Home Makala BAO LA MKONO: Si Tambwe tu, hata Messi aliwahi kufunga kwa mkono

BAO LA MKONO: Si Tambwe tu, hata Messi aliwahi kufunga kwa mkono

832
0
SHARE

NA NIHZRATH NTANI

JIONI ya Oktoba 1, 2016 nilikuwa na marafiki zangu tukitazama pambano la Simba na Yanga. Ni pambano hili la Simba na Yanga ndio tukio pekee hapa nchini ambalo halina itikadi. Maadui wenye kufanana kwa hisia huwa pamoja. Mke na mume hutengana kwa muda ikiwa tu kila mmoja ana mapenzi tofauti kuhusu timu hizi.

Ni wakati wa familia zenye upendo kugawanyika. Kila mmoja anapigania mapenzi yake kwa timu fulani. Ni tukio hili linalochukuliwa kama tukio kubwa kabisa la soka nchini.

Kuelekea pambano hili siku zote huibuka matukio ya kushangaza mno. Imani za kishirikina hutawala kwa kiasi kikubwa. Ndicho kipindi ambacho wale wanaojiita wataalamu wa ufundi wa sayansi ya giza wanapopata mavuno makubwa kupitia akili zao. Akili za kitapeli. Kwanini wasipige pesa ikiwa nguvu na akili zetu zimeegemezwa uko?

Nani amekuambia kuwa ushirikina katika soka unasaidia? Baada ya kuona vitendo hivyo ghafla nikawaza kuna mikoa na maeneo yanayosifika kwa kukithiri kwa imani za kishirikina. Mikoa kama Tanga, Shinyanga, Pwani hata Sumbawanga. Hii mikoa na maeneo haya si ndio yanasifika kwa imani hizi?

Hivi ziko wapi timu zao zinazoshiriki Ligi Kuu? Kama zilikuwepo je, zilifanya nini? Maswali mepesi majibu mepesi lakini yanachekesha.

Kisha nikaanza kulikumbuka taifa la Nigeria. Hili si ndio Taifa linalosifika kwa imani za kishirikina barani Afrika? Tuachane na kutwaa ubingwa wa dunia je, wamewahi hata kufika robo fainali ya Kombe la Dunia?

Kisha jiulize pesa tunazowapa hawa wataalamu wetu wa benchi la ufundi wasio na vigezo vyovyote katika soka tunafaidika vipi? Hakika tunapoteza muda mno.

Kisha ghafla kumbukumbu za miaka 12 iliyopita. Nilikuwa kijana mdogo wakati huo. Nilikuwa shabiki kweli kweli wa soka letu. Kilikuwa kipindi kigumu mno kwa soka letu hasa migogoro kuanzia klabu hadi Chama cha Soka cha Tanzania. Naam!

Goli la dakika ya 27 lililofungwa na Amissi Tambwe, Jumamosi wiki iliyopita dhidi ya Simba liliibua sekeseke kubwa uwanjani hapo. Picha za marudio ya televisheni zikathibitisha kuwa kabla ya Tambwe kufunga mpira ule mrefu aliutuliza kwa bahati mbaya na mkono, pengine mpira ulifuata mkono.

Refa Martin Saanya hakuona, wasaidizi wake pia hawakuona. Kwa mazingira yale ni ngumu kuona. Raha ya soka siku zote huanzia hapo. Utata katika maamuzi siku zote huamua matokeo.

Ndicho kilichotokea Taifa. Kwa hasira mashabiki wa Simba wakaanza kung’oa viti. Unajiuliza viti vilifanya nini? Iko wapi akili na ustaarabu wa Mtanzania? Unabaki kushangaa tu. Tatizo ni elimu au umbumbumbu wetu? Sina jibu.

Pengine tukio la Tambwe kufunga goli hilo linaweza kuwarejesha nyuma si mimi tu hata Abbas Tarimba, aliyekuwa Rais wa klabu ya Yanga miaka 12 iliyopita. Nimemkumbuka pia Omary Abdukadir refa wa mechi ya miaka 12 iliyopita.

Bila shaka nimemkumbuka pia Rais mstaafu Alhaji Hassan Mwinyi. Tangu nilipomuona uwanjani akiwa mgeni rasmi miaka 12 iliyopita, sijabahatika kumuona tena akiwa mgeni rasmi. Kulikoni?

Mnamo Machi 31, 2002. Inaweza kuwa moja ya siku mbaya kabisa kwa Abbas Tarimba na hao wengine niliowataja. Ilikuwa katika fainali ya michuano ya Kombe la Tusker iliyofanyika katika Uwanja wa Taifa sasa unaitwa Uwanja wa Uhuru, kabla ya huu mpya haujajengwa.

Ilikuwa katika dakika ya 32 wakati mshambuliaji wa Simba wakati huo, Madaraka Selemani ‘Mzee wa Kiminyio’, alipopokea mpira mrefu katikati ya mabeki wa Yanga. Alifanya vile vile kama alivyofanya Tambwe jioni ya Oktoba 1, 2016.

Kisha Madaraka alimtungua kipa Peter Manyika kwa shuti kali, huku mwamuzi Omary Abdukadir akionesha mpira upelekwe kati kuashiria goli halali. Mwamuzi huyo hakuona wakati Madaraka Selemani alipoumiliki mpira kwa mkono kabla ya kufunga goli hilo la pili katika ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Yanga.

Mashabiki wa Simba walibakia wakishangilia kwa nguvu uwanjani hapo, huku wale wa Yanga wakipandwa na jazba kweli kweli. Hata baadhi ya mashabiki wa Simba wenyewe walikiri kuona kitendo kile. Lakini hakukuwa na namna ya kubadili matokeo.

Kukubaliwa kwa goli hilo kulipelekea Rais wa Yanga, Tarimba Abbas, kuonesha ishara ya kuwataka wachezaji wake watoke nje akiwa jukwaa kuu pembeni kabisa na mgeni rasmi, Alhaji Hassan Mwinyi.

Mashabiki wa Yanga walipandwa na hasira na kupelekea vurugu kutokea kwa kitendo hicho cha mwamuzi kukubali goli la Madaraka Selemani. Chupa zenye mikojo na maji zikaanza kurushwa kuelekea jukwaa kuu wakati huo Tarimba hakuwepo mahala hapo.

Mashabiki walijaribu kuonesha hasira zao za kupinga maamuzi ya mwamuzi. Mwishowe waliendelea na mechi na kukubali kipigo cha aibu cha mabao 4-1.

Siku chache baada ya tukio hilo, Abbas Tarimba, alikuja kufungiwa na chama cha soka cha wakati huo kikiitwa FAT sasa TFF, kutojihusisha na soka kutokana na kitendo chake hicho.

Huo ukawa mwisho wa kumuona Alhaji Hassan Mwinyi viwanjani. Na ndio ulikuwa mwanzo na mwisho wa kutamba kwa mwamuzi, Omary Abdukadir, aliyekuwa anainukia kipindi hicho.

Bila shaka utata kama wa Tambwe, Madaraka Selemani si matukio ya kwanza kutokea katika soka. Ni mambo ya kawaida kutokea. Tambwe hakufunga kwa mkono. Nani anakumbuka goli maarufu la Diego Maradona linaloitwa ‘Goli la Mkono wa Mungu’, Maradona alifunga kwa mkono kabisa. Na refa alilikubali.

Si hao tu. Jumatano ya Novemba 18, 2009, Thierry Henry, alitoa pasi kwa mkono na kumpa mfungaji kufunga goli muhimu kabisa mwishoni mwa mchezo dhidi ya Jamhuri ya Ireland. Dunia nzima iligubikwa na huzuni. Lakini hakuna aliyejali. Ireland walikuwa wanaelekea kupata tiketi ya kufuzu michuano ya Kombe la Dunia 2010. Kwa tukio hilo Ufaransa wakafuzu.

Matukio ya utata ni mengi sana hata Raul Gonzalez akiichezea Real Madrid alifanya hivyo dhidi ya Leeds katika michuano ya mabingwa Ulaya, akifunga kwa mkono goli la tatu ambalo lilikuwa la ushindi.

Hata Lionel Messi pia amefanya hivyo dhidi ya Espanyol katika ‘Catalan Deby’. Alifunga goli la mkono. Ni Jumapili tu ya Oktoba 2, 2016 tumeshuhudia beki wa Arsenal, Laurent Koscielny, akifunga goli lililotokana na kutulizwa na mkono dhidi ya Burney. Hakuna kiti kilichovunjwa.

Wakati mwingine waamuzi wetu nao ni binadamu kama sisi. Hatuwezi kuwalaumu kwa tukio kama hilo. Kwa kasi ya mpira ule ilikuwa ngumu kuanza kumlaumu refarii au mwamuzi msaidizi namba moja.

Ni wakati sasa wa kubadili hisia zetu, kutazama upya ustaarabu wetu na kujifunza kupitia kwa wenzetu. Je, kung’oa viti ni suluhisho?

Tuachane na huu uwendawazimu usio na faida. Mwisho nimeikumbuka ile methali ‘muosha huoshwa’.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here