SHARE

NA MARKUS MPANGALA

MASHINDANO ya Olimpiki yamemalizika nchini Brazil. Kwenye mashindano hayo tumejionea mambo mbalimbali ya kimichezo na burudani. Tumeshuhudia ndondi, soka, riadha, kuruka juu na chini, wavu, handball na kila aina ya mchezo.

Kuanzia leo na kuendelea nitazungumzia mastaa mbalimbali walioshiriki michuano ya Olimpiki wakiwa na umri mkubwa. Kwamba kila Jumatano na Jumapili nitakuletea simulizi za wanamichezo mbalimbali walioshiriki huku tukitupia macho Olimpiki ya mwaka 2020. Tutasimulia mastaa waliobamba, wakasifika kwa uwezo, vipaji na ufundi mkubwa.

Ni mastaa wa kweli na wamekuwa kichocheo cha kuibuka kwa wengine kila kona ya dunia. Katika mashindano ya Olimpiki nako kuna wakongwe. Fuatana nami kwenye uchambuzi na huzuni zetu za kishkaji kwa wale tuliowapenda na kuwakaribisha wapya.

Agosti 5 mwaka huu, ndipo michuano ya Olimpiki ilianza rasmi jijini Rio De Janeiro nchini Brazil na kumalizika Agosti 20. Michuano hii inazishirikisha nchi nyingi  na michezo inayoshindaniwa ni mingi.

Wachezaji, viongozi, makocha na maofisa mbalimbali hujumuika kwenye michuano hii. Ni michuano ambayo inafanyika kwenye nchi inayowinda taji la soka la Olimpiki kwa muda mrefu.

Jamaica ni taifa linalosifika kwa mbio fupi. Ivory Coast imechukua nafasi nyingine ya riadha barani Afrika. Wanariadha wake wamekuwa moto kweli kweli. Kenya na Ethiopia wamekuwa wababe zaidi kwenye riadha na wamedhihirisha hilo.

Leo napenda kutoa mkono wa kwaheri kwa mwanariadha ninayempenda kutoka Jamaica. Ni mwanariadha ambaye amenipa fursa ya kumshuhudia kwa mara ya mwisho akiwa kati ya mastaa waliotesa kuanzia mashindano ya Olimpiki ya Beijing iliyofanyika nchini 2008, kisha michuano ya London mwaka 2012 nchini Uingereza pamoja na mashindano mengine ya riadha ya ubingwa wa kimataifa wa IAAF na Diamond League.

Leo namuaga rasmi mwanariadha au mtimua upepo mahiri zaidi wa Jamaika, Shelly-Ann Fraser-Pryce. Nimeona mashindano ya Olimpiki mwaka huu yamegoma kwake, mwili umemkatalia japo akili yake inapenda kuendelea kushindana.

Kwenye mbio za mita 100 alizidiwa maarifa na Mjamaica mwenzake, Elaine Thompson ambaye ni kipaji kipya kabisa kwenye michuano hii akiwa na umri wa miaka 24.

Shelly-Ann Fraser-Pryce, nimemuona akishindana, nimemfurahia na kusisimka kila anapotimua upepo. Ni mwanamke mahiri, ana nguvu, misuli, mrembo, mkakamavu, shupavu na mwenye kipaji cha hali ya juu. Dunia itajivunia kumshuhudia.

Mashindano ya Olimpiki ya mwaka huu yamemkuta Shelly-Ann akiwa na miaka 29 ukiwa ni mwaka mmoja pungufu ya gwiji Usain Bolt. Riadha ni  mchezo niupendao baada ya soka na masumbwi.

Shelly-Ann Fraser-Pryce ni lazima astaafu. Hakuna namna nyingine. Nilivyoona kasi ile na kushika nafasi ya tatu katika mbio za mita 100; moyoni nikajisemea basi tena, kipenzi changu Shelly hana nafasi nyingine.

Olimpiki ijayo yaani mwaka 2020 atakuwa na umri wa miaka 33, katu hataweza kuwa na kasi ileile. Nakupa mkono wa kwaheri Shelly-Ann Fraser-Pryce, ni afadhali Jamaica wameniletea burudani nyingine ya Elaine Thompson, japo yeye hana misuli au ulimbwende kama wako.

Japo ningeweza kukuelezea mrembo Shelly-Ann kuwa ameshiriki Olimpiki mwaka huu akiwa na maumivu ya kidole, jambo ambalo  limechangia kutong’ara kwake huko jijini Rio De Janeiro. Eti wapo rafiki zangu wanakutegemea kukuona ifikapo Olimpiki ya mwaka 2020. Sijui, lakini inatulazimu kumuaga mwanadada huyo na kukaribisha vipaji vipya michezoni.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here