SHARE

NA MICHAEL MAURUS, MOROGORO

KIPA mpya wa Yanga, Farouk Shikalo, ameanza mazoezi jana kwenye Uwanja wa Chuo cha Biblia, Bigwa, baada ya kuwasili mjini hapa juzi jioni, akitokea Dar es Salaam.

Shikalo alichelewa kujiunga na wenzake kutokana na kukabiliwa na michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati ‘Kombe la Kagame’ iliyomalizika wikiendi iliyopita jijini Kigali, Rwanda, akiwa na timu yake ya zamani, Bandari ya Kenya.

Wakati wote alipokuwa akijifua, Shikalo alionekana mwenye furaha, hususan kutokana na jinsi mashabiki walivyokuwa wakimshangilia.

Kwa kuwa alichelewa kambini, Shikalo alifika uwanjani hapo mapema zaidi na kuanza kujifua pamoja na Maybin Kalengo ambaye alikosa mazoezi kwa siku nne kutokana na kukabiliwa na majeraha.

Wawili hao walianza na mazoezi ya kusaka pumzi kwa kukimbia kabla ya kuchezea mpira, huku muda wote Shikalo akionekana kuwa mchangamfu kuonyesha jinsi anavyojiamini.

Baada ya kujifua kwa takribani saa moja na nusu, Shikalo na Kalengo walienda kupumzika kupisha mechi ya kirafiki kati ya Yanga na ATN FC ya hapa ambapo Wanajangwani hao walishinda mabao 7-0.

Mara baada ya mchezo huo, Shikalo, Kalengo na wachezaji ambao hawakuanza kikosi cha kwanza, waliendelea kujifua kuanzia saa tano asubuhi hadi saa sita.

Ujio wa Shikalo unafanya idadi ya makipa wa Yanga kufikia wanne, wengine wakiwa ni Klaus Kindoki, Ramadhan Kabwili na Mechata Mnata.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here