Home Michezo Kimataifa SHARAPOVA ATINGA NUSU FAINALI PORSCHE GP

SHARAPOVA ATINGA NUSU FAINALI PORSCHE GP

282
0
SHARE

STUTTGART, Ujerumani

MCHEZA tenisi raia wa Russia aliyekuwa nje ya uwanja  kwa muda mrefu, Maria Sharapova, ametinga hatua ya nusu fainali ya mashindano ya Porsche GP mara baada ya kumbwaga Anett Kontaveit, anayeshika nafasi ya 73 katika viwango vya ubora kwa wanawake.

Mwanamama huyo mwenye umri wa miaka 30 ambaye ni mshindi wa mataji makubwa duniani maarufu kama ‘Grand Slam’, alimbwaga Kontaveit kwa seti 2-0 za pointi 6-3, 6-4 na kuingia katika hatua hiyo kwa mara ya kwanza tangu alipotoka katika kifungo.

Ulikuwa ushindi wa kuvutia zaidi kwa nyota huyo ambaye  alikuwa na furaha kubwa mara baada ya mchezo  huo uliokuwa mgumu zaidi kwa upande wake kutokana na kuwa nje kwa muda mrefu.

“Nilikuwa mkimya na mwenye umakini  mkubwa na kujiamini zaidi  kutokana na uzoefu wangu, lakini ulikuwa ushindi mzuri kwangu najisikia vizuri sana,” alisema.

“Kila mmoja alicheza kwa  jitihada kubwa ili kuhakikisha anapata ushindi katika mchezo, lakini nashukuru mimi ndiye niliyeibuka na ushindi katika mchezo ule,” anasema Sharapova.

Sharapova jana Jumamosi jioni alitarajiwa kuvaana na Kristina Mladenovic wa Ufaransa katika mechi ya nusu fainali, huku Mromania Simona Halepa akimkabili Laura Siegemund wa Ujerumani katika nusu fainali nyingine.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here