SHARE

EZEKIEL TENDWA NA HUSSEIN OMARY,

KAMA ulidhani Kocha Mkuu wa Yanga, George Lwandamina aliposema analihusudu soka la Barcelona la pasi nyingi na za uhakika anatania, basi tenga muda wako uende ukachungulie mazoezi ya wanajangwani hao ujionee kitu anachokifanya Mzambia huyo.

Wakati wa utambulisho wake makao makuu ya klabu hiyo alisema analihusudu soka la miamba hao wa nchini Hispania, kwani lina pasi nyingi za uhakika na wachezaji wanapopoteza mpira kwa umoja wao hung’ang’ana kuurudisha, kitu ambacho anataka kitokee Yanga.

Sasa ipo hivi, kocha huyo alianza kibarua chake mwanzoni mwa wiki hii katika Uwanja wa Polisi jijini Dar es Salaam na kile ambacho alikisema kinaanza kutokea kutokana na soka linalochezwa na wachezaji.

Siku ya kwanza ya mazoezi Jumatatu hakuwa na kazi kubwa, kwani ilikuwa ni kama utambulisho ambapo kocha msaidizi, Juma Mwambusi ndiye aliyekuwa akiwapa mazoezi hayo wachezaji, huku Lwandamina akifuatilia akiwa na mtangulizi wake, Hans van der Pluijm.

Kwa ujumla siku hiyo ya Jumatatu ambayo ilikuwa ya kwanza kwa Lwandamina kuonana na wachezaji wake ilikuwa kama siku ya utambulisho na Jumanne ndipo alipoanza kuwanoa vijana wake, akiwapa mbinu mbalimbali.

Kikubwa alichokuwa akikifanya Lwandamina ni kuwajengea stamina wachezaji wake pamoja na kuwafundisha namna ya kufanya mashambulizi kwa kushtukiza, zoezi ambalo lilionekana kuwaingia haraka wachezaji kwenye vichwa vyao.

Siku ya tatu ambayo ilikuwa ni Jumatano, Lwandamina alianza kuwafundisha wachezaji wake namna ya kupiga pasi fupifupi na za uhakika, huku wakitakiwa kuhakikisha wanaunasa mpira haraka sana pale wanapoupoteza, zoezi ambalo pia lilifanyika kwa ukamilifu.

Zoezi hilo liliendelea siku ya Alhamisi, ambapo aliongeza pia lingine la kucheza mipira mirefu na jambo la kufurahisha ni kwamba, kila mchezaji alionekana kufurahia mazoezi hayo, hata wale waliokuwa wakisugua benchi chini ya Pluijm wakionekana kuanza kuiva vizuri.

Siku ya Ijumaa Lwandamina aliendelea na mbinu zake hizo ambapo hata baadhi ya mashabiki waliohudhuria mazoezi hayo yaliyofanyika Gymkhana, walisikika wakisema kuwa kama wachezaji watazingatia mafunzo hayo, ni wazi hakuna timu itakayowasumbua mzunguko wa pili na hata michuano ya kimataifa.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa Ufundi wa Yanga, Hans van der Pluijm, amesema anafanya mipango ya kutafuta timu kutoka nje ya nchi ambayo itacheza na kikosi hicho mchezo wa kirafiki kabla ya kuanza kwa mzunguko wa pili ili Lwandamina awapime vijana wake.

“Ni kweli ninaandaa mchezo wa kirafiki kabla ya mzunguko wa pili kuanza, lakini kwa sasa siwezi kukuambia tutacheza na nani,” alisema mtaalamu huyo kwa kifupi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here