunia’.

Hii ni kutokana na ukweli kwamba, ingefanikiwa kuingia hatua ya nusu fainali, basi ingekuwa imejikatia tiketi moja kwa moja ya kushiriki kombe la dunia baadaye mwaka huu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here